Home Habari UBINGWA SIMBA BADO SIKU 7 TU

UBINGWA SIMBA BADO SIKU 7 TU

8299
0
SHARE
NA EZEKIEL TENDWA   |  

KAMA Simba wataibuka na ushindi leo watakapowakabili Ndanda FC, watatakiwa kusubiri kwa siku saba watakapocheza na Singida United na hapo wakishinda moja kwa moja watatangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba ambao wapo kileleni wakiwa na pointi 62, leo watakuwa wenyeji wa Ndanda FC katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na wenyewe wamejiapiza kushinda kwani wanajua wamebakisha pointi tano tu kutwaa ubingwa.

Licha ya kwamba wamebakisha michezo minne kukamilisha ligi, wenyewe wamesema wanataka kumaliza kazi katika michezo miwili iliyopo mbele yao ambayo ni huu wa leo dhidi ya Ndanda na dhidi ya Singida United, siku saba zijazo.

Mchezo huo kati ya Simba na Singida United, utachezwa Jumamosi ya wiki ijayo Uwanja wa Namfua na kama Wekundu hao wa Msimbazi watapata matokeo mazuri, sherehe zao za ubingwa zitaanzia mkoani humo.

Kocha mkuu wa kikosi hicho, Mfaransa Pierre Lechantre, ameliambia DIMBA kwamba vijana wake wapo kamili na wameahidi kupambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri leo na pia mchezo dhidi ya Singida United.

“Malengo yetu tangu mwanzo ni kutokupoteza mchezo wowote na hilo linaonekana dhahiri kutaka kutimia, jambo kubwa ni kwamba vijana wangu wapo vizuri na wameahidi kuwapa raha mashabiki wao.

“Najua kwamba pointi tano tu zinaweza kutupa ubingwa, hivyo tumejipanga kuhakikisha hilo linatimia, lililopo mbele yetu ni kupambana japo michezo hiyo haitakuwa rahisi sana kwani hata wenzetu wanataka ushindi kama sisi tunavyotaka,” alisema.

Akizungumzia mchezo wa leo, Mfaransa huyo alisema Ndanda ni moja ya timu ngumu na mbaya zaidi kwao wanapambana ili wasishuke daraja, hivyo mchezo hautakuwa rahisi lakini ana uhakika wa kuzoa pointi zote tatu.

Katika mchezo huo wa leo, Simba itaendelea kuwategemea zaidi washambuliaji wake hatari, Emmanuel Okwi anayeongoza akiwa amepachika mabao 19 pamoja na John Bocco mwenye mabao 14, ambaye anashika nafasi ya pili kwenye orodha hiyo ya wafungaji bora.

Mbali na mchezo huo dhidi ya Ndanda na ule dhidi ya Singida United, michezo mingine ambayo Simba wamebakiwa nayo ni dhidi ya Kagera Sugar, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na wa mwisho ukiwa dhidi ya Majimaji unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Majimaji mkoani Songea.

Katika michezo hiyo minne, Simba wanatakiwa kutafuta pointi tano tu ili wafikishe jumla ya pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote ikiwamo Yanga ambao wana michezo sita mkononi.

Hata hivyo, Wekundu hao wanaweza kutwaa ubingwa Jumatano iwapo Yanga itapoteza mechi yake dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here