Home Chombezo UKIONA DALILI HIZI, UJUE HUNA MPENZI TENA

UKIONA DALILI HIZI, UJUE HUNA MPENZI TENA

9854
0
SHARE

Na Joseph Shaluwa          |       


UMUHIMU wa mapenzi upo palepale, hata kama yatageuka sumu kwako, lakini bado una nafasi ya kufanya marekebisho katika sehemu uliyokosea ili kuweka mambo sawa na maisha yaendelee kama kawaida.

Inawezekana upo katika uhusiano unaodhani ni imara sana, lakini siku moja unakuja kugundua kuwa mpenzi uliyenaye hakuwa na mapenzi ya kweli kwako, alikuwa akikutumia kwa ajili ya kujistarehesha mwili wake tu, hakuwa na kitu kinachoitwa mapenzi katika moyo wake.

Hili ni tatizo kubwa sana miongoni mwa wapendanao, lakini huwa kubwa zaidi baada ya wewe kuwa umetumia muda mwingi kuwa naye ukiamini siku moja ungekuja kuwa wake wa maisha, kumbe ni kinyume chake.

Ni vyema kama ukichukua hatua mapema baada ya kufanya uchunguzi wako na kubaini kuwa mpenzi uliyenaye hana mapenzi na wewe, bali ni matamanio ya mwili ndiyo yanayomdanganya.

Wakati mwingine unaweza kuwa na mpenzi ambaye anatarajia kukuacha, lakini usigundue mapema, anaweza akafanya mambo ya ajabu ambayo katika akili ya kawaida huwezi kujua mwenzio ana nia gani, kumbe ameshapanga kukuacha. Mwingine anaweza kuwa na visa vingi, nia yake ni kukutafutia sababu ya kukuacha.

Mwisho wa yote ni mateso na kuchukia mapenzi, lakini leo katika Love Moment kuna suluhisho. Zipo njia za kumwangalia mpenzi wako na kugundua kuwa anakupenda au anakutamani.

MAWASILIANO HUPUNGUA

Hili ni la kwanza kabisa kuonekana katika uhusiano unaolegalega. Hana msisimko na simu yako kama zamani, wakati mwingine huona kero hata kupokea. Chunguza jambo hili kwa makini, kama alikuwa na mazoea ya kukupigia simu mara tatu au zaidi kwa siku, hupunguza taratibu na wakati mwingine huacha kabisa.

Ukimuuliza, jibu analokupa halina maana yoyote, wakati mwingine ukimpigia simu, huchelewa kupokea au asipokee kabisa! Yote haya kusababishwa na mapenzi kupungua au kutoweka kabisa katika moyo wake. Ukiona mpenzi wako anapunguza mawasiliano na wewe ujue kuna kitu kinaendelea.

Kama alikuwa na kawaida ya kukuandikia meseji hupunguza kasi, hata kama akikuandikia inakuwa haina ladha ya mahaba kama ilivyokuwa awali. Ukimwandikia wewe anaweza asijibu na kama akijibu basi huwa kwa mkato, tena jibu tata ambalo litakuacha na maswali mengi kichwani mwako.

HANA MSISIMKO NA WEWE

Kwa kuwa alishapata alichokuwa anakitaka, hamu ya kuwa na wewe huisha kabisa. Hana muda wa kuwa na wewe tena! Mara zote hujifanya yupo bize na kazi, wakati mkianzisha uhusiano wenu hakuwa nazo.

Mazoea ya kutoka pamoja kama zamani huisha, unapomgusia kuhusu kuwa naye mahali kwa ajili ya kupanga maisha yenu ya baadaye, hukujibu kuwa ana mambo mengi ya kimaisha. Si ajabu kukuambia kuwa yupo makini na mambo ya kimaisha zaidi kuliko kukufikiria wewe.

Hatua hii ni ya mbali zaidi, ukiona mpenzi wako amefikia hapa, ujue kweli hana mapenzi na wewe tena, mtu wa aina hii hata mwanzoni huwa hana mapenzi ila tamaa ya mwili wake humdanganya, lakini kwa kuwa alishafanya mapenzi na wewe, umuhimu wako kwake huishia hapo.

HAKUJALI TENA

Kipengele hiki hakina tofauti sana na kilichotangulia, mwenye mapenzi ya dhati ni yule anayemjali mpenzi wake kwa kila kitu kila wakati, sasa kama ni kinyume chake ujue kuwa mapenzi nayo yamefikia mwisho!

Kama alikuwa na tabia ya kukujulia hali, siku hizi haoni umuhimu wa kufanya hivyo, hata kukuambia umeamkaje mpenzi, ni jambo gumu mno kwake! Kipengele hiki kinajumuisha mambo mengi kidogo, lakini kubwa zaidi ni lile la kukujali kimwili.

Kama wapenzi, mna wajibu wa kutimiziana tamaa zenu za kimwili, lakini wakati huu hana muda wa kufanya hivyo. Ukimwambia unahitaji kuwa naye faragha, haonyeshi ushirikiano.

Wakati mwingine unaweza kuwa unahitaji mahitaji muhimu kama  vipodozi n.k, ambavyo mwanzoni alikuwa akikuhudumia atabakia kutoa sababu nyingi zisizo na msingi. Hakuna kitu kibaya katika mapenzi kama kuwa na uhusiano na mwenzi ambaye unadhani anakupenda kumbe anakupotezea muda! Hilo ni tatizo ambalo baadaye linaweza kukusababishia maumivu katika moyo wako.

Wiki ijayo tutaendelea. Je, ungependa kujifunza zaidi masomo haya kwa njia ya simu? Karibu ujiunge na group letu la WhatsApp. Tuna meseji kwenda namba 0718-400146, utaunganishwa.

Jiandae kupata kitabu changu kipya cha SIRI ZA MAISHA YA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here