SHARE

Na Mwandishi Wetu

WAWAKILISHI wawili, katika michuano ya kimataifa Simba na KMC zimemaliza mbio zao mapema na sasa tunahitaji nguvu kwa timu mbili zilizobaki, Yanga na Azam FC.


Simba na Yanga zinawakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam na KMC wao walipangwa katika kinyang’anyiro cha Kombe la Shirikisho.


Kutolewa kwa Simba katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa taifa Jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita kwa kiasi kikubwa kumeonyesha kupunguza ari ya mashabiki kufuatilia michuano hiyo.


Kutokana na klabu hiyo kongwe kuwa na mashabiki wengi nchini, kwa kiasi kikubwa msisimko nao umepungua na hivyo kubaki kundi la mashabiki wa Yanga tu na wale wachache wa Azam FC.


Sisi Dimba kuna mambo mawili ya muhimu tunayoyaona yakiendelea katika timu hizi mbili kongwe Simba na Yanga.


Kwa upande wa Simba, hakuna siri kwamba mashabiki wake wameonyesha kukata tamaa, hasa kutokana na timu yao kiutolewa katika hatua za awali, ilihali msimu uliopita walifanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.


Kadhalika mashabiki hao bado wanapata wasiwasi juu ya kikosi chao ambacho licha ya kusajiliwa kwa gharama kubwa, lakini hakijaonyesha mabadiliko yanayolingana na hadhi yake, kiasi cha baadhi yao kuwakumbuika wachezaji walioachwa msimu uliopita.


Kana kwamba haitoshi upande wa Yanga licha ya kuwa na matumaini ya kushinda na kuendelea kufurahia mwenendo wa timu yao, lakini nao wanakosa imani ya moja kwa moja, kwani kikosi chao hakijaonyesha makali hasa yanayotoa matumaini ya moja kwa moja.


Sisi Dimba tunatoa rai kwa timu hizi zinazosonga mbele, Azam FC na Yanga zijipange vya kutosha, zikitambua jukumu zito la kuiwakilisha nchi kimataifa.


Pia Simba ni vizuri sasa wakasahau yaliyopita na kujipanga upya na kurejea kwenye ligi, ambayo inahitaji mshikamano wao na umoja.
Vilevile tunaiombea kila la heri Azam ambao wameonyesha dhamira ya kupigana kufa na kupona, ili kuona wanafika mbali katika uwakilishi wao huo Caf.


Ni wakati wetu mashabiki na wadau wa soka kuyaacha majina ya timu hizi na badala yake kuziona zote ni mali ya Tanzania, ili dua zetu tuzielekeze kwao bila kujali itikadi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here