SHARE

NA WINFRIDA MTOI

BAADHI ya wachezaji wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara, wamelalamikia kupitia katika kipindi kigumu cha kiuchumi kutokana na hali inayoendelea,  ikiwamo michezo kusimama.

Ligi Kuu imesimama tangu mwezi uliopita kutokana na janga la Corona lililovamia takriban  dunia nzima, hivyo kila mchezaji  kurejea nyumbani hadi pale hali itakapokuwa shwari.

DIMBA limezungumza na wachezaji mbalimbali kuzungumzia hali wanayopitia mtaani, lakini wengi walilalamikia maisha magumu kutokana na kukosa fedha.

Kati ya wachezaji waliozungumza kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini walisema, waliondoka katika timu zao wakiwa wanadai mishahara na posho  hali iliyowafanya wasipewe chochote hadi sasa.

“Huku mtaani kugumu jamani, hii Corona iishe tu, maisha yamekuwa magumu sana, bora tulivyokuwa kambini, kiongozi unaweza kumlilia shida akakusaidia.

“Ila huku utapiga simu hadi utachoka,wengine tunadai mishahara ya miezi miwili, upon a familia nyumbani, mama watoto haelewi kabisa,” alisema  mmoja ya wachezaji hao.

Mchezaji mwingine, alisema changamoto hiyo inawafanya washindwe hata kufanya mazoezi kwa umakini kwa sababu wanafikiria  familia  na fedha imekata.

Kutokana na malalamiko hayo, DIMBA liliwatafuta baadhi ya viongozi wa klabu mbalimbali na kukiri kuwa, posho walizokuwa wanawapa wachezaji kila siku kwa sasa hakuna zaidi ya kusubiri mishahara.

“Suala la posho kweli hakuna, ila mshahara wa wachezaji uko pale pale wanapata kila mwezi kwa sababu hiyo ni bajeti ilikuwepo tangu mwanzo wa msimu,” alisema Emmanuel Kimbe Katibu Mkuu wa Mbeya City.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Allince FC, Nyaitati Stephano, alisema wachezaji wao wanadai mshahara wa Aprili pekee.

Stephano alisema kutokana na hali ilivyo wanaweza kuathirika katika miezi ijayo kwa sababu mapato yao wanategemea katika shule zao wanazomiliki.

“Shule zote nchini zimefungwa na sisi  kati ya vyanzo vyetu vya mapato tunategemea ada zinazolipwa na wanafunzi wanaosoma katika shule za Alliance,  hivyo miezi inayokuja hali inaweza kuwa tofauto,” 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here