Home Habari TSHISHIMBI ASHUSHA VIFAA VIWILI YANGA

TSHISHIMBI ASHUSHA VIFAA VIWILI YANGA

0
SHARE

NA JESSCA NANGAWE

KIUNGO wa Yanga, Pappy Kabamba Tshishimbi, ameuambia uongozi wa klabu hiyo kwamba, anao uwezo wa kuwaonyesha sehemu wanapoweza kwenda kuwachomoa mastraika wa maana kama Donald Ngoma na mwenzake, Amis Tambwe, hawatapona haraka.

Unaambiwa Tshishimbi ameutonya uongozi wa klabu hiyo kuwa ana uwezo wa kuiletea timu hiyo mastraika ambao watailetea timu faida, hiyo ikimaanisha kwamba, kama mabosi zake watakubali, unaweza ukawa mwisho wa Ngoma na Tambwe.

Mmoja wa vigogo wa klabu hiyo alilitonya DIMBA kuwa, Tshishimbi amewaambia huko anakotoka aliacha wachezaji wenye kujua kazi yao wanapokuwa uwanjani, hivyo anaweza akafanya mpango wa kuwakutanisha na kumalizana.

“Aliulizwa akasema yeye anaweza akatuletea wachezaji wazuri, hasa kwenye safu ya ushambuliaji, hivyo kazi iliyobakia ni uongozi kumruhusu, lakini ukweli ni kwamba, kwa sasa tunahitaji kusajili kutokana na wachezaji wetu muhimu kama Ngoma na Tambwe kuwa majeruhi.

“Haijawa rasmi sana, lakini ametuhakikishia tu kwamba kuna mastraika ambao wana uwezo wa kucheza ndani ya klabu yetu na tunalifuatilia hilo kwa karibu sana, ikizingatiwa kuwa michuano ya Kimataifa inakaribia,” alisema kigogo huyo.

Alisema kama dili hilo litatiki, Ngoma na Tambwe watafungashiwa kila kilichochao, kwani msimu huu wanaonekana kutokuwa fiti, tofauti na misimu mingine, huku akimtaja Ngoma kama mchezaji msumbufu.

“Hapa lazima tuseme tu ukweli kwamba kama tutawapata washambuliaji wazuri, hatutakuwa na namna nyingine ya kumtumia Ngoma na Amis Tambwe, kwani wanaonekana msimu huu hawapo vizuri sana.

“Kubwa zaidi ni huyu Ngoma, ambaye anajiona kama Mungu kwenye Klabu yetu kutokana na kufanya kila analolitaka yeye, kwa mfano sasa hivi yupo kwao Zimbabwe na aliondoka bila kuaga, lakini wakati huohuo utamsikia akidai mshahara, sasa nani atakubali kubakia na mchezaji kama huyu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here