Home Michezo Kimataifa TULIZA PRESHA Pengo la Hazard litazibwa namna hii pale Chelsea

TULIZA PRESHA Pengo la Hazard litazibwa namna hii pale Chelsea

3630
0
SHARE

LONDON, England

ILIKUWA ni furaha isiyo kifani kwa mashabiki wa Chelsea waliposhuhudia timu yao ikikabidhiwa taji la Europa kufuatia ushindi mnono wa mabao 4-1 walioupata dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Arsenal.

Lakini, ndani ya muda mfupi tangu watangazwe kuwa mabingwa wa michuano hiyo ndugu na ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mashabiki hao waliokuwa anga ya saba kwa furaha, walirudishwa duniani haraka sana.

Mtu mmoja tu aliyeweza kuibadilisha furaha ya mamilioni ya mashabiki wa Chelsea duniani kote ni Eden Hazard, ambaye baada ya kufunga mabao mawili katika fainali hiyo, alitangaza kwamba ataachana na klabu hiyo.

Siku kadhaa tangu alipothibitisha kuondoka kwake, Hazard alitangazwa rasmi mwishoni mwa wiki hii kuwa ni mchezaji mpya wa klabu ya Real Madrid.

Kuna wale wenye mioyo midogo wameshindwa kuzuia hisia zao na kueleza wazi jinsi walivyosikitishwa na uhamisho huo, lakini haikuwazuia kumtakia kila la kheri Mbelgiji huyo katika timu yake mpya aliyoenda.

Hazard aliitumikia Chelsea kwa muda wa miaka saba, akifanikiwa kunyakua mataji sita makubwa yakiwemo Europa (2), Kombe la FA, Kombe la Ligi na mataji mawili ya EPL.

Kiujumla, winga huyo anastahili pongezi kwa kile alichoifanya Chelsea katika muda wote huo na pia, aliiheshimu na kuonesha busara kubwa katika muda wote huu ambao ulitawaliwa na tetesi.

Sasa jukumu limebaki kwa Chelsea kutazama maisha ya mbele yatakuwaje bila ya Hazard. 

Ukubwa wa pengo hilo ukoje?

Kama kuna mchezaji wa EPL ambaye wengi walikuwa hawamwelewi basi ni Hazard. Achana tu na umuhimu aliokuwa nao Chelsea, lakini kuna baadhi hawakutambua mchango mkubwa aliokuwa nao hasa msimu uliomalizika wa 2018/19.

Chelsea bila Hazard isingeweza hata kuingia ‘top four’. Tazama idadi ya mabao waliyofunga EPL, 63, wakashika nafasi ya sita kwa takwimu za mabao mengi kwenye ligi, lakini kwa ‘top six’ walishika mkia.

Katika takwimu hiyo, Hazard alihusika chini ya nusu ya mabao yote. Alifunga 16 na kutoa asisti 15, takribani asilimia 49.2 ya mabao yote yaliyofungwa na Chelsea kwenye EPL.

Timu pekee iliyoifuatia Chelsea kwa kumtegemea mchezaji mmoja EPL ilikuwa ni Leicester City, ambayo straika wao, Jamie Vardy alihusika kwa asilimia 43.1 ya mabao yote.

Ukweli uliopo ni kwamba Hazard kuwa mchezaji tegemeo ni suala la kawaida kulingana na uwezo mkubwa alionao, sasa anapoondoka ni lazima klabu iingie kwenye matatizo makubwa.

Ni wazi Chelsea itahitaji mbadala wake apatikane haraka, iwe ni ndani ya kikosi au nje (usajili) kutokana na kwamba Hazard hajaacha wachezaji wengi wa kuisaidia timu hiyo zaidi ya Pedro aliyemaliza msimu na mabao nane, asisti mbili.

Chelsea itahitaji mchezaji atakayesimama na kuvaa viatu vya Hazard haraka iwezekanavyo, si katika EPL tu, pia kwenye michuano mingine ambako winga wao huyo alifanya makubwa msimu uliopita.

