Home Habari WACHEZAJI YANGA WANUKIA UTAJIRI

WACHEZAJI YANGA WANUKIA UTAJIRI

6455
0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE


ILI kuonyesha kweli wana nia ya kufanya vizuri katika michezo yao ya kimataifa, uongozi wa Yanga umeamua kutoa Sh bilioni 1.3 kwa wachezaji endapo watafanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga jana walicheza mchezo wao wa kwanza wa raundi ya pili Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers ya Botswana katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mchezo huo, uongozi ulikutana na wachezaji na kuwapa hamasa juu ya mchezo huo kwa kutoa ahadi kuwa watawapa fedha yote ambayo watapewa na Caf kama wataitoa timu hiyo na kutinga robo fainali.

Iwapo Yanga itatolewa katika hatua hii, itashushwa hadi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na kusubiri washindi wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo ambayo wapinzani wao Simba wanashiriki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili wa klabu ya Yanga, Hussein Nyika, alisema ni kweli wamewaahidi fedha nyingi kama watafanikiwa kuwatoa Wabotswana hao, ingawa hakukubali kuwa ni kiasi kikubwa kiasi hicho.

“Hatujawaahidi fedha yote hiyo, ila tumetoa ahadi nono kwa kila mchezo, endapo watashinda katika michezo yote miwili wa jana na kila mchezo una ahadi yake ili kuwapa hamasa ya kufanya vizuri,” alisema Nyika.

Alisema endapo watawatoa kabisa kwenye michuano wapinzani hao, kuna hela nzuri na kubwa zaidi, ambapo hakutaka kuweka wazi kuwa ni kiasi gani kutokana na makubaliano ya Kamati ya Utendaji kuwa wasitangaze dau kwenye vyombo vya habari.

Nyika aliongeza kuwa zawadi walizoahidi ni makubaliano ya uongozi mzima wa Yanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here