SHARE

Ndanda Cosovo, Stonch, Elombe wagoma kula ugali maharage

NA JUMA KASESA

1045194_585829918105575_1946911406_nJUMAPILI wiki iliyopita katika simulizi ya kisa cha wanamuziki wa bendi ya FM Academia ‘Wajelajela’ kukamatwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji na mkasa wa kutungwa kwa wimbo ‘Prison’ msimulizi, Emery Malu Stonch, aliishia kwamba yeye na wanamuziki wenzake wameingizwa gerezani Segerea baada ya kukosa dhamana.

Ikumbukwe baada ya kukosa dhamana kesi yao iliahirishwa kwa muda wa wiki mbili ndio itakuja kutajwa tena katika mahakama hiyo. Pia kumbuka katika idadi ya watuhumiwa 10 ni meneja Zonte pekee ndiye aliyefanikiwa kuchomoka kitanzini baada ya kudhaminiwa na mkewe.

Aidha, itakumbukwa mmoja ya wanamuziki bendi hiyo, Lapape aliponea katika tundu sindano baada ya kusahaulika kujumuishwa katika kesi hivyo kuachiwa huru na kufanya idadi ya washtakiwa kubaki tisa.

Sasa endelea:

Saa 11 jioni tulifikishwa Segerea na kufanyiwa taratibu zote za kisheria anazopaswa kufanyiwa mahabusu anapoingia gerezani. Tulipekuliwa kila kitu mwilini ili isije ikawa tuna kitu chochote kinachoweza kuhatarisha usalama wetu na wa mahabusu wengine.

Upekuzi huo pia ulihusisha tahadhari ya kuingizwa kwa bangi au kilevi cha aina yoyote gerezani sambamba na kuorodhesha vitu vyote tulivyokua navyo mifukoni katika kitabu maalumu cha Magereza.

Tayari ilishakuwa jioni. Tulikuta wafungwa na mahabusu gerezani hapo wameshaingizwa kwenye selo zao za kulala. Kabla ya kuingia kwenye selo hizo mmoja ya maaskari katika gereza hilo alituita na kutupatia ugali na maharage ikiwa ndiyo chakula cha usiku.

Baada ya kuutazama tu ugali tulikataa kula ingawa tulikuwa na njaa kali kwani mchana kutwa tulikua hatujala zaidi ya ile chai tuliyoletewa asubuhi sentro Polisi wakati tunajiandaa kupelekwa mahakamani.

Kwanza ugali wenyewe ulishapoa muda mrefu na tayari ulishaweka gamba gumu kuashiria ulipikwa muda mrefu. Maharage yalikuwa na sura ambayo si ya kawaida kwani yalionyesha dhahiri yalikuwa hayajaiva.

Kwa mtu aliyezoea uraiani ni ngumu kutamani hata kuyatia mdomoni maana hayakuwa na tofauti na maharage mabichi. Walitusihi kula japo kidogo kwani kufika mpaka kesho asubuhi bila kula ingekuwa mtihani mkubwa kwetu. Tuliamua kushikashika ugali kidogo na michuzi ya maharage tukala kama matonge manne tukanawa.

Rasmi sasa tuliingizwa kwenye selo za gereza hilo kwa ajili ya kuanza maisha mapya kwa muda wa wiki mbili. Tulipokewa na nyapara mmoja ambaye baada ya kutuona tu alituita kwa kuigiza lafudhi ya kikongo ‘mweye kina Papa mukuye huku nimeshawatafutia fasi ya kulala” lazima mtuburudishe na nyimbo kabla hatujalala leo.”

Tulicheka kidogo. Kwani jamaa alituchangamkia sana kiasi ambacho tulihisi faraja kidogo. Kumbuka tulishaambiwa maisha ya jela ni magumu kuna utemi na vitendo vya kuoneana. Jamaa alituingiza ndani ya vyumba na kutuonyesha mahala tupumzike.

Kichwani nilikua najiuliza jamaa alijuaje kama sisi ni wanamuziki wa Kikongo. Ingawa kweli tulikuwa tunafanana na wasanii kweli. Baada ya muda niligundua kuwa jamaa walijua habari za kukamatwa kwetu kupitia kipindi cha Africa Bambataa cha Redio Clouds FM kilichokuwa kikirushwa saa 12 jioni.

Ndani ya gereza la Segerea kulikuwa na redio kwa ajili ya wafungwa na mahabusu inarusha matangazo humo waweze kusikia taarifa za habari na vipindi vingine vya kijamii na burudani.

Kwa gerezani mle redio kipenzi ilikuwa ni Clouds FM kwani itakumbukwa ndiyo kipindi kifupi imetoka kuanzishwa na kuingia na moto wa vipindi vya kisasa vya burudani na kujikuta ikiwa chaguo la wengi Dar es Salaam na mikoa ya jirani ilikokuwa imeanza kusikika.

Hata tulipokosa dhamana siku tuliyopelekwa mahakamani walishapata taarifa kupitia redio hiyo iliyorusha dondoo za kilichotokea mchana ule kuwa tumekosa dhamana. Ilishakuwa saa 12 jioni kigiza kimeshaanza kuingia kulikuwa na burudani ya muziki inapigwa jioni hiyo.

Sauti ya Dj Charlse Mwamiji na marehemu Amina Chifupa AC zilikuwa zikivuma kwenye kipindi cha Africa Bambataa huku wasanii Onyango, Mwita Maranya na wengineo nao wakivuma kwa vichekesho vya matangazo yao.

Je, nini kiliendelea baada ya wanamuziki hao kupokelewa na nyapara huyo. Maisha yao ya jela yalikuaje kwa siku hiyo ya kwanza usikose kusoma gazeti la Dimba Jumapili kupata mwendelezo wa simulizi hii. Kwa maoni na ushauri 0715-629298.

SHARE
Previous articleCheka kuzipiga na Mcolombia
Next articleFUNGA KAZI!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here