Home Habari UHAKIKA…Klopp ajibu mapigo ya Sarri, atamba kuiangamiza Chelsea leo

UHAKIKA…Klopp ajibu mapigo ya Sarri, atamba kuiangamiza Chelsea leo

1378
0
SHARE

MERSEYSIDE

LIGI Kuu ya England imefika patamu, leo katika Uwanja wa Anfield, Liverpool watakuwa wenyeji wa Chelsea ambao wamedhamiria kuharibu sherehe za ubingwa ili kuweka matumaini ya kuingia ‘top four’ hai.

Liverpool wanaongoza Ligi Kuu ya England kwa pointi 82 baada ya kucheza michezo 33, wakifuatiwa na Manchester City ambao wanazo 80 na mechi 32 pungufu ya mchezo mmoja dhidi ya vinara hao.

Mechi hiyo imekuwa na presha kubwa kwa timu zote mbili, Liverpool wanapambana kwa ajili ya kushinda taji la Ligi Kuu ya England baada ya miaka 29 kupita huku Chelsea wakihitaji ushindi ambao utawahakikishia kumaliza ndani ya timu nne za juu.

Hata hivyo, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, amekuwa na matumaini makubwa ya kuvunja mwiko wa kutopata ushindi dhidi ya Chelsea katika michezo saba iliyopita ndani ya Uwanja wa Anfield.

Lakini kocha huyo raia wa Ujerumani, alizidi kusema kuwa Liverpool ni timu bora kwa sasa, anaamini kiwango chao cha hivi karibuni kinaweza kuwapa matokeo ya ushindi dhidi ya vijana hao wa Maurizio Sarri wa Chelsea.

“Mara zote wamekuwa wakitusumbua na kutupa ushindani mkubwa, lakini kwa sasa naamini tuko katika kiwango kizuri cha kuweza kushinda mchezo huo.

“Chelsea wana wachezaji wa viwango vya juu, tutapambana kuhakikisha hatufanyi makosa kwenye ulinzi lakini uhakika wa kutumia nafasi uwe mkubwa zaidi,” alisema Klopp.

Timu hizo zimekutana mara 181, huku Liverpool wakishinda mra 77, Chelsea wakifanya hivyo mara 63 na michezo 41 ikimalizika kwa sare.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here