Ukijumlisha mabao aliyofunga EPL na katika makombe mengine waliyokuwa wakiyagombania, Hazard bado anaacha rekodi nzito, akihusika kufunga mabao 21 na asisti 17 (jumla 38).

Wanaomfuatia Mbelgiji huyo ni straika, Olivier Giroud na Pedro ambao kila mmoja alihusika katika mabao 21, wakipitwa mabao 17 na Hazard!

Bado haijaishia hapo, vipo vitu muhimu ambavyo Hazard huvifanya akiwa uwanjani na wakati mwingine huwa havizungumzwi sana, lakini havitakiwi kuchukuliwa poa.

Katika asisti zake 15 alizotoa EPL, winga huyo pia aliweza kutengeneza nafasi nyingi za mabao kupitia mashambulizi ya wazi kuliko mchezaji yeyote (80), akimpiku winga mwenzake wa Chelsea, Willian mwenye 31.

Chukua na takwimu ya nafasi alizotengeneza kupitia mipira ya kutenga, Hazard (98) alipitwa kidogo sana na kiungo mshambuliaji wa Leicester City, James Maddison (100), wawili hao walifuatiwa na Willian (77).

Kabla ya kutengeneza nafasi ya kufunga bao kuna kitu kinaitwa uwezo wa kumtoka mpinzani iwe kwa chenga hasa unapokutana naye ana kwa ana, kitu ambacho kilikuwa ni cha kawaida mno kwa Hazard alivyokuwa EPL. 

Hadi msimu ulivyomalizika, Mbelgiji huyo alimaliza na takwimu ya kuwatoka wapinzani mara 138, hakuna mchezaji aliyeweza kumfikia. Ni Pedro tu ambaye alimkaribia (takribani mara 100).

Huyo ndiye Hazard ambaye Chelsea wamempoteza, sasa watalizibaje pengo lake, hilo ndilo swali la msingi.

Mosi, bila kusajili

Chelsea wana uhitaji mkubwa wa kuingia sokoni ili waimarishe kikosi chao na hasa mbadala wa Hazard, lakini ukweli mchungu ni huu; wapo hatarini kupigwa rungu (rasmi) la kutosajili mchezaji wa aina yoyote.

Kwa sasa wamesimamishwa kusajili kwa muda wa miaka miwili, baada ya kukiuka kanuni za usajili wa vijana. Klabu hiyo ilikata rufaa ambayo hata hivyo ilikataliwa na FIFA.

Licha ya kwamba wamedhamiria kuipeleka rufaa yao katika mahakama ya usuhuluhishi wa masuala ya michezo (CAS), inaelezwa kwamba adhabu yao bado itaendelea kuwa hai.

Na kama CAS watawasaidia Chelsea, klabu hiyo itabidi ianze kufanya mipango ya usajili wa msimu ujao, hapa watatazama ndani ya kile walichonacho, mastaa waliopo na wachezaji watakaorudi kutoka kwenye mkopo.

Tuseme Chelsea labda itabaki na kocha wao, Maurizio Sarri, ina maana wataendelea na muundo ule ule wa 4-3-3 wakiwa na timu ile ile iliyowapeleka UEFA huku ikiwa na taji la Europa. Ingawa tayari imetajwa kwamba kocha huyo ataondoka wiki ijayo.

Kiujumla, Chelsea haitakuwa na mabadiliko kwenye safu ya ulinzi, wataweza kumtumia kinda wao, Reece James katikati, halafu Cesar Azpilicueta atarudi beki ya kulia, hiyo ni kuelekea msimu wa 2020/21.

Safu ya kiungo nayo haitarajiwi kubadilishwa sana na wachezaji watakaorudi kutoka kwenye mkopo au watakaotoka akademi, ikiwa na maana kwamba N’Golo Kante, Jorginho na Ruben Loftus-Cheek (akiwa fiti) wataendeleza gurudumu.

Kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita, Loftus-Cheek alionesha ukomavu hasa katika jukumu la kushambulia alipokuwa akitumiwa upande wa kushoto wa safu hiyo ya viungo wa Sarri.

