Home Makala Venus Williams ashikilia mafanikio ya Serena

Venus Williams ashikilia mafanikio ya Serena

462
0
SHARE
Serena Williams, left, and Venus Williams

LONDON, England

MARA tu baada ya Serena Williams kutwaa taji la 22 michuano mikubwa ya tenisi kwa wanawake, mjadala umeibuka kama anaweza kufikisha taji la 24 japo ni mtihani kufikia rekodi hii ya Margaret Court.

Raia huyo wa Marekani mwenyewe amekiri itakua vigumu kuendelea kucheza mchezo wa tenisi endapo dada yake Venus mwenye umri wa miaka 36 akiamua kustaafu jambo ambalo linaweza kumfanya na yeye kufikiria kuacha kucheza tenisi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Serena akiwa na umri wa miaka 34, alimfunga Mjerumani, Angelique Kerber 7-5, 6-3 na kufikia rekodi ya Steffi Graf ya kutwaa mataji 22 ya michuano mikubwa lakini Court na mataji yake 24 hayupo mbali.

Endapo Serena atapata nafasi ya kufanya hivyo (kufikia rekodi ya Court), basi itategemea zaidi dada yake.

Serena alisema hayo baada ya kufanikiwa kutwaa taji la pili mwishoni mwa wiki pale aliposhirikiana na Venus kutwaa ubingwa wa wazi Wimbledon kwa wachezaji wawili wawili upande wa wanawake.

Alipoulizwa kama anajiona ataweza kushindania mataji makubwa bila Venus kuwepo, nyota huyo wa tenisi upande wa wanawake alisema itakuwa ‘ngumu sana’ kufanya hivyo.

“Itakuwa ngumu,” alisema Serena. “Nani anayejua? Yeye amekuwa mhimili wangu mkubwa katika hii safari na tumekuwa pamoja kwa muda mrefu. Natumahi hatastaafu hivi karibuni. Itakuwa jambo la ajabu. Najua anapenda kuwa uwanjani akicheza na ninajua anatamani kuendelea kucheza zaidi.”

Imekuwa miezi 12 ya tabu kwa Serena tangu kutwaa taji hili kwa mara ya mwisho jijini London mwaka jana. Alipoteza kutwaa mataji yote makubwa ndani ya mwaka mmoja pale alipofungwa na Muitaliano Roberta Vinci kwenye fainali ya michuano ya wazi ya Marekani. Baadaye alishindwa kutwaa taji lake la 22 katika michuano ya wazi ya Australian na Ufaransa ambayo yote alifika fainali.

Alichanganyikiwa na kukosa usingizi kila alipojiona taji la 21 ndilo lililomg’ang’ania. “Haikuwa rahisi,” alisema Serena. “Nilikua nimepania kutengeneza historia lakini hesabu zilikuwa zinakataa.

“Kwangu mimi naweza kusema imekuwa mwaka mgumu. Nilikuwa na ushindi mwingi mzuri. Nilicheza vizuri sana lakini kuna wakati sikuwepo pale nilipokuwa nataka kuwepo.

“Finali za Australia, Ufaransa na pia ile ya Indian Wells na kushinda Rome, nilicheza tenisi nzuri lakini sikupata matokeo niliyokuwa nahitaji.”

Kocha wake, Patrick Mouratoglou, hivi karibuni alisema ‘Serena wa ukweli’ amerudi na ilibidi Serena kuulizwa nini alichokuwa anamaanisha kocha wake ambapo alijibu: “Ninawaahidi, siku moja nitaamka na kila kitu kubadilika. Ni jambo la kushangaza. Kwa kawaida haujui lakini unaihisi. Nilihisi kufarijika. Ilikuwa kama sasa sitahangaika kuwa na wasiwasi kuhusu mtu yeyote au kitu chochote. Ninataka tu niwe nawaza tenisi.

“Sitashughulika na nini watu wanachosema au wasichosema. Ninataka tu kuwaza kuhusu tenisi. Niliongea na Patrick, akanitumia ujumbe na kusema nimerudi.”

Alipoulizwa kuhusu raia wa Australia anayeshikilia rekodi ya kutwaa mataji ya michuano mikubwa mara nyingi aliyekutana naye mjini Perth mapema mwaka huu, Serena alisema: “Sijui mengi kumhusu Margaret Court isipokuwa alishinda mataji mengi.

“Nilikutana naye mwaka huu. Kumuona tu nilifarijika. Ni bingwa mzuri na mtu yeyote anayeweza kushinda hivyo ni dhahiri ni bingwa wa ukweli.”

Miezi 12 imemalizika kwa kutwaa mataji mawili katika michuano ya wazi ya Wimbledon wikiendi iliyopita na kama anavyosisitiza kocha wake, si vigumu kufikiri Serena amerudi. Je, ni kwa muda gani? Hilo litategemea na dada yake mkubwa Venus.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here