SHARE

LONDON, England

MABINGWA wa zamani wa EPL, Leicester City, si wale uliowazoea ndani ya miaka miwili ya hivi karibuni. Msimu huu wamekuwa wa moto mno, jana walicheza mechi ya kwanza EPL tangu walipoichakaza Arsenal mabao 2-1.

Baada ya kutuacha hivyo, wakaingia katika kipindi cha mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa huku tukiwa tunaitafakari jinsi gani itakavyomaliza msimu huu. Pengine itamaliza ndani ya nafasi nne za juu?

Kiwango walichokionyesha hadi kufikia kipindi hiki kimedhihirisha jinsi gani timu hiyo ilivyoandaliwa vyema kiasi cha kuzitia presha Liverpool na Man City ambazo zinajulikana kuwa ndio zilizoshikilia mpini.

Kabla ya mechi za wikiendi hii, Leicester ilikuwa ndio timu yenye rekodi nzuri kiulinzi kwa kufungwa mabao nane tu, huku ikifunga mabao 29, ikizidiwa na Man City pekee. 

Cha kufurahisha ni kwamba, Leicester imekusanya pointi nyingi ndani ya mechi 12 za EPL msimu huu, ukilinganisha na ule wa 2015/16 ambao walifanikiwa kuibuka mabingwa. 

Zaidi ya yote, hautakosea kusema wachezaji waliopo katika kikosi cha Leicester msimu huu ni bora zaidi ya wale waliobeba ubingwa wa EPL kwa sababu ya usajili makini uliofanywa. 

Ni kawaida ya klabu za aina ya Leicester kutozungumziwa kwa kina zinapofanikiwa kutengeneza timu imara kama waliyonayo sasa. Na kiujumla, kazi iliyofanywa na maskauti wa timu hiyo ni kubwa na nzuri. 

Kikubwa ambacho huangaliwa katika suala la usajili ni kiasi gani cha fedha kilichotumika kuliko namna gani fedha hizo zilivyotumika kupata wachezaji bora kwa kuzingatia uskauti mzuri na mipango ya kikosi.

Katika miaka michache ya hivi karibuni, Leicester imesajili wachezaji hodari na wenye ubora kwa gharama ya kueleweka. Ni mbinu ambayo imewasaidia kuibuka na kikosi chenye vijana ambao wanaelewana mno. 

Ndani ya misimu kadhaa baada ya kunyakua taji la EPL, wachezaji wawili ambao Leicester iliwasajili na wamefanya makubwa ni kiungo mkabaji, Wilfred Ndidi (pauni mil.16) na Harry Maguire (pauni mil.12).

Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa msimu uliopita, harakati zao katika soko la usajili zililipa kwa kiasi kikubwa, kwani wachezaji wanne ambao waliwasajili katika majira ya kiangazi, hivi sasa ni tegemeo.

Wachezaji hao ni kiungo mshambuliaji, James Maddison (pauni mil.22), mabeki Ricardo Pereira (pauni mil.20), Caglar Soyuncu (pauni mil.19) na Jonny Evans (pauni mil.3.6). 

Ni wazi mpango thabiti na unaohitaji subira kama huo hugeuka kuwa furaha kwa klabu kama Leicester, kununua wachezaji vijana huku wakitambua wazi watawauza kwa faida baada ya kuwatumia kwa misimu kadhaa. 

Mfano mzuri ni Maguire, alinunuliwa na kuuzwa ndani ya kipindi cha miaka miwili kwa faida ya zaidi ya pauni milioni 70. Mtazame mrithi wake, Soyuncu, ni wazi Leicester itajichotea faida kwa mara nyingine tena. 

Kiufupi, suala hilo halitegemei miujiza. Ni miundombinu ‘konki’ kuhakikisha wanapatikana wachezaji bora wa kuchukua nafasi za wale wanaoondoka na Leicester imekuwa mfano wa kuigwa katika sekta hiyo. 

Katika majira yaliyopita ya kiangazi, Leicester iliendelea na mbinu yake ya kusajili mbadala bora mapema baada ya maskauti kuifanya kazi yao, na mmoja wa wachezaji waliosajiliwa ni James Justin.

Beki huyo wa pembeni alisajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 6 tu akitokea Luton Town. Ana uwezo mkubwa wa kucheza pembeni kulia au kushoto. 

Ikiwa na maana Leicester tayari imeshajiandaa na maisha bila Ben Chilwell na Pereira, ambao wanafukuziwa na klabu nyingi na kubwa Barani Ulaya. 

Mwingine ni Dennis Praet, Mbelgiji aliyetua King Power akitokea Serie A na bila shaka kiungo mshambuliaji huyo alisajiliwa kama tahadhari tu iwapo Maddison ataondoka.

Hoja ya msingi hapa ni kwamba Leicester imekuwa imara kwa sababu ya kutokurupuka katika suala zima la usajili wa wachezaji bora. 

Je, ni dhambi kuishauri Man Utd kujifunza kupitia Leicester? Hapana. Hautapigwa mawe na yeyote ukisema hivyo kwa sababu ni ukweli mchungu.

Leicester inaweza kuwa mwalimu bora kwa Man Utd ambayo imekuwa klabu ya hovyo katika sekta ya usajili na mipango dhabiti ya kutengeneza kikosi imara tangu Sir Alex Ferguson astaafu. 

Mfano mzuri ni jinsi klabu hiyo ilivyozembea kusajili mapema mrithi wa Antonio Valencia ambaye alishaanza kuisha kiwango, ilipomsajili Diogo Dalot ilikuwa imechelewa na presha ikawa ni kubwa.

Kinda huyo raia wa Ureno akajikuta akisugua benchi kwa muda mrefu na Ashley Young akawa ndiye msaidizi wa Valencia katika nafasi ya beki wa kulia! 

Miaka michache mbele, leo Man United wana beki mwingine wa kulia, naye ni kinda, Aaaron Wan-Bissaka ambaye ameziba kabisa nafasi ya Dalot ambaye alishatabiriwa kuwa chaguo la kwanza. 

Wakati Leicester ikiamka na kufanya vizuri mno kwa sababu ya mipango mizuri ya kikosi na usajili makini, Man Utd inarudi nyuma kutokana na maamuzi mabovu na kutegemea zaidi nguvu ya kifedha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here