Home Makala WALIOCHEZA CHINI YA KIWANGO KARIAKOO ‘DERBY’

WALIOCHEZA CHINI YA KIWANGO KARIAKOO ‘DERBY’

882
0
SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

HATIMAYE joto la mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga lilimalizika rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita, kwa kuushuhudia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo Simba waliweza kuondoka uwanjani wakiwa kifua mbele kwa kushinda mabao 2-1.

Huu ulikuwa ushindi wa kwanza wa Simba dhidi ya Yanga, tangu uongozi wa Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva, achukue kijiti cha kuiongoza timu hiyo kutoka kwa Alhaji Ismail Aden Rage mwaka 2014.

Baada ya mchezo huo kumalizika na mengi kuzungumzwa, DIMBA Jumatano lilifuatilia mchezo huo kwa makini na kubaini baadhi ya wachezaji waliocheza chini ya kiwango na kushindwa kuwa msaada katika mchezo huo.

Simon Msuva

Msuva ni kati ya wachezaji waliouanza vizuri mchezo huo kwa kuwapindua atakavyo mabeki  wa Simba kwa dakika 15 za kipindi cha kwanza, lakini tangu hapo mpaka mwamuzi wa mchezo huo, Mathew Akrama anapuliza kipyenga cha kuashiria kumaliza mchezo huo, Msuva hakuwa na madhara makubwa kwa Simba, licha ya kufunga bao la Yanga kwa mkwaju wa penalti.

Msuva na Obrey Chirwa waliwaweka kwenye wakati mgumu walinzi wa Simba na kusababisha dakika ya tatu ya mchezo huo, beki Novartus Lufunga kusababisha penalti ambayo ilikwenda kufungwa na Msuva.

Baada ya Msuva kufunga penalti hiyo hakuonyesha kucheza kwa ajili ya kuisaidia timu, alicheza chini ya kiwango, hakuwa tena na madhara ndani ya eneo la hatari la Simba.

Hatua hiyo iliwafanya Simba watoke nyuma na kusawazisha bao la kwanza dakika ya 14, baadaye kupachika bao la pili lililoumaliza mchezo huo, Yanga ikikubali kichapo cha mabao 2-1.

Novartus Lufunga

Kama kuna mchezaji wa Simba ambaye hakuwa mchezoni katika pambano hilo, basi ni Lufunga, ambaye alishindwa kabisa kuendana na kasi za washambuliaji wa Yanga waliokuwa na kasi langoni mwa Simba.

Lufunga hakuwa makini kwenye maamuzi yake mengi na kufanya asababishe penalti ya kizembe baada kushindwa kuumiliki mpira, kwa kumkaba kwa nyuma Obrey Chirwa, aliyemzidi maarifa kwa umiliki wa mpira huo na beki kumkwatua kwa nyuma.

Baada ya kufanya kosa hilo, mashabiki wa Simba hawakuwa na imani na mlinzi wao na kulifanya benchi la ufundi lililo chini ya Mcameroon, Joseph Omog kumtoa beki huyo nafasi yake ikichukuliwa na Shiza Kichuya.

Haji Mwinyi

Mwinyi, mlinzi mahiri upande wa kushoto hivi sasa, hakuwa katika kilele cha ubora wake katika mchezo huo, kwani mabao yote ya Simba yalipitia upande wake wa kushoto.

Mlinzi huyo wa zamani wa timu ya KMKM ya Visiwani Zanzibar hakuweza kabisa kusimama imara katika eneo lake kuondosha hatari nyingi zilizolenga upande wake na kusababisha makosa ya kizembe yaliyoigharimu timu.

Kichuya, mfungaji wa bao la pili la Simba, aliweza kumtambuka yeye kabla ya kuachia shuti kali la chini lililomshinda mlinda mlango Deogratius Munishi ‘Dida’, ambaye hakuwa na la kufanya.

Deogratius Munishi ‘Dida’

Mlinda mlango huyo namba moja wa Yanga kwa siku za hivi karibuni hakuwa vizuri katika mchezo huo na alishindwa kusimama vyema kulilinda lango lake.

Ndani ya mchezo Dida alifanya makosa ya kizembe na kuleta hatari nyingi langoni mwake. Dida alishindwa kuwasiliana vyema na mabeki wake, hatua iliyomfanya Kelvin Yondani ‘Vidic’ kumfokea mara kwa mara.

Haikuwa kawaida kwa Dida yule mwenye ubora wake anapodaka mpira, haijalishi timu inaongaza idadi ngapi ya mabao au imepoteza anakuwa mwepesi kuanzisha mpira kutoka mikononi mwake, lakini siku hiyo ilikuwa tofauti, dakika za mwanzo kabisa alionekana kupoteza muda, kitendo kilichomfanya mwamuzi kutoa adhabu ya ‘indirect football’.

Haruna Niyonzima ‘Fabregas’

Niyonzima ndiye aliyekuwa nahodha wa Yanga, lakini alishindwa kuonyesha uongozi wake juu ya wachezaji wenzake ndani ya uwanja.

Niyonzima, aliyeanza nafasi ya kiungo wa pembeni, alishindwa kurudi nyuma kumsaidia mlinzi wake, Haji Mwinyi na kusababisha hatari zote za mabao ya Simba kupitia upande huo.

Haikutosha hiyo, kwa kujua uzito wa kitambaa chake mkononi, ilimpasa aunganishe timu, ikiwamo kuwasiliana kila mara, hakulifanya hilo.

Nyota huyo, ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, taarifa zinadai ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga walioko kikaangoni baada ya mchezo huo kumalizika, wakidai alionekana kucheza vibaya na kuwakera mashabiki na wanachana wa Yanga waliofura kwa hasira baada ya mchezo huo kumalizika.

Juma Luizio

Luizio, aliyeko Simba kwa mkopo akitokea Zesco United ya Zambia, alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba walioshindwa kutekeleza vyema majukumu yake uwanjani na kusababisha benchi la ufundi limfanyie mabadiliko mwanzoni mwa kipindi cha kwanza. Katika mabadiliko hayo, nafasi yake ilichukuliwa na Said Ndemla, aliyetimiza majukumu yake ya soka la kusisimua kwenye eneo la kiungo.

Luizio  alishindwa kwenda sawa na kasi za wachezaji wa Yanga ambao mwanzoni mwa kipindi cha kwanza walitawala eneo kubwa la uwanja, ambapo Omog alishtuka mapema kama kijana wake mechi ilikuwa kubwa kwake na kumuachia nafasi hiyo fundi Ndemla.

Andrew Vicent ‘Dante’

Dante alishindwa kabisa kumzuia vema straika wa Simba, Laudit Mavugo, ambaye aliisumbua muda mrefu  beki hiyo ya kati aliyokuwa sambamba na Kelvin Yondani.

Beki huyo mara kwa mara alikuwa akiunganishwa ‘tela’ na kama Mavugo angekuwa makini katika mchezo huo angefunga zaidi ya mabao matatu.

Hilo lilidhibitika kwa bao la kusawazisha la kichwa alilofunga Mavugo, akifanya hivyo mbele yake kwa kushindwa kuokoa krosi iliyopigwa na Shiza Kichuya na kufanya Mavugo aruke juu peke yake na kufunga bao kwa kichwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here