Home Michezo Kimataifa UJIO WA SALAH UMEONGEZA BALAA ANFIELD

UJIO WA SALAH UMEONGEZA BALAA ANFIELD

376
0
SHARE

LIVERPOOL, England

SIMU ya Jose Mourinho ilitosha kubadili kila kitu kwenye mawazo ya Mohamed Salah wakati ule yupo timu FC Basel, ambayo ilimpa dhamana ya kutumia miguu kuwapa matokeo.

Kabla simu ya Mourinho haijaingia kwa Salah, akili ya mchezaji huyo ilibeba mawazo ya kuitumikia timu ya Liverpool, lakini ni mchezaji gani anaweza kukataa kuwa chini ya Mourinho?

Kwa wakati ule Liverpool ilikuwa chini ya Brendan Rodgers, akili ya Salah ilitosha kupima uwezo wa makocha hao, kisha kufanya maamuzi ya kujiunga na Chelsea, ambako alishindwa kuonyesha uchawi wake wa FC Basel.

Unadhani Mourinho alikuwa hajui miguu ya Salah inavyofanya kazi? La hasha, aliogopa sumu ambayo Rodgers alikuwa akiitengeneza pale Merseyside kwa wakati ule angesumbua sana.

Mzani wa Mourinho hauwezi kuwa sawa na Rodgers, sababu ni makocha wawili tofauti ambao wana malengo tofauti mwisho wa msimu unapofika. Mourinho ni mshindi mara zote, ndiyo maana ushawishi wake kwa wachezaji ni mkubwa sana, tofauti na Rodgers.

Historia ya Rodgers haina tofauti na David Moyes wakati yupo Manchester United, jamaa alishindwa kushawishi wachezaji kujiunga na timu hiyo, sababu hakuwa kocha wa daraja la juu ambaye amefanya kazi kubwa kwenye dunia ya mpira, hususan kwenye kushinda mataji.

Mwishowe Salah aliishia kuvaa koti kubwa kama mchezaji wa akiba kwenye kikosi cha Chelsea, lakini mwishowe alifanikiwa kuvaa medali ya Ligi Kuu ya England, ambayo hakuitolea jasho.

Liverpool sasa ina mwanamume ambaye akitoa sauti kila mmoja anasikiliza kilichosemwa. Kila mmoja anamwangalia Jurgen Klopp kama mwarobaini kwenye timu hiyo.

Miaka mingi imepita bila timu hiyo kubeba kombe la Ligi Kuu. Miaka zaidi ya 20 ni mingi sana kwa timu kariba ya Liverpool kushindwa kubeba kombe hilo ambalo ni heshima kubwa ndani ya England.

Tangu Klopp aingie kwenye timu hiyo ameonyesha mwanga ambao unaleta matumaini kwa mashabiki wa Liverpool, ambao wanaamini huu unaweza kuwa wakati wao wa kufutwa machozi.

Jaribu kufikiri timu ambayo Klopp anaisuka pale Liverpool. Fikiria kwa undani zaidi kisha iangalie ile Borrusia Dortmund alivyoitengeneza wakati ule.

Msingi mkuu wa Klopp ni kucheza soka la kasi ambalo uhakika wake ni kufunga magoli mengi kila nafsi zinapotengenezwa. Wajerumani wenyewe wanamuita mfalme wa Gegen-pressing.

Falsafa yake hiyo alianza nayo vizuri Liverpool, lakini mwishoni mwa msimu walionekana kuchoka, sababu inahitaji kucheza kwa nguvu nyingi na kasi muda wote.

Roberto Firmino, Philippe Coutinho, Adam Lallana na Sadio Mane ni wachezaji wa Liverpool ambao walisimama imara katika safu ya ushambuliaji ya Liverpool na kusababisha misiba kwa timu pinzani.

Kuongezeka kwa Salah kunaonyesha jinsi gani Klopp amedhamiria kumaliza ligi mapema tu kama walivyofanya Chelsea, ambao waliongozwa na safu kali ya ushambuliaji.

Liverpool hawana safu nzuri ya ulinzi, anachokifanya Klopp ni kutengeneza nguvu kwenye safu ya mashambulizi ambayo mwisho wa siku itaamua matokeo hata kama wataruhusu magoli mawili au matatu.

Pia msimu ujao Liverpool watashiriki michuano ya klabu bingwa Ulaya. Ujio wa Salah utatoa machaguo mengi kwa kocha huyo ili kuweza kuwakabili wapinzani kwa mtindo atakaoutaka.

Majeruhi aliyopata Mane yalionyesha jinsi gani timu hiyo kutoka Merseyside ilikuwa na mapungufu makubwa katika safu ya ushambuliaji. Kwa wakati husika walimkosa mtu muhimu ambaye aliweza kuamua matokeo karibu kila mchezo.

Ujio wa Salah utaleta ahueni kwa Liverpool hata watakapomkosa Mane au Coutinho au hata Firmino, sababu ni mchezaji ambaye anamudu kucheza kwa ustadi mkubwa eneo la ushambuliaji akitokea pembeni au katikati.

Salah atatukumbusha Borrusia Dortmund ya Klopp ambayo ilikuwa na wachezaji hatari ambao waliweza kuipa matokeo timu hiyo muda wowote pindi walipokwama.

Hata Liverpool inaelekea kuwa na sura hiyo, ambayo inatengenezwa na Klopp. Kitu pekee unachoweza kutofautisha kwao labda tabia za wachezaji ni tofauti kidogo, licha ya uwezo karibu kufanana.

Marco Reus, Robert Lewandowski, Ilkay Gundogan, Shinji Kagawa, hata Mario Gotze ni wachezaji ambao waliifanya timu hiyo kutisha na kuogopeka na wapinzani, sababu ni wachezaji ambao walikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kuamua matokeo.

Ubovu mwingine ambao Klopp anaufanyia kazi kwenye kikosi cha Liverpool ni aina ya wachezaji ambao wanahitajika. Kitu pekee ambacho kiliipa ubingwa Chelsea ni kikosi kipana kilichojaa wachezaji bora.

Kwa Liverpool ilikuwa na wachezaji wazuri wa kikosi cha kwanza tu, tofauti na wale waliokuwa wakikaa kama wachezaji wa akiba na mwisho wa siku walikosa kitu cha ziada chenye ulazima kwa timu kutoka kwa wachezaji hao wa akiba.

Wakati ule Salah alikuwa sahihi kuikimbia Liverpool na kuihusudu simu ya Mourinho, lakini sasa yupo kujiunga na Liverpool ya Klopp.

Miguu yake iliyojaa dharau na uwezo wa hali ya juu imeingia sehemu sahihi iliyo na ubongo wa ‘gegen-pressing’ kutoka kwa Klopp, hata shujaa wa timu hiyo, Billy Shankly atakuwa amekubaliana na usajili huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here