Home Habari TSHISHIMBI APEWA MAJUKUMU 3 MAZITO YANGA

TSHISHIMBI APEWA MAJUKUMU 3 MAZITO YANGA

462
0
SHARE

tshishimbi
NA JESCA NANGAWE

KIUNGO Kabamba Tshishimbi ameanza rasmi kujifua na kikosi cha Yanga, kwenye mazoezi yaliyofanyika jana katika Uwanja wa Gombani, mjini Pemba, ambapo amepewa majukumu matatu mazito kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, pamoja na michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga walifanya mazoezi yao jana asubuhi na Tshishimbi alikuwa mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri eneo la katikati, hiyo ikimaanisha kuwa, lile pengo la Haruna Niyonzima limeshaanza kuzibwa vilivyo.
Tshishimbi, raia wa DRC, ambaye alitua kambini Pemba juzi mchana, alianza mazoezi na wenzake asubuhi ya jana na leo anatarajiwa kuuwasha moto wakati kikosi chao kitakapowakabili timu ya Jamhuri ya Pemba, katika mchezo wa kirafiki.
Katika mazoezi hayo, Tshishimbi alionekana kufanya vizuri zaidi, akitoa pasi za uhakika, huku akionekana kana kwamba alikuwa na wenzake kwa muda mrefu, kutokana na jinsi walivyokuwa wakielewana.
Baada ya mazoezi hayo ya jana asubuhi, kigogo mmoja wa Yanga aliliambia DIMBA, kwamba, moja ya majukumu ambayo Tshishimbi amepewa ni kuwasahaulisha mashabiki habari ya kuondoka kwa Niyonzima, aliyetimkia Simba.
Jukumu la pili alilopewa Tshishimbi, ni kuhakikisha anaisaidia safu ya ushambuliaji kupata matokeo mazuri kama ilivyokuwa kwa Niyonzima, ambaye alikuwa akiwapa msaada mkubwa akina Donald Ngoma na Amis Tambwe.
Pia alielezwa umuhimu wa kihistoria wa mpambano wa watani wa jadi unavyokuwa na presha kubwa, hivyo ametakiwa kuhakikisha anatuliza akili, asije kubabaishwa na kelele za aina yoyote kutoka majukwaani na badala yake apige kazi kutokana na maelekezo ya benchi la ufundi.
“Amepewa majukumu mazito sana kuhakikisha anawasahaulisha mashabiki habari ya Niyonzima, aliyekwenda Simba, pia moja ya majukumu yake ni kuisaidia safu ya ushambuliaji kupata mabao mengi kadri inavyowezekana na pia kushusha presha linapokuja suala la mpambano dhidi ya Simba,” alisema kigogo mmoja wa Yanga.
DIMBA lilimtafuta kocha msaidizi, Shadrack Nsajigwa, kumzungumzia mchezaji huyo, ambapo alishauri atafutwe Kocha Mkuu, George Lwandamina, ambaye hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumza.
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, kiungo huyo ataanza kuonekana leo mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Pemba, hivyo mashabiki wao watapata fursa ya kumuona.
“Kiwango cha Tshimbimbi nadhani kocha mkuu ndiye ana nafasi kubwa ya kukielezea, baada ya kumtumia kwenye mazoezi yake, lakini pia leo mashabiki watapata nafasi ya kumuona tutakapocheza na Jamhuri,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here