Home Habari Wanaume Yanga warejea mzigoni

Wanaume Yanga warejea mzigoni

529
0
SHARE
yanga
Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi.

NA EZEKIEL TENDWA,

YANGA kweli imepania kufanya kweli. Kwani baada ya kutwaa mataji mawili ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na lile la FA, wachezaji walipewa muda wa wiki kwenda kula bata na familia zao lakini kuanzia jana benchi la ufundi la timu hiyo limewaita tena mzigoni ‘wanaume wote’ kuanza mazoezi fulani ya nguvu kama wanajeshi.

Kikosi hicho kilianza rasmi mazoezi yao jana asubuhi katika Uwanja wa Chuo cha Polisi kikiwa chini ya kocha msaidizi, Juma Mwambusi, huku nyota kadhaa wapya akiwemo Hassan Ramadhani Kessy wakianza kazi rasmi, huku wakimsubiri Kocha Mkuu Mholanzi, Hans Van de Pluijm, ambaye anaanza kazi leo.

Mbali na Pluijm, wachezaji wengine wa kigeni nao wanatarajiwa kuungana na wenzao leo wakiongozwa na Wazimbabwe, Thaban Kamusoko na Donald Ngoma ambao walikuwa nchini kwao kwa ajili ya mapumziko baada ya kufanya kazi kubwa ya kuisaidia timu yao.

Licha ya kwamba kikosi hicho kinafanya mazoezi uwanja huo wa Polisi ambao una ulinzi mkali, lakini DIMBA Jumatano linafahamu kuwa wachezaji waliokuwepo walifanya mazoezi ya nguvu chini ya Mwambusi na hii ni kutokana na kazi kubwa waliyonayo mbele ya safari.

Wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kuungana na wenzao leo ni pamoja na kipa Beno Kakolanya kutoka Tanzania Prisons ya jijini Mbeya pamoja na beki wa Mtibwa Sugar, Andrew Vincent ambao usajili wao ulikuwa wa kushtukiza juzi.

Kessy jana alijituma sana mazoezini akijua fika kwamba ana kazi kubwa kumshawishi Pluijm kumpa namba mbele ya Juma Abdul ambaye kwa sasa ni mmoja wa mabeki wa kutumainiwa.

Hata hivyo, kutokana na uwezo wa Kessy ni wazi Pluijm hatakosa sehemu ya kumuweka hata kama ni kumsogeza mbele acheze kama winga wa kulia kwani hata alivyokuwa Simba mara kadhaa kocha wake Jackson Mayanja, alimjaribisha nafasi hiyo na kuonyesha uwezo mkubwa.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wataanza kucheza na Mo Bejaia ya nchini Algeria mwishoni mwa wiki ijayo ugenini, hali inayowafanya kukaa mguu sawa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ikizingatiwa kuwa wanacho kikosi kizuri msimu huu tofauti na misimu kadhaa iliyopita.

Licha ya kwamba Wanajangwani hao wanakabiliwa na uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya mwishoni mwa wiki hii hilo haliwaumizi kichwa na badala yake akili zao zote wamezipeleka kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Katika michuano hiyo Yanga wapo Kundi A sambamba na Waarabu hao wa MO Bejaia ya Algeria, Medeama ya Ghana pamoja na waliokuwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, TP Mazembe ya Congo anayochezea Mtanzania, Thomas Ulimwengu.

Licha ya kwamba Yanga wamepangwa na Mazembe wenye historia nzuri kwenye michuano ya kimataifa, mashabiki wa Wanajangwani hao wanaamini kuwa kikosi chao ni bora sana na kwamba hakuna wa kuuzuia muziki wao.

Katika mazoezi ya jana ambayo Pluijm mwenyewe anatarajiwa kuyaongoza kuna mbinu mbalimbali ambazo atawafundisha ili kukabiliana na timu hizo walizonazo na kuvuka kizingiti kutinga hatua inayofuata.

Moja ya mambo anayotarajiwa kuyafanya ni kuisuka kisawasawa safu yake ya ulinzi ambayo imeongezeka baada ya kusajiliwa kwa Kessy, namna ya kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani pamoja pia na kuifundisha safu yake ya kiungo namna ya kupiga pasi za uhakika kusaidia mashambulizi na namna ya kuwasaidia mabeki kuzuia.

Katika safu ya ushambuliaji, Pluijm atahakikisha anawanoa vijana wake wakiongozwa na Ngoma pamoja na Amissi Tambwe, namna ya kutumia vizuri nafasi watakazozipata kwani michuano hii anayepoteza nafasi anampa adui yake mwanya wa kumdhuru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here