Home Burudani Unakumbuka kisa cha FM Academia ‘Wajelajela’? No.16

Unakumbuka kisa cha FM Academia ‘Wajelajela’? No.16

655
0
SHARE
  • Ndanda aachiwa Stonch arudi Segerea

NA JUMA KASESA
NI Jumatano nyingine tunakutana katika simulizi hii ya kisa cha wanamuziki wa bendi ya FM Academia ‘Wajelajela’ kukamatwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji na mkasa wa kutungwa kwa wimbo ‘Prison’.
Wiki iliyopita msimulizi wetu Malu Stonch aliishia kwamba yeye na wanamuziki wenzake baada ya kusota kwa wiki mbili gerezani Segerea hatimaye wamepandishwa tena kizimbani kujibu mashtaka yanayowakabali.
Stonch na wenzake wanane wameshtakiwa kwa kosa la kuishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria, kwani hawakuwa na kibali hata kimoja.
Huko uraiani Meneja Zonte ambaye ni mmoja ya watuhumiwa kwa kushirikiana na promota Hamisi Mujibu walikuwa wakiendelea kusuka mipango ya kuimaliza kesi hiyo au wanamuziki hao wapate dhamana.
Sasa endelea.
10552615_772223602799538_89972482604956369_nBaada ya kupandishwa kizimbani Zonte ambaye alitokea nyumbani kwa kuwa alitangulia kupata dhamana huku akiwa mshtakiwa namba moja akisomewa shtaka lake upya sambamba na wanamuziki wake, upande wa mashtaka ulieleza upelelezi wa shauri hilo ulikuwa bado haujakamilika kwa kuwa bado kuna watuhumiwa wengine walikuwa hawajapatikana. Ulieleza haukuwa na pingamizi la dhamana kwa wanamuziki wengine waliokuwa wakisota Segerea.
Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo aliwauliza washtakiwa kama kuna ambaye amekamilisha masharti ya dhamana, ndipo kidole cha Elombe Kichinja kiliponyanyuliwa juu.
Kwa muda ambao Elombe alikuwa yuko Dar es Salaam alishapendana na dada wa Kitanzania ambaye alikuwa mchumba wake. Familia ya mwanamke ilikuwa ikimtambua Elombe kama mchumba wa binti yao.
Mchumba yule wa Elombe alishasuka mipango mwanamuziki huyo apate dhamana siku kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Mmoja wa wanafamilia kutoka ukweni kwake alijitokeza kumdhamini shemeji yake. Hapo ndipo bahati ya mtende ilipomuangukia Elombe. Machozi ya furaha yalimchomoza ikiwa ni hali ya kutoamini kwamba siku hiyo angelala na kula uraiani.
Wakati ni furaha kwa Elombe, mambo yalikuwa magumu kwa wanamuziki wengine, kwani haikuwa habari njema kwangu Ndanda, Palipali, Desir Mwamba, Lily Kinondoni na wenzetu wengine.
Kitendo bila kuchelewa Elombe alikamilisha taratibu za dhamana na kuanza siku mpya kwa kurudi mtaani katika maisha ya kawaida. Sisi ambao hatukuwa na wadhamini tulirudishwa selo ya mahakama hiyo kusubiri saa tisa ifike karandinga liturudishe Segerea.
Kabla ya kuondoka kwenye viunga vya mahakama hiyo, Meneja Zonte alituhakikishia tusiwe na wasiwasi, mchakato wa kutafuta wadhamini unaendelea na kila kitu kitakwenda sawa.
Tulirudishwa Segerea. Hali ya maisha ndani ya gereza hilo ilikuwa ngumu.
Haivumiliki. Ugali mbele mboga nyuma. Maharage na ugali ni vyakula vilivyotupa shida. Hali ya uchafu ndani ya gereza ilianza kututafuna, kwani miili yetu ilianza kuvilia damu kutokana na kung’atwa na kunguni. Mwenzetu mmoja, Palipali ambaye ni mdogo wake Nyoshi El Saadat alipatwa na ugonjwa hatari wa ngozi.
