SHARE
Na Joseph Shaluwa

LEO ni siku ya mwisho katika mwaka huu wa 2017, tukiwa tunaelekea mwaka mpya wa 2018, kwa hakika ni furaha kubwa kumaliza mwaka salama. Inatupasa tumshukuru Mungu kwa neema hii ambayo ametupa bure tu!

Marafiki wapo wengi waliotamani kuifikia leo lakini kwa mapenzi yake Mungu, leo hatunao. Hii haina maana kuwa sisi ni wa maana sana au tumefanya mema sana, la hasha. Ni neema, huruma na mapenzi ya Mungu mwenyewe.

Sasa hebu tuingie kwenye mada yetu. Nazungumzia namna ya kuboresha uhusiano na kuwa mpya kila siku. Yapo mambo ya msingi sana kuzingatia ili kufanya uhusiano wako uendelee kuwa mpya siku hadi siku.

Jambo la kwanza kabisa ambalo husaidia sana kuboresha uhusiano usichuje ni kutoana out. Hii ni kwa wote, hakuna mwenye wajibu pekee juu ya kumtoa mwandani out. Mwanaume anaweza kufanya hivyo hata mwanamke kwa lengo la kuimarisha uhusiano.

Swali la msingi ni je, mkiwa out nini unapaswa kuzingatia ili kujenga, kuboresha uhusiano kama ambavyo lengo lako lilivyokuwa? Twende katika kipengele kinachofuata hapo chini:-

ONYESHA MAPENZI YAKO

Wengine ambao mawazo yao husafiri kwa kasi tayari wameshanihukumu! Wamenihukumu wakidhani kuwa nawafundisha watu kufanya ngono! Sipo huko ndugu yangu. Safu hii ni kwa ajili ya kuwafundisha watu kuacha tabia zisizofaa na kufanya yale yanayostahili.

Ninaposema onyesha mapenzi, namaanisha kuwa lazima utumie kauli nzuri ambazo zitaweza kuonyesha ni kiasi gani unampenda. Onyesha kuwa unamjali na bila yeye maisha yako hayawezi kwenda. Ni kazi ndogo sana kufanya hayo.

Kumbusu mashavuni mwake au kumkumbatia huku ukisikiliza joto la mwili wake, ukimhemea masikioni mwake huku ukimwambia maneno matamu, utaweza kumfanya mpenzi wako asifikirie kukusaliti na uhusiano wenu kuendelea kuwa bora, wenye nguvu na imara.

WEKENI MAMBO SAWA

Usikubali kukaa na kinyongo moyoni mwako, kama kuna jambo ambalo mpenzi wako anakufanyia na huridhiki nalo, ni vyema ukatumia muda huo kumweleza. Utakapomuweka wazi atajua ni wapi amekosea na inakuwa rahisi yeye kubadilika.

Ila jambo la kuzingatia katika hilo, unapaswa kutumia kauli ya taratibu ambayo itamsihi, mweleze jinsi unavyokereka na jambo linalokuchukiza. Kuwa wazi kwake, hiyo itasaidia kulinda penzi lenu.

USIKUMBUSHE YALIYOPITA

Hili ni moja kati ya matatizo yanayowakumba watu wengi walio katika uhusiano wa mapenzi. Kama aliwahi kukukosea, akakuomba msamaha na mkasameheana, huna sababu ya kumkumbusha juu ya jambo hilo. Si busara kumwambia kuwa kila siku amekuwa mtu wa kukosea. Kumwambia hivyo kunamfanya ajisikie mkosaji kwako na wakati mwingine anaweza kukosa hamu ya kuendelea kuwa na uhusiano na wewe.

Mwingine anaweza akasema: “Kila siku wewe umekuwa mtu wa kukosea, wewe ni mtu wa aina gani? Uliniambia hutarudia tena kunikosea lakini bado umefanya kwa mara nyingine, kwanini unakuwa hivyo lakini?”

Kauli hii haifai kabisa kwa mpenzi wako.

VIJIZAWADI VYA KIMAPENZI

Kwa wanawake si jambo gumu sana kutimiza kipengele hiki, lakini kwa rafiki zangu wanaume ni wagumu sana kuwanunulia wapenzi wao zawadi! Zawadi si lazima iwe gari, hata ukimnunulia nguo ya ndani tu Sh 5,000 pia ni zawadi ambayo ataifurahia sana!

Lakini wakati mwingine unaweza ukafanya mambo kwa mtindo wa utani, yaani unafika nyumbani, unamwambia mpenzi wako afumbe macho, kisha unafungua pipi iliyo ndani ya karatasi unamwambia afumbue macho, kisha unamkabidhi zawadi yake, unadhani atajisikiaje?

Si lazima iwe pipi, unaweza ukanunua hata apple tu na ukamfurahisha sana mpenzi wako. Haijalishi una zawadi kubwa kiasi gani au umetumia gharama kubwa kiasi gani, ila umefikishaje zawadi yako? Inaweza kuwa ndogo lakini ulivyoifikisha kwa utundu na manjonjo ukamfanya mpenzi wako aifurahie na kuona penzi lenu linazidi kuchanua na kuwa jipya kila siku.

Leo natia nanga hapa, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine. Nakutakia maandalizi mema ya kuupokea mwaka mpya 2018.

Je, unapenda kujifunza masomo haya zaidi kwa njia ya simu? Wasiliana nami kwa simu 0712 170745/0763 255818.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano. Ameandikia vitabu vingi vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here