SHARE

LONDON, England


MWEZI Januari katika soka huwa ni mwezi mgumu mno kwa usajili wa wachezaji. Baadhi ya makocha hujitahidi kuepukana na matumizi kwenye dirisha hili dogo la usajili, huku wengine wakinyakua mchezaji mmoja au wawili kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao.

Lakini kuna wakati ambao timu hizo hufanya usajili wa maana mno kwenye dirisha dogo, ambapo husukumwa zaidi na vita ya kuwania ubingwa, tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na hata wale walio kwenye harakati za kutoshuka daraja na hapa Daily Mail imeorodhesha wachezaji bora waliosajiliwa katika dirisha dogo Januari.

 

  1. Mikel Arteta

Januari 2004, David Moyes alikabiliwa na mtihani mkubwa wa nani atakayerithi nafasi ya Thomas Gravesen, aliyekuwa njiani kuelekea Real Madrid.

Mtihani huo ulimjia katika kipindi ambacho Everton ilikuwa kwenye vita ya kuwania tiketi ya kushiriki UEFA, hivyo Moyes alichemsha kichwa na mwisho wa siku akambeba kwa mkopo Mikel Arteta kutoka Real Sociedad, ambapo mechi 12 tu alizochezeshwa ziliisaidia Everton kumaliza nafasi ya nne kabla hajasaini mkataba wa muda mrefu.

  1. Asmir Begovic

Kwa muda wa mwezi mzima hadi ilipofika mwanzoni mwa Februari 2010, klabu za Tottenham na Stoke zilivutana sana mashati kuiwania saini ya mlinda mlango Begovic, ambaye aliwekwa sokoni na timu yake ya Portsmouth iliyokuwa ikikabiliwa na ukata.

Na baada ya vuta nikuvute hiyo, Begovic akaichagua Stoke, lakini alikabiliwa na changamoto ya kumpokonya namba Thomas Sorensen.

Alisubiri sana hadi alipokuja kupata nafasi, na hakuichezea, alifanya kazi nzuri hadi Chelsea ilipomuona na kumsajili kwa dau la pauni milioni 3.25 miaka michache baadaye.

  1. Clint Dempsey

Mmarekani huyo alinyakuliwa na Fulham, Januari 2007 na thamani yake ya pauni milioni 2 ilionekana kwa mabao aliyoyafunga ndani ya klabu hiyo.

Bao lake la kwanza alilifunga Mei mwaka huo, walipoichapa Liverpool bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, kabla ya kufanya makubwa ndani ya miaka mitano aliyoishi ndani ya dimba la Craven Cottage, pia akiisaidia kutinga fainali ya Ligi ya Europa.

  1. Nemanja Matic

Kwa mshangao wa wengi, Mserbia huyo alirudishwa Stamford Bridge Januari 2014 kwa dau la pauni milioni 21, baada ya Chelsea kumuuza kwenda Benfica, kila mtu aliwaona Chelsea kama wamechanganyikiwa.

Lakini ndani ya msimu huo huo, Matic alionesha ukomavu kwenye eneo la kiungo cha ukabaji na akawasaidia kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.

  1. Daniel Sturridge

Alipokuwa Chelsea kila mtu alishaona Sturridge ndio amefika mwisho wa maisha yake ya soka, mabao yalikauka na hata kama alifunga basi ni baada ya kukosa nafasi nne au tano za wazi.

Lakini alipotua Liverpool Januari 2013 kwa dau la pauni milioni 12, Sturridge akabadilika na kurudi kwenye ukali wake wa kushambulia na almanusura Liverpool itwae ubingwa wa Ligi Kuu England.

  1. David Luiz

Beki huyo wa kati raia wa Brazil alitua Chelsea Januari 2011 kwa dau la pauni milioni 21 akitokea Benfica.

Tangu kipindi hicho, Luiz ameikonga mioyo ya mashabiki wengi wa ‘The Blues’, akikumbukwa kwa jitihada zake za kuisaidia timu kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na majeraha.

Hata hivyo, Chelsea ilimuuza kwa ada ya pauni milioni 50 kwenda PSG na miaka miwili baadaye (mwaka huu) wakamsajili tena.

  1. Christophe Dugarry

Usajili wa mkopo walioufanya Birmingham City Januari 2003, kwa kumchukua straika huyu wa zamani wa Ufaransa kutoka Bordeaux ni mfano mzuri wa timu zilizofanya biashara ya faida ulipofika mwezi huo.

Dugarry aliisaida kwa asilimia kubwa timu hiyo isishuke daraja mwaka huo kwa kupachika mabao matano muhimu ndani ya mechi nne, ambapo timu yake hiyo iling’atuka kutoka kwenye janga la kushuka daraja hadi ya nafasi ya 13.

  1. Patrice Evra

Sir Alex Ferguson alimnyakua beki huyo wa kushoto kutoka AS Monaco kwa dau la pauni milioni 5.5, Januari 2006.

Mchezo wake wa kwanza dhidi ya Man City kipindi cha pili haukuwa mzuri sana, lakini kadri miezi ilivyoendelea kukatika, Evra akafanikiwa kuwa mmoja wa mabeki bora wa klabu na ligi kwa ujumla. Evra alinyakua mataji matano ya ligi na moja la UEFA chini ya utawala thabiti wa Ferguson.

  1. Nemanja Vidic

Huu nao ulikuwa ni usajili bora uliowahi kufanywa na United katika dirisha dogo la Januari, ambapo mwaka 2006 Ferguson aliifanyia ‘umafia’ klabu ya Fiorentina ambayo ilikuwa mbioni kumsainisha, kwa kutoa ofa ya pauni milioni 7, akitokea Spartak Moscow.

Msimu wa kwanza kwa Vidic pale United, ndani ya mwezi na nusu tu alitwaa Carling Cup na kwa kushirikiana na Rio Ferdinand, United ilikuwa na safu ngumu ya ulinzi iliyowapa taji la ligi kuu msimu uliofuata. Hadi Vidic anaondoka United, bado anaheshimika kuwa ni mchezaji bora aliyetua England kwenye dirisha dogo la usajili wa Januari.

  1. Luis Suarez

Anayekamata nafasi ya kwanza kwenye orodha hii ni Luis Suarez. Mtu hatari aliyekosa bahati ya kunyakua taji la ligi kuu pale ilipoonekana ni jambo lililowezekana.

Januari 2011, kocha wa zamani wa Liverpool, Kenny Dalglish alimnyakua mkali huyo kwa dau la pauni milioni 22.8 kutoka Ajax na kwa misimu minne aliyoichezea klabu hiyo alifanya makubwa hadi kuwa mmoja wa washambuliaji hatari kuwahi kuchezea Ligi Kuu England.

Liverpool walikuwa na bahati kuwa naye, kwani alikuwa na uwezo wa hali ya juu wa upachikaji mabao ambapo wastani wake ulikuwa ni zaidi ya bao moja kwa kila michezo miwili na msimu wake wa mwisho alitisha zaidi kwa kupachika mabao 31 ndani ya mechi 33 za ligi.

SHARE
Previous articleMGHANA WA AZAM AITAMANI YANGA
Next articleKARIBU 2017

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here