Home Makala THAMANI YA SAMATTA NI SH BIL 10.5

THAMANI YA SAMATTA NI SH BIL 10.5

7612
0
SHARE
Voetbal voorronde Europa League 515357 KRC Genk Brondby Doelpunt 10 Mbwana Ally Samatta SAMAGOAL

NA ISIJI DOMINIC

TIMU nne za Ligi Kuu England zimetajwa kuwania saini ya mshambuliaji raia wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta, anayekipiga katika timu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji maarufu Jupiler League.

Samatta ameanza msimu vizuri ambapo mabao yake saba yameiwezesha Genk kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 26 na ndiyo timu pekee miongoni mwa 16 inayounda Jupiler League ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja.

Tayari msimu huu Samatta amefunga hat-trick mbili, moja katika ligi na nyingine kwenye michuano ya Ligi ya Europa. Hat-trick yake katika mechi ya ligi aliifunga Septemba 29 mwaka huu, Genk ikiipacha Waregem 4-0 huku ile ya Ligi ya Europa ilikuwa Agosti 23 mwaka huu dhidi ya Brondby ya Denmark ambao Wabelgiji hao walishinda 5-2.

Haishangazi kuona kasi aliyoanza nayo Samatta msimu huu imeanza kuwashawishi hususan timu za England kuwinda saini yake. Gazeti la Daily Mirror la England limetaja timu zinazomwania nahodha huyo wa Taifa Stars kuwa ni Everton, West Ham United, Burnley na Brighton and Hove Albion.

Hakuna mshambuliaji katika hizo timu nne ambaye hadi sasa msimu huu amemfikia Samatta kwa idadi ya mabao na hii huenda ikawa sababu kwanini wanahitaji huduma ya Samatta. Anayeongoza kupachika mabao katika timu ya Brighton ni Glenn Murray aliyefunga mabao matano huku Gylfi Sigurdsson na Richarlison kila mmoja akiwa amefunga mabao manne ndio vinara wa kucheka na nyavu timu ya Everton.

Marko Arnautovic na mabao yake manne akiichezea West Ham United na Ashley Barnes wa Burnley ambaye amefunga mabao mawili hadi sasa, wote hawa hawajafikia mabao saba ya ligi tu ambayo amepachika Samatta.

Takwimu zinaonyesha Samatta ambaye alijiunga na Genk msimu wa 2015/16, amecheza jumla ya mechi 94 za ligi kuu akifunga mabao 33 na hajawahi kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Idadi ya mechi za Ligi ya Europa alizocheza ni 25 akifunga mabao 12.

Samatta aliyejiunga na KRC Genk akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ambao walivutiwa na kipaji chake wakati anakipiga Simba, alikuwa anawindwa na Levante inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania maarufu La Liga wakati wa dirisha la usajili kuelekea msimu wa 2018/19.

Kwa mujibu wa ‘Cadena Ser’ ambayo ni moja ya vituo vya redio Hispania, Levante ilikuwa inapigana vikumbo na moja ya timu kutoka Ujerumani inayoshiriki Bundesliga. Japo timu hiyo haikutajwa, vidole vilikuwa vinanyooshewa Borussia Monchengladbach, Borussia Dortmund na Mainz.

Taarifa kutoka Genk zilisema wapo tayari kumwachia Samatta kuondoka endapo Levante watatoa kiasi cha Euro milioni nne (sawa na shilingi bilioni 10.5). Nahodha huyo wa Taifa Stars alihamia Genk akitokea TP Mazembe kwa ada ya uhamisho wa Euro 800,000 (sawa na Sh. bil 2).

Ni dhahiri habari za Samatta kutakiwa na timu za England kwasasa ni gumzo hata huko Cape Verde ambako Taifa Stars itawakabili wenyeji wao keshokutwa katika mchezo wa Kundi L kufuzu Kombe la Afrika 2019, zitakazofanyika nchini Cameroon.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here