SHARE

LONDON, England

BEKI wa timu ya Liverpool, Virgil van Dijk, amedai kuwa baada ya kufanikiwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, wapo tayari kwa ajili ya kukusanya makombe mengine.

Kauli hiyo ya Van Dijk imekuja wakati ambao Liverpool bado wana kumbukumbu ya kulikosa kombe la Ligi Kuu England (EPL) msimu uliopita na kuwashuhudia Man City wakilichukua kwa msimu wa pili mfululizo.

Licha ya maumivu hayo ya kulikosa taji hilo, Liverpool walipambana vilivyo na kufanikiwa kubeba lile la Ligi ya Mabingwa (UEFA).

Kwa sasa Liverpool wapo kwenye mapumziko wakati huu ambapo michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwa inaendelea, kabla ya kuanza tena harakati za kulisaka taji lao la kwanza la EPL tangu msimu wa 1989/90.

Van Dijk, ambaye aliumaliza msimu uliopita kwa kunyakua pia tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka (PFA) kutokana na kiwango bora alichokionesha dimbani, alisema kuwa matumaini na ubora wa kikosi ni vitu vitakavyowabeba msimu ujao.

“Nadhani Liverpool msimu itakuwa vizuri zaidi. Kikosi ni kizuri mno na kina wachezaji wenye kiu ya kuwa bora zaidi na kuisaidia klabu kwa ujumla,” alisema Van Dijk.

Wiki kadhaa zilizopita beki huyo alitoka kuitumikia timu yake ya Taifa ya Uholanzi katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mataifa Ulaya dhidi ya Ureno, mechi ambayo hata hivyo walipoteza.

Kwa sasa ‘kitasa’ huyo pamoja na mabeki wengine wa Liverpool waliofanya vyema msimu uliopita; Trent Alexander-Arnold, Andy Robertson, Joel Matip na Dejan Lovren, wanafurahia kipindi cha mapumziko.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa washambuliaji wa klabu hiyo ambao kwa sasa wanazitumikia timu zao za taifa katika michuano inayoendelea kutimua vumbi Barani Afrika na Amerika Kusini.

Roberto Firmino yupo Brazil katika michuano ya Copa America, huku Sadio Mane na Mohamed Salah wakiziwakilisha timu zao za Senegal na Misri katika mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here