SHARE

NA MWANDISHI WETU


KAMA kuna kitu huwa ‘naenjoy’ sana kwenye maisha yangu, basi ni kuzaliwa Tanzania.

Kuna utulivu mkubwa sana hapa. Mbali na utulivu na amani kubwa tunayosifika nayo nje ya mipaka ya nchi hii, watu wa hapa tuna upekee wetu ambao huwezi kuupata popote pale duniani.

Zunguka kote, pande zote bado mambo ya Tanzania yanabaki kufanana na ya Tanzania tu!

Tayari George Lwandamina ameanza kazi, kwa tuliopata bahati ya kufika kwenye mazoezi ya klabu ya Yanga tunaweza kutumia maneno machache sana ya kumwelezea Mzambia huyu.

‘Lwandamina ni mtu wa kazi kweli kweli.’

Si mtu wa kusema na kurudia mara mbili. Fanya hivi, unafanya, ukishindwa adhabu inakusubiri. Hana huo muda wa kuzungumza sana.

Mbali na mazoezi makali na magumu anayowapa wachezaji, Lwandamina pia alitufundisha wapenda soka wa nchi hii jambo jipya ndani ya kikosi cha Yanga, sikuwa najua kabla!

Ndiyo, sikuwa najua kabla katika kikosi cha Yanga kuna wachezaji ambao hawawezi hata ‘kukontroo’ mpira. Hawajui kumiliki mpira na hata namna ya kupiga pasi ni tatizo kwao, wewe ulikuwa unajua hili?

Katika kikosi cha Yanga, Oooh No.. ngoja niweke hivi ili tuelewane, katika kikosi cha mabingwa wa VPL, mabingwa wa Kombe la FA kuna wachezaji ambao viwango vyao ni duni kiasi hicho.

Inashtua na kushangaza kidogo, lakini ndilo somo aliloanza nalo Lwandamina katika kikosi hicho. Na alifanya hivi kwa sababu.

Kwenye maelezo yake mwanzoni alidai mfumo anaotaka kuutumia ni lazima wachezaji wawe na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga pasi zenye macho.

Na kwenye kufanya wengi waelewe, akadokeza kuwa mfumo wake unajaribu kufanana fanana kidogo na ule unaotumiwa na FC Barcelona.

Barcelona ndiyo! Na si wale wa Vingunguti tuliowaona kwenye Ndondo Cup, la hasha, wanaomaanishwa hapa ni FC Barcelona ile yenye Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.

Lwandamina ana kazi kubwa ya kufanya kwa kweli!

Si shida kuifanya Yanga icheze kama Barca, ila shida kubwa ni kulitekeleza hili ukiwa na kikosi chenye wachezaji wenye viwango vidogo kiasi cha kushindwa kufahamu namna ya kupiga pasi.

Na hili si kosa la Yanga, ni kosa la mfumo mzima wa soka letu la Kiafrika.

Haya mazoezi anayohangaika nayo Lwandamina leo hii pale Gymkhana, kina Marcos Rashford walianza kuyafanya wakiwa na miaka nane.

Kujua namna ya kupiga pasi, kumiliki mpira ni masomo ya awali kabisa ambayo wachezaji hufundishwa mwanzoni mwa safari yao kisoka.

Ni jambo la ajabu kabisa mchezaji mwenye miaka 26 ndio aanze kujifunza namna ya kumiliki mpira, hii inapatikana Tanzania tu!

Na hili linatupa picha kamili ya ubora wa soka letu ulivyo, tutakuwa wapuuzi kama tukiendelea kushangaa kwanini tuko kwenye nafasi ya 160 kwenye orodha ya viwango vya FIFA na matatizo haya tuliyonayo.

Tuna rundo la wachezaji wenye vipaji vya kupiga chenga, lakini hawajui nini wafanye linapokuja suala la kucheza kitimu, Mungu ampe nguvu na uvumilivu Lwandamina kwenye safari yake.

Kila siku Watanzania ni hodari wa kuponda na kutimua makocha, lakini tunakuwa wavivu kutazama aina ya wachezaji tulionao.

Viwango vya wachezaji wetu viko chini mno, na si kwa wazawa tu, hata hawa wanaoitwa ‘profeshino’ wengi ni ‘maprofeshino wa passport tu’.

Viwango vyao na vyetu ni vilevile tu.

Kuna tatizo naliona, sipendi wala sitaki litokee, lakini kama ukweli ukitenda haki, hakuna mwenye nguvu ya kuweka kulizuia.

Huenda Lwandamina yule wa Zesco akabaki na sifa zake kwenye mitandao tu, hapa Tanzania akapata shida sana.

Na si kwamba ni kocha wa kawaida, shida ni aina ya wachezaji atakaokuwa anafanya nao kazi, binafsi sijashangaa sana kwanini hakuna mchezaji hata mmoja wa Zesco aliyekuwa tayari kumfuata Lwandamina Tanzania.

Chaila kayeyuka, yule Ayo Oluwafemi ndio hataki hata kusikia hizi habari, na bahati mbaya zaidi yule Jese Were ameamua kuwa mkweli, yaliyowakuta Wakenya wenzake hapa, yametosha kumfundisha jambo.

Tuna safari ndefu na soka letu na hili darasa analotupa George Lwandamina leo hii ni mwanzo mzuri wa kujifunza kama tutaamua kwa dhati kukaa chini na kumuelewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here