Home Habari WANAOACHWA SIMBA, YANGA HAWA HAPA

WANAOACHWA SIMBA, YANGA HAWA HAPA

8449
0
SHARE

EZEKIEL TENDWA NA SAADA SALIM

WAKATI dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu, timu kongwe za Simba na Yanga zimetajwa kutaka kutema baadhi ya wachezaji wao ili kuingiza maingizo mapya.

Timu hizo zinafahamu kwamba mwakani zinakabiliwa na michuano migumu ya kimataifa, na sasa zinataka kusafisha wachezaji ambao wanaonekana ni mizigo na kuingiza wapya wenye uwezo mkubwa.

Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wataiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba wakishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho, baada ya kukaa kwa misimu kadhaa bila kufanya hivyo.

Baadhi ya wachezaji ambao wanatajwa kwamba huenda wakakutana na panga kwa upande wa Yanga yupo Donald Ngoma pamoja na Mrundi Amis Tambwe, ambao msimu huu wameshindwa kufanya kile ambacho kilitarajiwa.

Ngoma amecheza michezo michache na baada ya hapo akatimkia kwao Zimbabwe bila ruhusa ya uongozi wala benchi la ufundi, ambapo wenye Yanga yao wamekasirika wakitaka aondoke asije akajifanya ‘Mungu mtu.’

Kwa upande wa Tambwe, tangu msimu huu uanze hajagusa nyasi za uwanja kutokana na majeraha aliyoyapata msimu uliopita na taarifa kutoka Yanga zinadai kuwa, wanafikiria kumtema ili asije akawagharimu mbele ya safari, ikizingatiwa kuwa, timu inashiriki michuano ya kimataifa.

“Ngoma yeye kuna asilimia kubwa ya kumtema kutokana na ukweli kwamba, anajiona yeye ni mfalme anaweza kufanya lolote, ndiyo maana amekwenda kwao bila taarifa kwa uongozi, kwa Tambwe dalili zinaonyesha naye yatamkuta makubwa, kwani majeraha yanaweza yakamsababishia kushindwa kushiriki vizuri Ligi ya Mabingwa.

“Lililopo ni kwamba, tunataka kusajili washambuliaji wazuri watakaoziba mapengo yao, kwani Yanga ni timu kubwa ambayo mashabiki wake siku zote wanataka matokeo mazuri,” alisema kigogo mmoja kutoka Yanga.

Wachezaji wengine ambao taarifa zinasema ama watatemwa jumla au kutolewa kwa mkopo ni kipa Beno Kakolanya, Juma Mahadhi na Matheo Anthony, ingawa mchujo bado unaendelea kwa wengine.

Kwa upande wa Simba, taarifa zinadai kuwa, beki Mzambia, Method Mwanjali na straika Mrundi, Laudit Mavugo, wapo kwenye hali tete na kamati ya usajili ambayo ilitarajiwa kukaa wikiendi hii, inaweza kutoka na jibu moja.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa, wanataka kumtema Mwanjali kwa kigezo cha umri, ambao wenyewe wanadai ndio unaosababisha achelewe kupona pindi anapoumia, huku Mavugo naye akidaiwa kutokuwa na ile kasi yake ya upachikaji mabao aliyokuwa nayo katika klabu yake ya Vital’O ya Burundi akiwa Simba.

Taarifa hizo zinadai kuwa, huenda Mavugo akatimkia kwa mabingwa wa Ligi Kuu nchini Kenya, Gor Mahia, ambayo inanolewa na kocha wa zamani wa Wekundu hao wa Msimbazi, Dylan Kerr.

Mbali na wawili hao, pia wapo wanaotajwa kwamba watatolewa kwa mkopo kwenye timu nyingine, akiwamo winga Jamal Manyate, Jamal Mwambeleko na Juma Luizio, ambaye inadaiwa kuwa ameweka bayana kwamba, anataka kupewa barua ya kutemwa akatafute maisha kwingine.

Baada ya taarifa hizo kulifikia DIMBA, lilimtafuta Katibu Mkuu wa Simba, Arnold Kashembe, ambaye alikiri kwamba kamati ya usajili inakutana ili kupitia ripoti ya benchi la ufundi na ndio watakaotoka na jibu la moja kwa moja.

“Hao wachezaji uliowataja (Mwanjali na Mavugo) kwamba wanatemwa hilo sina uhakika nalo, isipokuwa subiri mpaka kamati ya usajili itakapokaa na kumaliza kazi yake. Wenyewe wanaweza kukaa siku hizi mbili, naamini wanaweza wakatoka na jibu.

“Nikuhakikishie tu kwamba, mchakato wa usajili unaendelea na kamati husika inakutana wikiendi hii kupitia na kuangalia mahitaji ya benchi la ufundi na baadaye kila kitu kitawekwa wazi,” alisema.

Licha ya Katibu huyo kutoweka wazi majina ya wachezaji wanaoondoka, lakini DIMBA lilipata taarifa kutoka kwa mmoja wa vigogo wa Simba kwamba Mavugo na Mwanjali wapo kwenye mstari mwekundu.

Dirisha dogo la usajili wa wachezaji linafunguliwa rasmi Novemba 15, siku ya Alhamisi wiki ijayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here