SHARE

MERSEYSIDE, England

INASIKITISHA kuiona Everton ikiwa katika mstari wa kushuka daraja, baada ya kichapo cha mabao 5-2 kutoka kwa Liverpool, mabosi hao wa Goodison Park walifikia maamuzi ya kumtimua Marco Silva.

Silva aliingia Everton akichukua mikoba ya Ronald Koeman, lakini alifukuzwa baada ya kikosi hicho kushindwa kufanya vizuri tangu mwanzo wa msimu huu.

Everton waliandamwa na matokeo mabaya licha ya kuwa moja ya klabu zilizotumia fedha nyingi katika usajili ili kuimarisha kikosi chao.

Kumekuwa na maswali mengi nani atapewa mikoba yake katika klabu hiyo, ingawa, kumekuwa na tetesi kuwa Vitor Pereira atachukua nafasi yake.

Pereira ni raia wa Ureno, lakini, ni ngumu kumfahamu kama haufatilii Ligi Kuu China ambako anafundisha klabu ya Shanghai SIPG FC.

Je, kocha huyo ni mtu wa aina gani? Ipi falsafa yake ya soka? Na mambo mengine kibao.

MOURINHO MWINGINE

Mashabiki wa Everton wanaweza kuwa katika mshangao mkubwa kwa kuongozwa na kocha mwingine raia wa Ureno baada ya Silva kuondoka na kushindwa kuwafikisha kwenye malengo.

Kama ilivyokuwa kwa Mourinho, hata Pereira hajacheza soka la ushindani sana, kwani alistaafu akiwa na miaka 28 tu, kabla ya kuamua kuwa kocha wa timu ya Daraja la Tatu nchini Ureno.

Bado anafanana na Mourinho hata kwenye kazi, kwani kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 sasa aliwahi kuifundisha FC Porto baada ya Andre Villas-Boas kutimkia Chelsea.

Mashabiki wa Everton watarajie mambo makubwa kutoka kwa kocha huyo Mreno.

ANAONGEA SANA

Pengine huu ni mfanano mwingine na Mourinho, lakini kocha huyo wa zamani wa Olympiacos haogopi kuongea chochote anapokuwa kwenye mahojiano.

Wakati akiwa kocha wa Porto, Pereira alisema ni mashindano ya kipuuzi na uchafu, kwani waamuzi waliandaa ubingwa uende kwa wapinzani wao Benfica.

Nyingine, alipokuwa akifundisha Al-Ahli ya Ufalme za Kiarabu, alishindwa kuzuia hisia zake na kuanza kubishana na mwongozaji wa mkutano wa waandishi wa habari.

KITAMBO ALIANZA KUFUKUZIWA

Jambo ambalo haulijui ni kwamba, hii si mara ya kwanza kwa Pereira kuhusishwa na Everton, iliwahi kutokea mwaka 2013 wakati David Moyes alipoenda Manchester United lakini kazi hiyo mwisho wa siku alipewa Roberto Martinez.

Hata hivyo, Martinez hakudumu ndani ya klabu hiyo. Naye alifukuzwa na kuanza kuingia makocha wengine kama Ronald Koeman, David Unsworth, Sam Allardyce na Marco Silva, wote hao ni kwa kipindi cha miaka miwili. Labda Pereira ataweza kukaa muda mrefu.

MSHINDI

Pereira amekuwa akifanikiwa katika ligi mbalimbali alizofundisha, kitu ambacho makocha wengine hawakuwa nacho kwa ajili ya kurudisha hali ya timu hiyo.

Alishinda ubingwa wa Ligi Kuu Ureno alipokuwa na Porto, Ugiriki alifanya hivyo na Olympiacos na huko China aliiongoza Shanghai SIPG kushinda taji lao la kwanza.

Ligi hizo zinaweza zisiwe na ubora mkubwa kama Ligi Kuu England, lakini ile hali ya ushindi inaweza kuwarudisha Everton na kuanza kushindania makombe kama FA na Carabao.

SI MKAAJI KWENYE TIMU

Katika kipindi cha miaka 15 alichofundisha soka, Pereira tayari amefundisha kocha wa timu tisa tofauti kwenye nchi sita tofauti.

Alikaa kwa kipindi kirefu alipokuwa Porto, ambako alikinoa kikosi hicho kwa miaka miwili tu.

Hiki ni kitu ambacho kinaweza kuwaweka mashabiki wa kikosi hicho cha Everton kwenye mashaka makubwa, kwani rekodi yake si nzuri katika timu ambazo anafundisha. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here