Home Habari UTAJIRI WAREJEA YANGA, WACHEZAJI WAMWAGIWA NOTI

UTAJIRI WAREJEA YANGA, WACHEZAJI WAMWAGIWA NOTI

475
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

MASHABIKI wa Yanga ni lazima wachekelee watakapoisoma taarifa kwamba, utajiri umeanza kurejea tena Jangwani baada ya mabosi wa timu hiyo kuhakikisha masuala yote yanayohusu mishahara ya wachezaji yanakwenda sawa.

Yanga inapambana kufa na kupona kuhakikisha inafanya vizuri katika mechi zake zote zijazo, ikiwamo kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kombe la FA na kuweka rekodi ya kuwang’oa Waarabu katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Mapema mwaka huu Yanga iliingia katika misukosuko baada ya mwenyekiti wa timu hiyo kupata matatizo na kushikiliwa na maofisa wa uhamiaji, hali iliyopelekea kuchelewa kwa mishahara.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo, akiwamo beki wa kati Vincent Bossou, kutamka hadharani kwamba, wanadai mishahara yao, lakini kwa sasa mambo yamekwenda vizuri.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, ameliambia DIMBA katika mahojiano maalumu kwamba, sasa anapata usingizi baada ya wao kama uongozi kufanya kila linalowezekana na kufanikiwa kulipa malimbikizi yote, isipokuwa ya mwezi huu wa tatu ambao haujamalizika na yale ya Agosti, mwaka jana, waliyokuwa hawajalipwa, hivyo wachezaji wasiwe na wasiwasi na waendelee kuitumikia timu yao kwa moyo wao wote.

“Sasa hakuna mchezaji anayetudai zaidi ya mwezi huu ambao bado siku chache na ule wa Agosti ambao hatukuwalipa, hivyo nina imani siku chache zijazo tutamalizana nao, kilichobakia waendelee kupambania timu yao,” alisema.

Alisema suala hilo la mishahara ya wachezaji lilikuwa linamuumiza sana, ikizingatiwa kuwa, hata yeye alikuwa mchezaji kipindi cha nyuma na anajua maumivu wanayoyapata, lakini atahakikisha anakabiliana na changamoto zote ili kutimiza majukumu yake.

Alisema hadi hivi sasa anaweza kusema anapata usingizi mzuri, kutokana na kutokuwa na deni lolote, hasa kipindi hiki walichokuwa wakijiandaa na michuano ya kimataifa, ikiwamo maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia, ingawa walitupwa nje na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho.

Mbali na hivyo, Mkwasa pia ameelezea mikakati yao ijayo ya kuhakikisha timu inatengeneza fedha nyingi kutoka kwa wadau wao, ikiwamo kuandaa harambee kubwa itakayojumuisha wanachama na vigogo wenye fedha zao, lengo likiwa ni kuhakikisha timu hiyo haiyumbi kwa namna yoyote ile, hasa wakati huu wanapokabiliwa na michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

“Sasa tumekubaliana hilo, wiki ijayo tunatarajia kuzindua harambee hiyo kwa mashabiki kuchangia fedha kidogo kwa ajili ya kuendesha klabu yetu, kwanza hapa lazima tuweke wazi kuwa, hali imeyumba kidogo, hivyo sisi kama viongozi lazima tupambane.

“Tumeamua kuanzia hapa kwenye harambee, lakini kubwa nataka kuwahakikishia mashabiki wetu kwamba, sisi kama viongozi hatutataka Yanga itufie mikononi mwetu, hivyo tunahitaji kila anayeipenda timu hii ajitokeze kuisaidia kwa kila hali, mbali na hilo, pia tunaendelea kuangalia namna nyingine ya kukusanya fedha,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here