SHARE

NA NIHZRATH NTANI

HAPA ni kwetu nyumbani.Hapana si kwetu nyumbani, najiuliza?
Bila shaka, sisi ni wakimbizi ndani ya nchi yetu wenyewe. Ni watumwa juu ya ardhi yetu wenyewe. Mateka ndani ya ngome yetu.

Sisi ni wendawazimu tuendao peku na uchi angali nguo na viatu tumebeba kichwani, kisa tunataka kuonekana tunatembea na mzigo kichwani. Sielewi! Sielewi!

Haya ni maneno yaliyowahi kutoka kinywani mwa mwendawazimu mmoja ,siku moja. Ni maneno yaliyojaa falsafa kubwa ndani yake. Nadhani unahitaji tafakuri ya kina kuelewa kuhusu falsafa hii.

AJIBU NI KIWAKILISHI CHA UWENDAWAZIMU WETU

Wiki moja iliyopita, ilisambaa habari ya kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga, Ibrahim Ajibu Migomba kuikatalia klabu ya TP Mazembe iliyokuwa na nia ya kumsajili kwa uhamisho huru.

Tulielezwa kuwa; maslahi madogo ni sababu ya kiungo huyo fundi wa mpira nchini kuikataa nafasi hiyo ambayo mimi naweza kuiita ya dhahabu.

Kuna wakati wanadamu wanapata bahati, na Ajibu ni mmoja ya wanadamu hao waliopata kuwa na bahati. Achana na kipaji chake maridhawa. Kitendo cha kutakiwa na Mazembe ni bahati pia.

Amepata wapi ujasiri wa kuikataa nafasi hii? bila kujua ama washauri wabovu wanaomzunguka wamemshauri vibaya. Ila kwa hili Ajibu hakuhitaji ushauri.

Wachezaji wengi wa Afrika Magharibi ndipo mahala hapa wanapotushinda.Hivi leo wametapakaa barani Ulaya. Wanatafuta mafanikio kwa nguvu zote.

Ajibu alipaswa kuisoma simulizi aliyonayo Mbwana Samata mpaka alipofika hapa alipo. Kuna wakati Mbwana alitaka aingie katika akili hii ya Ajibu . Ni wakati ule aliposajiliwa kutoka African Lyon kwenda Simba.

Mbwana inasemekana aligoma kucheza Simba mpaka wampatie gari waliomuahidi kwenye mkataba. Mwishowe alikubali kucheza bila kutimiziwa ahadi yake. Shukrani kwa washauri wake.

Hivi leo,Tungali tunaimba jina lake na mfalme mahala hapa. Ajibu alipaswa asome historia ya Mbwana Samata na si kuifuata akili ya Mrisho Ngasa.

Historia ya Mrisho Ngassa ilishapatwa kuandikwa. Leo hii hakuna anayemjali tena Ngassa.Kuna tetesi kuwa ameshasaini mkataba wa awali na klabu ya Simba na kuikacha TP Mazembe. Bila shaka , Ajibu ni mmoja ya wanadamu wachache Duniani wenye kuweza kufanya maamuzi kama aliyoyafanya.

Unapata wapi ujasiri wa kuikataa Mazembe mbele ya Simba na Yanga?
Ajibu alipaswa kwenda TP Mazembe hata kwa mshahara wa milioni moja tu kuliko kubakia Simba ambako angepata milion 2. Nadhani unaweza kunishangaa.

Kwa kipaji cha Ajibu, ilihitajika jitihada binafsi tu. Angehitaji msimu mmoja au miwili kabla ya safari yake ya kucheza soka Barani Ulaya kugeuka kuwa rahisi. Huwezi kuifananisha TP Mazembe kwa Simba.

Ni rahisi kwa Ajibu kuuzwa moja kwa moja katika moja ya ligi maarufu Duniani kama angeenda Mazembe kuliko Simba. Ilihitajika akili ya ziada kutambua hili.

Mwisho, tunapaswa kumuacha Ajibu na uamuzi wake. Ila tuna shida kubwa sio tu kwenye soka letu hata kwenye utawala wa viongozi wetu wa kisiasa. Huko nako ni shida pia.

TFF WANAPATA WAPI UJASIRI WA KUJIITA VIONGOZI WA SOKA NCHINI?

Inahuzunisha kila ukifikiria. Kuna mahala nadhani tumelaaniwa. Haingii akilini kwa namna ya hawa viongozi wa soka wanayoyafanya katika soka letu.

Kuna wakati najiuliza, kwanini tusiuingize mchezo wa soka kama sehemu ya kivutio kwa watalii wanaokuja nchini? Haya yanayotendeka hapa sidhani kama kuna mahala yanatendeka.Wiki chache zijazo tutashiriki michuano ya Afcon kule Misri. Wenzetu tuliokundi moja wapo kambini wakijiandaa na michuano hiyo.

Sisi bado tunaendelea kupiga siasa tu. Haitaji kupiga ramli ama elimu ya utabiri kujua kitakachotokea huko Misri. Bila shaka, tutaenda kama watalii na sio kushindana.Mwishowe, tutaendeleza ile kauli yetu maarufu ya “Tumekufa kiume” halafu tutarudi na kupiga soga zetu. Maisha yanaendelea.

HILI NALO LIMENIFANYA NICHANGANYIKIWE

Achana na mechi ya “Play Off” kati ya Pamba dhidi ya Kagera Sugar iliyohairishwa Juni 2 pale dimbani Nyamagana jiji Mwanza.

Kituko kilikuwa hichi; Tiketi zilizouzwa kwa ajili ya mechi hiyo ni tiketi iliyoonesha ni mechi kati ya Toto Africa dhidi ya Tanzania Prisons. Mechi iliyochezwa April 3, 2013, yaani miaka sita iliyopita.

Kama mechi ile ingechezwa bila shaka mgawanyo wa mapato tungeambiwa kuna mgawo wa gharama za tiketi. Huu ni uhuni ambao tumeuzoea katika soka letu.

Kituko kingine kinachonipa ukakasi hadi hivi leo. Kanuni ya ligi kuu inasema; Timu tatu zitashuka daraja kwenda ligi daraja la kwanza na timu tatu za daraja la kwanza zitapanda kwenda ligi kuu kila msimu.

Ratiba ya “Play Off” imepangwa kwa Geita Gold Mine ambayo imetoka daraja la kwanza inacheza na Mwadui iliyokuwa ligi kuu msimu uliopita. Vile vile Pamba ya Mwanza iliyo daraja la kwanza inacheza na Kagera Sugar iliyokuwa ligi kuu.

Je ikitokea timu za Pamba na Geita Gold Mine zikafungwa?, kiujumla Kagera na Mwadui zitasalia ligi kuu msimu ujao. Hapo ligi kuu itakuwa imeshusha timu mbili tu badala ya tatu.

Je kanuni inataka timu tatu kushuka, itakuwaje? Hivyo hivyo, ikitokea Pamba na Geita Gold Mine zikashinda, kanuni itasimamaje? Sielewi! Sielewi! Nimebakia njia panda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here