Home Habari UBINGWA YANGA JASHO NA DAMU

UBINGWA YANGA JASHO NA DAMU

492
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

YANGA wameyaondoa kabisa mawazo yao kwenye michuano ya FA, ambayo bingwa wake anaiwakilisha nchi Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kufungwa na Mbao FC, na sasa wanatakiwa kuzitumia dakika 450 kwa jasho na damu kuhakikisha wanalitetea taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wanajangwani hao, ambao walikuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo ya FA, walijikuta wakifungwa na Mbao bao 1-0 hatua ya nusu fainali, mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na sasa fainali wanaingia Simba na Mbao.

Hiyo inamaanisha kwamba, tayari Yanga wameshajitoa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa kitu pekee kinachoweza kuwafanya washiriki kimataifa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo kwa sasa inaelekea ukingoni.

Katika msimamo wa ligi Yanga wanashika nafasi ya pili, wakiwa na pointi 56, nyuma ya wapinzani wao wa jadi, Simba, wenye pointi 59, na kitu pekee kinachoweza kuwapa ubingwa Wanajangwani hao ni kuhakikisha wanashinda michezo yao yote iliyobakia.

Simba, ambao wapo juu ya msimamo wamecheza michezo 27, wakibakiwa na michezo mitatu, huku Yanga wao wakiwa wamecheza michezo 25, wakibakiwa na michezo mitano mkononi, sawa na dakika 450 ambazo wakizitumia vizuri wataendelea kujiita ‘Wakimataifa’.

Kama Yanga watashindwa kuzitumia vizuri dakika hizo 450 na kuwaacha Simba kutwaa ubingwa, itamaanisha kwamba Wanajangwani hao watashindwa kushiriki michuano ya kimataifa na kuwaacha watani zao hao na Mbao kupeta, bila kujali matokeo yatakayopatikana mchezo wa fainali wa Kombe la FA.

Michezo hiyo mitano, ambayo ni sawa na dakika hizo 450 walizonazo Yanga, ni dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo utakaochezwa mwishoni mwa wiki hii Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Kagera Sugar, Mbeya City, pamoja na Toto African pia ikichezwa Uwanja wa Taifa na ule dhidi ya Mbao FC, utakaochezwa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Wakati Yanga wao wakibakiwa na michezo hiyo, kwa upande wao Simba, wana michezo mitatu, sawa na dakika 270, ambayo ni dhidi ya African Lyon, Stand United pamoja na Mwadui FC, lakini hata wakishinda yote itabidi waombe wapinzani wao hao wa jadi wateleze.

Kocha wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, George Lwandamina, ameshaweka wazi kwamba kilichoko mbele yake ni kuhakikisha wanashinda michezo yote, japo hawezi kutabiri nini kitatokea, kwani haya ni mapambano.

“Siwezi kuwa mtabiri kwamba nini kitatokea mbele, lakini ijulikane wazi kwamba, tunapambana kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu, hilo ndilo ninaloweza kusema,” alisema kocha huyo asiye na maneno mengi.

Kutokana na timu hizo kushikana mashati kwenye kinyang’anyiro hicho, huenda bingwa akaamuliwa kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, ambapo kama itafikia hatua hiyo, Yanga wanaweza wakapeta, kwani safu yao ya ushambuliaji ina mabao mengi na ina uchu wa kufunga tofauti na Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here