Winga ya kulia inatarajiwa kuwa na nguvu ya ziada kutoka kwa usajili mpya wa Januari mwaka huu, Christian Pulisic ambaye aliachwa Borussia Dortmund kwa mkopo, bado ni mdogo na ana kasi.

Ujio wa Pulisic utaifanya Chelsea iwe na makali katika winga zote mbili, kwani Mmarekani huyo ni mzuri linapokuja suala la kuwatoka wapinzani.

Msimu uliopita wa Bundesliga alikuwa na wastani wa kufanikiwa kuwatoka wapinzani mara 4.1 kwa kila dakika 90, pia akitengeneza nafasi kwa wastani wa 1.37 kila dakika 90.

Mbele kabisa, tunaweza kuiona sura mpya ingawa si ngeni kwa mashabiki wa Chelsea, huyu ni kinda anayekipiga kwa wababe waliorejea EPL, Aston Villa, kwa mkopo, Tammy Abraham.

Abraham anatarajiwa kuanza kupata nafasi ya kucheza msimu ujao, licha ya kuongezewa mkataba kwa straika Mfaransa, Olivier Giroud. Nafasi pekee inayobaki ni ya Hazard na uzuri wanaye mchezaji mwenye sifa zake.

Callum Hudson-Odoi. Huyo ndiye kinda ambaye iwapo atapewa uhuru wa kucheza soka lake na kusahau tabu aliyoipata msimu uliopita, kabla ya kuonesha makali yake mwishoni hasa kwenye Ligi ya Europa. 

Hudson-Odoi aliumaliza msimu uliopita kwa mabao matano na asisti tano ndani ya mechi 24 na aliweza kuanza kwenye mechi nne mfululizo za EPL kabla ya kuumia.

Ana kipaji cha hali ya juu, udhaifu wake ni kutotimiza vyema majukumu ya ulinzi, lakini Chelsea wanatakiwa kujivunia sana kuwa na Hudson-Odoi kwani anao uwezo wa kuvaa viatu vya Hazard akiwa fiti.

Kama wataruhusiwa, watasajili hivi

Suala la adhabu kupunguzwa kama sio kufutwa kabisa ni ndoto kwa mashabiki wa Chelsea. Lakini, iwapo ikatokea ‘wakasamehewa’, ni wazi watatumia fedha za Hazard kunasa nyota wakali sokoni.

Zipo ripoti zinazodai kuwa Chelsea wanamfuatialia Philippe Coutinho ambaye yuko mbioni kuondoka Barcelona. Wanadhani huyo ndiye mrithi wa Hazard.

Tangu atue Camp Nou mwaka jana, Coutinho ameshindwa kuonesha kiwango alichotabiriwa na wengi huku akiwa amesajiliwa kwa fedha nyingi mno.

Licha ya kupotea kwake, Coutinho si mchezaji wa kuchukuliwa poa. Ana kipaji cha hali ya juu, anachokihitaji ni kupata timu ambayo atafanya kazi yake kwa uhuru mkubwa kama alivyokuwepo Liverpool.

Nikitazama timu ambazo zitamfaa Coutinho, siioni zaidi ya Chelsea ambayo imetoka kumpoteza mchezaji wao bora zaidi.

Itakumbukwa kuwa, Coutinho wa msimu wa 2017/18 kabla ya kuhamia Barca alikuwa amefunga mabao saba na kutoa asisti sita katika mechi 14 alizoichezea Liverpool msimu huo. 

Kama hiyo haitoshi, aliweza kutengeneza nafasi za mabao 40 na kufanikiwa kuwatoka wapinzani mara 39. Iwapo atacheza kwenye mfumo sahihi, Coutinho ataweza kuifanya kazi ya Hazard vizuri kabisa.

Lakii, thamani yake inatajwa kuwa kubwa. Coutinho hataondoka Barcelona bila pauni milioni 140, hivyo kama Chelsea wataihitaji saini yake watajikuta wakimsajili yeye tu hivyo Giroud au Abraham kupewa jukumu la kuongoza safu ya mashambulizi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here