Home Habari TSHISHIMBI: BADO NIPO SANA YANGA

TSHISHIMBI: BADO NIPO SANA YANGA

7107
0
SHARE
MWAMVITA MTANDA NA CLARA ALPHONCE      |

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba, kiungo wao fundi, Kabamba Tshishimbi, ameamua kuweka bayana hatima yake akidai yeye bado ni mali ya Wanajangwani hao na kama kuna timu inammezea mate lazima wafuate taratibu.

Tshishimbi ameamua kuweka wazi suala hilo baada ya kuhusishwa na Azam FC, kwamba huenda msimu ujao akaungana na straika wa zamani wa Wanajangwani hao, Donald Ngoma.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Tshishimbi alisema taarifa kwamba Azam FC wanamhitaji, anazisikia  mitaani na kwamba yeye hawezi kujiamulia mwenyewe na badala yake Yanga ndio wenye mamlaka kwa sasa kutokana na mkataba alionao.

“Unajua mimi bado ni mchezaji halali wa Yanga kwani ninao mkataba, hivyo kama kweli Azam watanihitaji, ni lazima wakazungumze na uongozi wa timu yangu, siwezi kujiamulia mwenyewe.

“Nadhani wakienda kuzungumza na uongozi wa Yanga, wanaweza kupata majibu sahihi kwa sababu wao ndio wananimiliki kwa sasa, zaidi ya hapo hakuna kitakachoendelea,” alisema.

Pia Tshishimbi alisema mbali na taarifa hizo za kutakiwa na Azam FC ambazo hata hivyo anazisikia juujuu, ipo timu nyingine kubwa nchini kwao Kongo ambayo imeonyesha nia ya kumsajili lakini amewaambia lazima wakutane na Yanga.

“Kuna timu nyingine kutoka kwetu Kongo nayo inanihitaji, lakini nimewaambia wazungumze na uongozi wa Yanga. Mkataba wangu na Yanga uliobakia ni mwaka mmoja hivyo wanaonihitaji lazima wafuate taratibu,” alisema.

Taarifa ambazo DIMBA Jumatano ilizinasa zinadai kwamba, Azam FC wamemtengea Tshishimbi Sh milioni 80 ili kuinasa saini yake na kwamba baada ya kuona imekuwa ngumu, wakapanda mpaka wakafikia milioni 90.

“Azam FC wamemwambia Tshishimbi watamuongezea dau lifikie Sh milioni 90, hiyo fedha ni kubwa sidhani kama Yanga wanaweza kumpa na ukiangalia awali yeye alisajiliwa na Yanga kwa Sh milioni 30 kwa mkataba wa miaka miwili.

“Kama unakumbuka Tshishimbi aliwaandikia Yanga barua akitaka kupewa mishahara yake yote anayodai ya miezi mitatu, ila ngoja tusubiri mana katika kipindi cha usajili mengi yanazungumzwa,” kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo, kauli ya Tshishimbi kwamba wanaomhitaji wakakutane na Yanga ni kama imewakata maini Azam FC, kwani vyovyote itakavyokuwa Wanajangwani hao hawawezi kumruhusu kiungo huyo aondoke ikizingatiwa kuwa wanakabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here