Alikuwa akiwashwa mwili mzima. Ngozi ilianza kumenyeka na muwasho ukizidi kuongezeka kila kukicha. Uhaba wa dawa na ukosefu wa tiba za kutosha ikawa moja ya changamoto ya kupona tatizo hilo.
Ndani ya gereza hilo kuna dispensari ya uchunguzi wa magonjwa ya awali. Alipatiwa dawa lakini hazikuonyesha dalili ya kuponyesha tatizo lililokuwa limempata.
Kitu kingine kikubwa kwetu gerezani ilikuwa ni bahati ya kupendwa pia na bwana jela. Moja ya mambo ya msingi aliyokuwa akitusaidia ni uhakika wa maji ya kunywa na kuoga, lakini pia tusisumbuliwe na mahabusu wakorofi.
Lakini pia yule nyapara aliyetupokea siku ya kwanza tunaingia gerezani alitupenda, kwani tulikuwa miongoni mwa watu wenye kutoa burudani ya muziki kwa wafungwa na mahabusu.Ukaribu wetu na nyapara pia ulifanya tuendelee kuogopwa na watu wengine.
Tulipoianza wiki ya tatu gerezani mshtakiwa mwenzetu, Ndanda Cosovo ‘Kichaa’ alitumiwa hati ya kutolewa gerezani (remove order) kwa ajili ya kudhaminiwa. Askari polisi wawili walitumwa kuja kumchukua kupitia wito huo uliotoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jeraha la maumivu moyoni mwetu lilizidi kuongezeka kuona wenzetu wanazidi kutuacha gerezani. Hatukujua hatima yetu nasi ingekuwa lini.
Ikumbukwe bado tulikuwa wageni Dar es Salaam, kwani ndugu wa kubeba jukumu kubwa la kutudhamini ni jambo ambalo halikuwa kwenye fikra zetu.
Mahabusu na wafungwa waliokuwa wakipelekwa mahakamani kuitika tarehe ya kesi zao waliunganishwa na Ndanda Cosovo. Baada ya kufikishwa mahakamani mmoja wa wadau wetu wakubwa wa muziki wa dansi nchini, hasa FM Academia, Jimmy Chocolate wakati ule alijitokeza kumdhamini Ndanda Cosovo na kuachiwa huru.
Ulipotimu mwezi mmoja tukiwa bado hatujapata dhamana ndipo mnenguaji Lily Kinondoni ambaye alikuwa amesweka Keko alipofanikiwa kuchomoka tunduni. Lily alifanyiwa mpango na meneja Zonte na Promota Hamisi Mujibu akajitokeza mdau mmoja kumdhamini.
Kesi yetu iliendelea kutajwa kila baada ya wiki mbili, nasi tukiendeleza msimamo wa kutokubali shtaka lililo mbele yetu. Kwa muda wote wa mwezi mmoja na nusu tuliokuwa tumeshasota jela, Chitoto, marehemu Nuru Rubama na mumewe Sergi Mwila na baadhi ya watu wengine walioguswa na tatizo letu hawakuacha kuja kutufariji.
Kitu kikubwa tulichojifunza kwenye kesi hiyo ilikuwa kwamba wanamuziki hatupendani. Kwani hatukuona wanamuziki kutoka bendi nyingine kuja walau kutufariji tu. Hili halikuwa jambo lenye afya kwa ustawi muziki wa dansi nchini.
Kadri wenzetu walivyoondoka Segerea na Keko kwa kupata dhamana wengine unyonge ulizidi kuchukua nafasi, kwani kampani ilikuwa imepungu sana. Tayari jela tulishapata marafiki wa kutosha. Jambo kubwa zaidi lililokuja kutufariji ni ujio wa baadhi ya watoto wa Kinondoni waliokamatwa kwa makosa mbalimbali na kuletwa Segerea ambao walituchangamsha nao kwa stori za maeneo tuliyokuwa tukiishi.
Ilipotimu mwezi mmoja na siku 21 nikiwa Segerea ndipo nilipotokewa na ndoto nzito usiku. Ni ndoto gani iliyomtokea Malu Stonch? Nini hatima yake yeye na wenzake waliosalia Segerea. Hali ya Palipali Segerea aliyekuwa akiumwa ugonjwa wa ngozi iliendeleaje?
Usikose kusoma Dimba Jumapili kupata mwendelezo wa simulizi hii. Kwa maoni na ushauri 0715-629298.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here