Home Habari VYUMA VIMEACHIA

VYUMA VIMEACHIA

1172
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

YANGA walikumbwa na misukosuko mingi kipindi cha hivi karibuni kutokana na tatizo la mishahara kwa wachezaji na pia kupata matokeo mabaya ikasemwa vyuma vimekaza, lakini sasa kauli hiyo imebadilika na inakuwa ‘vyuma vimeachia.’

Katika kipindi hicho iliripotiwa kuwa wachezaji waliamua kugomea mazoezi kutokana na madai yao ya mishahara, lakini sasa bilionea wao amerudi upya hali imekuwa kama Ulaya ndiyo maana ushindi unapatikana.

Mbali na tatizo hilo la mishahara, pia idadi kubwa ya wachezaji wa Yanga walikuwa wakisumbuliwa na majeraha hali iliyowafanya kukosa baadhi ya michezo, lakini sasa mambo yanakwenda vizuri na tayari wamechimba mkwara kwamba Simba hawatoki siku ya Oktoba 28, mwaka huu timu hizo zitakapokutana.

Baadhi ya wachezaji wao kama Obrey Chirwa, Geofrey Mwashiuya, Beno Kakolanya na Amis Tambwe, walikosa michezo ya ufunguzi kutokana na majeraha hayo, lakini sasa wameshapona na kilichobakia ni kazi tu.

Chirwa na Mwashiuya walilazimika kukosa michezo ya ufunguzi lakini wamerudi kwa kasi kubwa mfano mzuri ni jinsi Chirwa alivyoisaidia timu kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, akionyesha uwezo mkubwa.

Kwa upande wa Tambwe ambaye tangu kujiunga na kikosi hicho amekuwa msaada mkubwa kutokana na kufunga mabao mengi na muhimu, hajacheza mchezo wowote tangu ligi ianze lakini amepona na anasubiri tu mchezo dhidi ya Simba.

Donald Ngoma na Thaban Kamusoko ambao pia walikosa mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar, nao wapo vizuri ambapo wamepumzishwa mchezo ujao dhidi ya Stand United ili kusubiri hiyo Oktoba 28.

Jambo kubwa na la kufurahisha ni kwamba, kwa sasa huwezi kusikia wakilia njaa baada ya bilionea wao kuamua kurudi upya ambapo taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho zinadai kuwa, wakimaliza mchezo huo dhidi ya Stand United wanaweza wakaenda Pemba kuwawinda Simba.

Kwa sasa kambi ya Yanga iliyoko mjini Tabora iko vizuri na wanachotaka ni kumalizia kazi ya kuondoka na pointi sita Kanda ya Ziwa.

Yanga wameamua kuweka kambi mjini Tabora kabla ya kurejea mjini Shinyanga ambako watawavaa Stand United wikiendi hii.

Mmoja wa maofisa wa Yanga ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, watajiandaa vizuri na kurekebisha mambo kadhaa ambayo wameyaona katika mechi yao dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa mujibu wa kigogo huyo, licha ya kwamba timu hiyo itacheza na Stand United Jumapili ijayo, lakini tayari wamekwishaanza mipango ya kuwazima Simba muda mrefu hivyo mchezo wao dhidi ya Wapiga debe wa Shinyanga wala hauwaumizi kichwa.

“Mchezo wetu dhidi ya Stand mwishoni mwa wiki wala hautuumizi kichwa, kwani mipango yetu ni kuhakikisha tunawafunga Simba na kukaa rasmi kileleni na tukishafika hapo hakuna atakayetushusha.

“Hao Stand United tutawafunga tu kwani hawawezi kutuzuia ndiyo maana akili zetu tumezihamishia kwa Simba Oktoba 28, mwaka huu, mikakati yetu imeanza muda mrefu sana,” alisema.

Wakati hayo yakiwa upande wa Yanga, kwa upande wa Simba nako hali si mbaya kwani licha ya hofu iliyokuwa imetanda kwamba huenda wakamkosa straika wao, John Bocco, kutokana na majeraha aliyoyapata walipokutana na Mtibwa Sugar, uongozi umethibitisha kuwa atakuwepo kuwakabili Yanga.

Bocco alipata majeraha hayo mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki hii Uwanja wa Uhuru na kumalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, lakini sasa naye atapumzishwa mchezo ujao dhidi ya Njombe Mji ili kuisubiri Yanga.

Taarifa kutoka Simba zinadai kuwa kikosi hicho kikimaliza tu kucheza na Njombe Mji, kinakwenda kuweka kambi Unguja kujiwinda na Yanga ambapo licha ya kwamba watamkosa beki Salum Mbonde, hiyo haina shida kwani Jjuuko Murushid atasaidiana na Method Mwanjali katika safu ya ulinzi.

Mbali na hivyo, kiungo wa timu hiyo aliyesajiliwa kutoka Yanga, Haruna Niyonzima, ameahidi kufanya maajabu ili kufuta kelele za mashabiki wanaodai kwamba ameshuka kiwango.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here