Home Habari Wamenyamaza

Wamenyamaza

328
0
SHARE
 • Yanga yarejea kileleni
 • Yampiga mtu ‘Mkono’
  NA SAADA SALIM
  MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wamezima kelele za watani zao wa jadi, Simba, baada ya kufanikiwa kuwapiga kumbo na kurejea kileleni kufuatia ushindi mnono wa mabao 5-0 waliopata jana dhidi ya ‘Wanakimanumanu’ African Sports.
  SIMBA-YANGA-3Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Yanga ilicheza kandanda la kuvutia kwa dakika zote 90 na kumfanya Kocha wake Mkuu Mholanzi, Hans van der Pluijm, kutabasamu muda wote.
  Wakifahamu wazi kuwa wanatakiwa kushinda mchezo huo ili kurejea kileleni na kuwaengua Simba, Yanga waliuanza mchezo huo kwa kasi kubwa, wakipeleka mashambulizi ya nguvu langoni mwa African Sports.
  Mastraika wa Yanga, Donald Ngoma, Amis Tambwe na Deus Kaseke, walitumia muda kuhemea langoni mwa African Sports na kujikuta wakiwapa wakati mgumu mabeki wa timu hiyo kufanya kazi ya ziada ya kuuokoa.
  Yanga walianza kujiandikia bao la kwanza kupitia kwa beki wake, Kelvin Yondani, dakika ya 32 kwa shuti kali ambalo lilimgonga Thaban Kamusoko na kujaa wavuni, ikiwa ni kazi nzuri iliyofanywa na Deus Kaseke, aliyepiga pasi kali kutoka wingi ya kulia.
  Dakika ya 37 Donald Ngoma alifunga bao maridhawa kwa ‘tiktak’ mithili ya lile alilofunga Wayne Rooney wa Manchester United dhidi ya Manchester City, akiunganisha krosi ya Juma Abdul kutoka wingi ya kulia na kuiandikia Yanga bao la pili.
  Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Yanga ilikuwa mbele kwa mabao hayo mawili.
  Kipindi cha pili Yanga walikianza kwa kasi kubwa na kufanikiwa kupata bao la tatu kupitia kwa Mrundi Amis Tambwe dakika ya 51, akiwazidi mbio mabeki wa African Sports, kutokana na pasi ndefu iliyopigwa na Haruna Niyonzima na kufunga kirahisi.
  Dakika ya 59 Yanga walidhihirisha kuwa hawapo kwenye utani baada ya kufanikiwa kupachika bao la nne kupitia kwa Mateu Anthony kwa kichwa, akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Haji Mwinyi kutoka wingi ya kushoto.
  Tambwe alikamilisha karamu ya mabao dakika ya 72, akifunga bao zuri kwa shuti kali la mguu wa kushoto baada ya kupenyezewa pasi nzuri na Kamusoko, ambapo mpaka dakika 90 za mchezo huo zinakamilika Wanajangwani hao walirudi kileleni kwa kishindo.
  Kwa matokeo hayo, Yanga wamewaengua Simba kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 50 na kuwaacha Wekundu hao wa Msimbazi katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 48, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Azam FC yenye pointi 47.
  Katika mchezo huo, Yanga iliwakilishwa na Ally Mustafa, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Vicent Bossou/Paul Nonga, Pato Ngonyani, Deus Kaseke/Salum Telela, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma/Matteo Anthon, Amis Tambwe pamoja na Haruna Niyonzima.
  Kwa upande wa African Sports, golini alikaa Kabali Faraji, Mwaita Ngereza, Hamza Kassim/Khalfan Twenye, Juma Shemvuni, Rahim Juma, Ally Ally, Husein Issa, Pera Mavuo, Rajab Isihaka, James Mendi na Omar Issa/Mohamed Mtindi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here