Home Maoni UDHAMINI KCB UONGEZE TIJA LIGI KUU

UDHAMINI KCB UONGEZE TIJA LIGI KUU

6817
0
SHARE

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), juzi lilipokea Sh mil. 420 kutoka benki ya KCB kwa ajili ya udhamini wa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Udhamini huo umekuja katika kipindi ambacho timu zitakazoshiriki michuano hiyo zitaongezeka kutoka 16 hadi 20, hivyo kuongeza mahitaji ya ziada ya udhamini.

Kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, fedha hizo zitaelekezwa zaidi katika kuimarisha soka la vijana, kwa timu zitakazocheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sisi Dimba tunathamini udhamini huo, kwa vile tunajua ndio utakaoboresha michuano hiyo na pia kuandaa vizazi vijavyo vitakavyoendeleza mchezo huo.

Mara nyingi tumekuwa tukiandika maoni yanayoshinikiza kupatikana kwa wadhamini wengi zaidi kwa ajili ya kuboresha Ligi Kuu, kwa sababu tunajua jinsi michuano hiyo inavyokosa ushindani wa dhati kutokana na ukosefu wa fedha.

Tunadhani udhamini huu na ule utakaohusisha kampuni nyingine zitakazofuata utaziweka timu zote 20 katika mazingira mazuri ya kushiriki michuano hiyo.

Sisi Dimba tunatoa rai kwa kampuni nyingine zione umuhimu wa kujitokeza na kudhamini michuano hiyo, kwani nafasi bado zipo na mahitaji kwa sasa ni makubwa.

Tunajua kwamba katika kipindi hiki ambacho soka linaendeshwa kisasa, mchezo wa soka umekuwa nafasi nzuri ya kujitangaza na wanaofanya hivyo kupata manufaa makubwa.

Ni imani yetu kwamba, timu zitakazonufaika na udhamini huo uliokamilika na mwingine utakaofuata zitapambana kufa na kupona kuhakikisha zinafanya vizuri na huo utakuwa ndio wakati wa mafanikio ya kuiboresha ligi yetu, ili iweze kutoa wachezaji bora wa timu ya taifa na pia kupata wawakilishi wenye sifa na uwezo wa kutuwakilisha katika michuano ya kimataifa.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here