Home Makala Tusimlazimishe Mzee Mwinyi atengue kauli, tujitafakari

Tusimlazimishe Mzee Mwinyi atengue kauli, tujitafakari

1517
0
SHARE

NA ABDULAH MKEYENGE

SIMBA wamekufa bao 5-0 tena nyingine kutoka kwa Al Ahly. Haishtui sana. Muda mrefu tumeamua kuujenga mpira wetu katika njia ya kushindwa si kushinda. Hizi 5-0 walizokutana nazo pale Alexandria na zile 5-0 za kule Kinshasa ilistahili.

Tunacheza mpira mwingi katika vyombo vya habari. Huko tunajisifia sana. Tunawajaza ‘ujinga’ wachezaji wetu. Wanauvaa ‘ujinga’ tuliowavalisha. Wanaamini wao ni mastaa wakubwa kumbe si lolote.

Hatuchezi mpira halisia ambao wenzetu wa AS Vita, Al Ahly na timu nyingine wanaucheza. Katika mazingira haya ungetarajia kitu gani kwa Simba kule Congo na pale Misri? Tumejichagulia njia ya kuishi katika mpira.

Muda mrefu soka letu limekuwa na simanzi juu ya upatikanaji matokeo katika michuano ya kimataifa. Lakini hatujawahi kujali wala kujiuliza kipi kinachotumaliza. Kila timu inaishi kivyake. Hakuna utambulisho wa aina yetu ya soka.

Kikubwa tulichonacho ni kuchekana. Hivi sasa Yanga wanayacheka matokeo ya Simba na kuna muda Simba watakuja kuyacheka matokeo ya Yanga. Haya ndiyo yamekuwa maisha yetu.

Baada ya kujitazama ya nini cha kufanya ili kuupandisha mpira, kila uchwao tumekuwa tukimfuata Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, atengue kauli yake juu ya soka la Tanzania kuwa sawa na kichwa cha mwendawazimu.

Kila mmoja kujifunzia. Kwa Mzee Mwinyi ni kama tumegeuka wachungaji wa ng’ombe wanaotumia nguvu kubwa kumswaga ng’ombe aende mtoni kunywa maji wakati hana kiu.

Tunachokisahau ni kwamba, ng’ombe akiwa na kiu haitaji kuswaga ayafuate maji yalipo. Mwenyewe ataongoza mtoni, atakunywa maji na mara moja atarudi zizini.

Ndani ya michezo miwili, Simba wamefungwa mabao 10. Walifungwa na AS Vita ya Congo mabao 5-0, wakafungwa na Al Ahly ya Misri mabao 5-0. Mashabiki Simba wamefura hasira.

Hawana imani na kocha wao Mbelgiji, Patrick Aussems. Wapo wanaomlaumu kocha. Wapo wanaowalaumu wachezaji. Wapo wanaowalaumu viongozi. Mpaka sasa hawajui wamlaumu nani zaidi. Kipigo ni kama kimewapagawisha.

Siku tutakayoacha kuzitumia kalamu zetu kwa kusifiana na kuwaandikia ukweli Watanzania, ndiyo unaweza kuwa mwanzo wa soka letu kuamka. Lakini kwa sasa acha tuishi kwa kusaidiana maisha.

Soka letu liko chini sana. Ni watu wachache wanaoujua ukweli wa hili. Wengi wanaamini wachezaji wetu wana uwezo wa kucheza sehemu yoyote ile, kitu ambacho si kweli. Kuna mabadiliko makubwa yanatakiwa kufanyika.

Tuna kundi kubwa la wachezaji wasiojitambua. Wengi wao hawajajengwa kuja kuwa wacheza mpira. Sasa wanapokuja kuwa wachezaji na wanasajiliwa na timu kubwa wanakengeuka na starehe. Wanalala kumbi za starehe, wanatoroka kambini na kwenda disko.

Huko disko wanataka kutembea na kila msichana mrembo anayekatisha mbele ya mboni zao, lakini kwa mchezaji aliyejengwa tangu chini, kwake inakuwa gumu kumwona akiyafanya haya wanayofanya mastaa wetu.

Muda huu ambao Simba imefungwa mabao 10 katika michezo miwili na mashabiki wake hawamjui mchawi wao nani na watu wengine wakitumia nguvu kubwa kumtaka Mzee Mwinyi atengue kauli yake, tukae tu kimya na tusaidiane maisha.

Siku tutakayoamua kukaa chini na kulijua tatizo letu, Mzee Mwinyi hatotaka shinikizo la mtu ili atengue kauli yake, mwenyewe atatokeza na kuitengua, lakini si hivi sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here