Home Makala WAKALA TAJIRI ALIYEMPELEKA RONALDO REAL MADRID

WAKALA TAJIRI ALIYEMPELEKA RONALDO REAL MADRID

6876
0
SHARE

LISBON, URENO


UNAPOTAJA majina ya mawakala wanaofanya kazi yao katika ubora wa hali ya juu katika soka la Ulaya, ni ngumu kulikosa jina la wakala raia wa Ureno, Jorge Paulo Agostinho Mendes ambaye anamiliki Kampuni ya GestiFute aliyoisajili mwaka 1996.

Wakala huyo umaarufu wake unatokana na kuwasimamia nyota wengi wenye majina makubwa barani Ulaya pamoja na Amerika.

Mendes alizaliwa Januari mwaka 1966 huko Lisbon, ambapo alikuwa akiishi katika kota zilizokuwa za wafanyakazi wa Kampuni ya Petrogal zilizopo katika jiji hilo nchini Ureno.

Wazazi wa wakala huyo walikuwa na kipato cha kati, baba yake alikuwa mfanyakazi wa kiwandani wakati mama yake mzazi alikuwa fundi wa kushona kofia na vikapu.

Zifuatazo ni dondoo tano za wakala, Jorge Mendes, wakala mwenye jina kubwa aliyefanikisha dili nyingi kubwa barani Ulaya.

Sajili zake tatu ghali

Kati ya sajili ambazo ziliushtua ulimwengu wa mchezo wa soka ambazo zimebaki katika kumbukumbu ya mafaili ya wakala huyo, ni ule Cristiano Ronaldo kutoka Manchester United kwenda Real Madrid uliogharimu Euro milioni 83.

Usajili uliofuata ulimhusisha James Rodriguez kutoka Monaco kutua Madrid kwa kiasi cha Euro milioni 63, huku Angel Di Maria kutoka Madrid kwenda Manchester United ambao ulikuwa wa kiasi cha Euro milioni 59.

Anamiliki utajiri bilioni 172

Mkali huyo ambaye alikuwa akifanya kazi ya kuonyesha filamu, hivi sasa anamiliki utajiri wa dola milioni 76.9 ambazo ni sawa na bilioni 172 za Kitanzania kutokana na mauzo ya wachezaji pamoja na mikataba ya makocha ambao anawasimamia.

Kampuni yake inamiliki wanamichezo 53

Mmiliki huyo wa Kampuni ya Gestifute, anamiliki zaidi ya wanamichezo 50 ambao miongoni mwao ni wacheza soka pamoja na makocha wa mchezo huo.

Baadhi  ya  nyota wanaomilikiwa na wakala huyo ni pamoja na Cristiano Ronaldo, James Rodríguez, Pepe, Marcelo, Di María, Diego Costa, Adrián, Quaresma, Mangala, Falcao, Carvalho, Moutinho, De Gea, Bruno Alves na  Bernardo Silva.

Wengine ni Jose Mourinho, Nuno Espíritu Santo, Thiago Mota, William Carvalho, Ederson Morares, Bosingwa, Ezekiel Garay, Carlos Vela, Rubén Neves, André Gomes na Fabinho.

Mteja wake wa kwanza ni kocha Nuno Espirito

Akiwa na miaka 20, alikuwa akicheza soka katika klabu inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, lakini mambo yalipomuendea kombo, aliamua kuachana na mpira na kufanya kazi katika kumbi za starehe ili kujikimu ndipo alipokutana na Nuno Espirito Santo, kocha wa FC Porto, wakati huo alikuwa mchezaji wa Vitória Guimarães.

Alikuwa mfunga Ice Cream

Kila mwanadamu ana mapito yake, kupiga moyo konde na kuendelea kurusha hatua ni ushujaa, ndivyo ilivyo kwa wakala huyo ambaye maisha yake ya utotoni yalijaa mitihani mingi ambapo kuna kipindi alilazimika kufunga ice cream ili kujikimu, lakini hakukata tamaa na kuamini katika ndoto zake ambapo hivi sasa anakula matunda ya uvumilivu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here