Home Makala Thomas Mashali aliaga dunia akiulilia mchezo wa masumbwi

Thomas Mashali aliaga dunia akiulilia mchezo wa masumbwi

449
0
SHARE
Thomas Mashali

NA MWANDISHI WETU,

ILIKUWA ni simanzi kila kona, baada ya kuthibitika kwamba habari zinazosambaa kuhusu bondia mashuhuri nchini, Thomas Mashali, ni za kweli.

Kilichozidisha huzuni katika tukio hilo, ni aina ya kifo chake kilichotokea ghafla, huku tasnia ya masumbwi ikiwa bado inamhitaji.

Hakika mchezo wa masumbwi nchini umepata pigo kubwa, Mashali atabaki kukumbukwa milele.

Siku chache kabla ya kifo chake alipata wasaa wa kuzungumza mengi yanayohusu maisha na mchezo wenyewe wa ngumi, hata hivyo, sauti yake leo inapata uwakilishi tu, kwani haiwezi kusikika tena.

Licha ya kucheza ngumi za kulipwa, lakini jitihada za bondia huyo zilikuwa wazi, kwani kwa kipindi kifupi tayari alikuwa ameshatwaa mikanda tofauti, ikiwemo ya WBF, IBF, UBO, UBO na Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, IBF na WBF.

Mbali na kushikilia mikanda yote hiyo, Mashali pia alikuwa na rekodi ya kipekee ya kumtwanga mbabe Francis Cheka, ambaye aliwatesa mabondia wengi wenye majina makubwa hapa nchini.

Ilikuwa kama vile anajua nini kinamsogelea katika maisha yake, maana alionekana akiwa ana neno la kuzungumza pale alipowaalika waandishi wa gazeti hili na kufanya nao maongezi.

Siku hiyo alizungumza mengi kuhusu maisha yake ya ndani na nje ya ulingo, ikiwemo yale wanayoishi mabondia wenzake pamoja na mipango yake ya hapo baadaye.

Kwa mara ya kwanza Dimba lilifunga safari mpaka wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani alikokuwa ameweka kambi kujiandaa na pambano lake dhidi ya bondia raia wa Malawi, Chimwemwe Chiota, lililotarajiwa kupigwa mkoani Morogoro.

Mashali aliyasema haya kabla ya kukutwa na umauti: “Mabondia wengi wanaishi maisha magumu. Wanashindwa kutimiza ndoto zao kwa kukosa usimamizi  mzuri. Nayaomba makampuni makubwa yatuangalie na huku pia kwenye suala la udhamini.”

Baada ya mchezo wa ngumi kupoteza mpambanaji wao, wadau pamoja na viongozi wa mchezo huo hapa nchini wameyazungumzia mambo mbalimbali aliyowahi kuyafanya marehemu enzi za uhai wake.

Wamboi Mangore, Katibu Mkuu DABA

Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Ngumi za Ridhaa Mkoa wa Dar es Salaam, Wamboi Mangore, alisema taifa limepoteza mpiganaji mahiri mwenye rekodi nzuri katika mchezo huo.

Alisema, Mashali alikuwa mfano wa kuigwa kwa chipukizi na ataendelea kukumbukwa kwa mengi, ikiwemo uwezo wake mzuri aliokuwa akiuonyesha pindi awapo ulingoni.

“Ataendelea kukumbukwa na wanamasumbwi. Rekodi zake zitaishi milele,” alisema.

Francis Miyeyusho

“Ni pigo kubwa sana kwangu, kwani Mashali na mimi tulikuwa kama ndugu kutokana na ushauri aliokuwa ananipa kuhusu mchezo wa ngumi.

“Hakika ‘gym’ ya Lazima Ukae imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na moja kati ya nguzo muhimu sana. Alikuwa kiongozi na mshauri mzuri mazoezini.

“Tulikuwa na mpango wa kubadili jina la ‘gym’ yetu kutoka jina la Lazima Ukae hadi kuitwa Lazima Uige, lakini lengo limeshindikana kutimia, inaniuma sana.

“Apumzike kwa amani Mashali,” alisema.

Ibrahim Twaha

Bondia huyu ni mmoja wa chipukizi wanaofanya vizuri katika ndondi hivi sasa, alisema hataweza kumsahau Mashali kwa mazuri yake mengi aliyomfanyia, ikiwemo kumpa ushirikiano wa kutosha katika kipindi kigumu alichopitia.

“Mchezo wa ngumi umempoteza mtu muhimu sana, ambaye alililetea taifa sifa kubwa kutokana na ushindi wake wa mapambano mbalimbali aliyopigana nchini na kujulikana kimataifa.

“Alinishauri na kunikanya pale nilipokosea, kwangu alikuwa zaidi ya mwalimu,” alisema.

Francis Cheka

Mkali huyu alisema kuwa, atamkumbuka Mashali kwa mengi, ikiwemo mapambano yao mawili waliyokutana ambapo yeye alishinda pambano moja na anaamini kuwa yalikuwa ni mapambano bora zaidi kuwahi kutokea hapa nchini.

Cheka alisema, ulingo wa ndondi umepoteza mtu muhimu sana. Atakumbukwa kwa mchango wake.

“Sitamsahau Mashali kirahisi, kwa kweli kifo chake kimenigusa mno,” alisema.

Kaike Siraju

Promota huyu alisema: “Mashali alitegemewa kucheza pambano lake Desemba 26 mwaka huu, mkoani Morogoro, lakini kazi yake Mola haina makosa.

“Tanzania ina mabondia wengi wenye uwezo, lakini uwezo wa Mashali ulikuwa wa kipekee zaidi. Alikuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wanaochipukia,” alisema.

Anthony Luta

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa (PST), Anthony Rutta, alisema kuwa Mashali atabaki kuwa bondia bora zaidi kuwahi kutokea hapa nchini katika kizazi hiki.

Alisema kuwa, kabla mauti hayajamkuta, aliamua kufuata nyayo za wakongwe wengine maarufu ulimwenguni, kama Mohamed Ali na Mike Tyson, ambao pia walibadili dini mara baada ya kuachana na mchezo wa ngumi.

“Alibadili dini na kuitwa Mohammed kutoka jina lake la mwanzo la Thomas Mashali. Alituelezwa kwamba aliamua mwenyewe kwa hiari yake kuwa Muislamu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here