Home Funguka/Mapenzi UPO KWENYE PENZI HAI AU LILILOKUFA?

UPO KWENYE PENZI HAI AU LILILOKUFA?

584
0
SHARE

Na Joseph Shaluwa

NILIWAHI kusema na leo narudia tena kueleza kuwa mapenzi ni hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine. Hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na penzi la dhati, huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo.

Yes! Hii ndiyo maana hasa ya mapenzi, ingawa kwa upande wako unaweza kufikiri tofauti. Ni hivi, unapoingia katika uhusiano na mpenzio hupaswi kabisa kuwa na mtu mwingine, kwakuwa utakuwa unaunyima haki moyo wako.

Pamoja na ukweli huo juu ya mapenzi, lakini hivi sasa maana halisi ya mapenzi imepotoshwa, imebadilishwa na kuwa nyingine. Mapenzi ya siku hizi yamejaa ulaghai mtupu, hayana ukweli, kila siku ni maumivu juu ya maumivu.

Kuna matatizo mengi ambayo yanaweza kutokea ikiwa utakosa uaminifu kwa mpenzi wako, wakati mwingine matatizo hayo huweza kumlenga mwenzi wako moja kwa moja bila kukusumbua wewe, lakini mwisho wa siku wewe utakuja kuwa na matatizo zaidi ya hayo unayoyafanya nyuma ya pazia hivi sasa.

Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi zaidi ya kumi huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya, maana kuna siku utakuja kuumbuka kwa kuonekana kwako huna uaminifu!

Inawezekana unachanganyikiwa na mambo mengi na hujui umesimamia wapi katika uhusiano wako. Inawezekana unawaza mema juu ya uhusiano wako lakini mwenzako anawaza tofauti. Pengine anafikiria kukuacha au umeshaachika kabisa lakini hujui.

Ndugu zangu, wakati mwingine si ajabu ukawa umekaa na mwenzako kwa miaka mingi ukiwa na matarajio ya ndoa, lakini mwenzio hawazi hivyo. Anajitahidi kukuonesha kila dalili kuwa amekuchoka, lakini hujui maana upo kwenye penzi la upofu.

Haya mambo yapo rafiki zangu. Katika mada hii naamini utafumbuka macho na utajua kwamba umesimamia katika uhusiano wa aina gani.

Ni suala la kutuliza akili yako na kufuatilia kwa makini mada hii ambayo bila shaka ni mkombozi wako.

 UMESIMAMIA WAPI?

Kuna suala la uongo katika mapenzi. Wengine  ni tabia yao ya asili, siyo wakweli kuanzia malezi ya wazazi hayasisitizi juu ya ukweli. Kwa mpenzi wa aina hii ni vigumu sana kudumu naye.

Ni mwepesi wa kutamka maneno ya mapenzi, lakini ndani ya moyo wake kukawa na vitu viwili; kwanza anakutamani wewe na pesa zako na wakati huohuo anatamani kuwa na bwana mwingine kwa ajili ya kuongeza kitega uchumi, hili ni tatizo!

Mwanamke wa aina hii siyo ngumu kwake kukuita majina mazuri ya kimapenzi, lakini akiwa hamaanishi kutoka moyoni mwake kwamba anakupenda. Hawa wapo wengi, lakini ni vigumu sana kuwagundua mapema. Hawa huharibu kabisa maana halisi ya mapenzi.

Utakuta mwanamke ana mpenzi wake, tena huenda ni mchumba kabisa na wana malengo ya kuoana, lakini bado anakuwa na mwanamume mwingine. Ya nini yote hayo?

Huyo mwanamume anayekudanganya leo, kesho hayupo na wewe na atakuwa amekuachia maumivu katika maisha yako, hasa kama mwenzako atagundua amewekeza penzi lake sehemu siyo na kuamua kubadilisha uamuzi.

 KUNA SUALA LA USHAWISHI

Hili  ni tatizo lingine linalochochea kuharibu maana ya mapenzi. Ushawishi ni sumu nyingine katika hili. Hapa nitazungumzia pande mbili – mshawishi na mshawishiwa! Naweza kusema wote wana makosa, maana anayeshawishi hutumia kila njia kumpata anayemhitaji, lakini wakati huo huo anayeshawishiwa kukubali wakati akijua ana mpenzi ni kosa kubwa sana.

Wanaume wengi watu wazima tena wenye familia zao hivi sasa ndio wanaoongoza kutafuta dogodogo wakidai kuwa damu zao zinachemka! Hutumia fedha, magari na kila aina ya vishawishi ili waweze kuwanasa wasichana hao wadogo wakitafuta penzi.

Kutoka nje ya ndoa siyo suluhisho, sanasana utakuwa unayafuata matatizo mwenyewe, hasa kama utatumbukia kwenye sehemu ambayo utashindwa kutoka.

Jambo la msingi zaidi ni kukaa na mwenzako ndani ya ndoa na kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kufanya uhusiano kuwa imara. Kukimbilia barabarani si dawa.

Kwa wanaoshawishiwa sasa, asilimia kubwa huwa na wapenzi wao, lakini kwa tamaa ya pesa hujikuta wakijitumbukiza katika uhusiano mpya wa kisaliti.

Tangu umeanza kukimbiakimbia huko mitaani umepata nini? Ni suala la kufumbuka ubongo na kuchukua hatua.

Bado mada hii inaendelea. Wiki ijayo nitakuwa hapa kwa mwendelezo wake. USIKOSE!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here