SHARE

NA AYUBU HINJO

MOJA ya mambo ambayo klabu ya Simba wanajivunia ni uwepo wa mashabiki wao ambao wamekuwa wakifunika kwa kuujaza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nadhani hakuna haja ya kuelezea sana, kila kitu kinajulikana juu yao.

Mchezaji mmoja wa Power Dynamos kutoka Zambia, alidai kufungwa kwao katika Simba Day iliyofanyika mwaka jana kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na mashabiki wa wapinzani wao, ambao walifurika na kushangilia kwa kupiga kelele. Hakuwahi kuona.

Hata hivyo, si mara ya kwanza kwa mashabiki wa Simba kufanya hivyo, michezo ya kimataifa ambayo walicheza msimu uliopita, walikuwa sehemu ya timu yao. Wakiishangilia, Waliimba na kucheza.

Wapinzani wengi walipotezwa. Simba waliufanya Uwanja wa Taifa kuwa machinjio yao pindi walipokosa matokeo ya ushindi ugenini.

Msimu uliopita, mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara hao walicheza michezo sita katika Uwanja wa Taifa. Walishinda mara tano na kutoa sare mmoja huku msimu huu wakicheza mechi moja tu.

Makala haya yanakuletea mechi saba ambazo Simba walicheza katika Uwanja wa Taifa, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia msimu uliopita hadi huu.

SIMBA 4-1 MBABANE SWALLOWS

Hii ndio mechi ambayo ilionyesha mwanga wa mafanikio kwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara hao, ulikuwa mchezo wa hatua ya awali kama ulivyo huu wa leo.

Mechi ya kwanza ilichezwa hapo, wenyeji waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 ambao uliwapa uhakika wa kusonga mbele hatua iliyofuata dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini.

Tena, kubwa zaidi, Simba walishinda jumla ya mabao 8-1 dhidi ya Waswazi hao, kwani, mchezo wa marudiano waliziona nyavu za wapinzani waoa mara nne na kufanya matokeo kuwa mabao 4-0.

SIMBA 3-1 NKANA FC

Mechi ya kihistoria zaidi kwa Wanamsimbazi. Baada ya kuwatoa Mbabane Swallows walikutana na Nkana FC ya Zambia ambayo walisonga mbele kwa kuichakaza UD Songo.

Simba walikumbana na kichapo cha mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza, uliochezwa kwenye Uwanja wa Nkana, nchini Zambia.

Kama kawaida yao, mashabiki wa Simba waliujaza Uwanja wa Taifa, wote walikuwa tayari kuona historia ya klabu yao kutinga hatua ya makundi inaandikwa hapo. Kwa pamoja, walishangilia na kucheza.

Hakuna kingine kilichotokea zaidi ya ushindi wa mabao 3-1 kwa mnyama, kilichovutia na kuwapagawisha mashabiki wa Simba ni lile bao la Clatous Chama alilofunga dakika za mwishoni, baada ya Jonas Mkude na Meddie Kagere kufunga hapo awali huku Walter Bwalya akifunga la kufutia machozi kwa upande wa wageni.

Simba walifanikiwa kuingia hatua ya makundi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15 kupita.

SIMBA 3-0 JS SAOURA

Ulikuwa mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi kwa Simba, walicheza dhidi ya JS Saoura kutoka nchini Algeria ambao nao ilikuwa mara ya kwanza kutinga hatua hiyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Emmanuel Okwi aliwanyanyua vitini mashabiki wa Simba, kwa kufunga bao la kwanza, kabla ya meddie Kagere aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya majeruhi John Bocco kupachika kupigilia misumari miwili.

SIMBA 1-0 AL AHLY

Safari hii, Simba waliwakaribisha vigogo wa soka la Afrika katika ardhi ya Dar es Salaam, Jiji linaloongozwa na Paul Makonda, tena lililobeba uchumi wa Tanzania kwa asilimia kubwa.

Kila mmoja alisubiri kuona kipi Simba watakifanya baada ya kukumbana na kichapo cha mbwa mwizi cha mabao 5-0 nchini Misri. Al Ahly waliwanyoosha kisawasawa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo, Kagere alikuwa sumu kwa timu hiyo iliyotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara nane, nyingi zaidi ya klabu nyingine yoyote, kwa kupachika bao pekee kwa shuti kali.

SIMBA 2-1 AS VITA

Kama ilivyokuwa dhidi ya Nkana FC. Simba walihitaji ushindi ili watinge hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, walicheza dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mchezo wa awali, uliochezwa ugenini, Simba walifungwa mabao 5-0. Kilikuwa kipigo cha pili mfululizo baada ya kukutana na kichapo kama hicho nchini Misri dhidi ya Al Ahly.

Ingawa, mwisho wa siku zilihesabika pointi, wala hakukuwa na sheria ya timu hizo zilipokutana matokeo yalikuwaje (head to head)!.

Mbele ya umati wa mashabiki wa Simba waliofurika uwanjani hapo, Chama kwa mara nyingine alifunga bao la ushindi dakika za mwishoni, baada ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kusawazisha, kwani wageni hao walitangulia kuziona nyavu za wenyeji wao.

SIMBA 0-0 TP MAZEMBE

Simba walipangwa kucheza na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo ulimalizika kwa suluhu, kabla ya Simba kuchapwa mabao 4-1 katika mechi ya marudiano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

SIMBA 1-1 UD SONGO

Mnamuona huyo Luis Miquissone anayevaa jezi ya Simba hivi sasa? Basi, alikuwa adui mkubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo alipokanyaga nyasi za Uwanja wa Taifa akiwa na kikosi cha UD Songo ya Msumbiji.

Matumaini makubwa ambayo yalikuwa katika mioyo ya mashabiki wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, yaligeuka simanzi na uchungu kwao baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Simba walishindwa kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani mchezo wa kwanza uliochezwa Msumbiji ulimalizika kwa suluhu.

Bao la wageni hao lilifungwa na Miquissone kwa njia ya faulo lakini Simba walisawazisha kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na beki wa kati, Erasto Nyoni. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here