Home Habari USAJILI MPYA SIMBA WAVUJA

USAJILI MPYA SIMBA WAVUJA

271
0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE,

SIMBA imesikia kilio cha mashabiki wake ambao wamekuwa wakiukosoa udhaifu uliopo kwenye kikosi chao na sasa uongozi wa timu hiyo umeamua kufanya kweli, kwa kupanga mikakati ya usajili kimya kimya, ili kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Huku Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiendelea ukingoni, Simba imeanza kukitathmini kikosi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi na michuano ya kimataifa kama watapata nafasi hiyo.

Habari za uhakika kutoka kwa mmoja ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, zimelieleza gazeti hili kwamba, kwa sasa wanahitaji kujaza wachezaji wa kimataifa katika nafasi tatu muhimu, ambazo ni straika, beki wa kulia na kati.

Nafasi ya straika mpaka sasa wana uhakika wa kumsainisha straika wao wa zamani, Mganda Emmanuel Okwi, kuchukua nafasi ya Frederick Blagnon anayetemwa, huku utata ukibaki kwa beki Mcongo Janvier Bukungu.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo, Bukungu ameibua mvutano baina ya viongozi, kwani kuna wanaotaka abaki, wengine wakitaka aachwe ili atafutwe beki wa kulia shupavu atakayeweza kuhimili michuano ya kimataifa.

Mwingine anayetajwa kutupiwa virago ni beki Method Mwanjali, ambaye umri mkubwa na majeraha ya mara kwa mara vinatajwa kutolishawishi benchi la ufundi kumbakisha kikosini.

Straika wa kimataifa Mrundi, Laudit Mavugo, amebakizwa kundini kutokana na mchango wake mkubwa, huku Mganda Jjuuko Murshid naye akisalia kwa vile bado ana mkataba na Simba.

Aidha, kipa Daniel Agyei amefanikiwa kufanya kile kinachotakiwa langoni, kwani ameonyesha uimara wa kutosha tangu ajiunge na timu hiyo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

Alisema hata hivyo, kikosi hicho kinaweza kikapanguliwa zaidi kama watapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, kwani timu hiyo ya sasa haiwezi kuhimili michuano ya kimataifa.

“Viongozi wengi wanasikilizia kwanza, kama Simba itapata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa, kikosi kitafumuliwa, utashangaa watabaki wachezaji wachache sana,” alisema mjumbe huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here