Home Michezo Kimataifa WANAWINDWA ZAIDI DIRISHA DOGO

WANAWINDWA ZAIDI DIRISHA DOGO

822
0
SHARE

LONDON, England

DIRISHA dogo la usajili barani Ulaya linatarajiwa kufunguliwa Januari, mwakani na kuna timu ambazo zitafanya usajili mkubwa tu, tusubiri kwa wiki hizi chache zilizobaki.

Klabu ya Manchester United inatagemewa kuuza takribani wachezaji wake 10 wa kikosi cha kwanza, ingawa mchezaji wa kwanza anayetabiriwa kudondoka mapema ni Bastian Schweinsteiger.

Wakati United ikionekana kuwa ni timu itakayofanya sana biashara ya kusajili na kuuza Januari hii, zipo klabu nyinginezo Ulaya ambazo hazitakuwa nyuma kuangaza macho yao sokoni na wachezaji hawa 10 huenda wakatua kwenye klabu mpya hivi karibuni.

Virgil van Dijk

Bila shaka, Mholanzi huyu anayekipiga katika klabu ya Southampton ana kiwango bora zaidi msimu huu wa Ligi Kuu England, jambo linalowapa tabu mabosi wa klabu yake wakati dirisha dogo la usajili likikaribia kufunguliwa.

Mojawapo kati ya timu hizi huenda zikanasa saini yake Januari: Liverpool na Everton. Na ada ya pauni milioni 30 au 40 huenda zikatosha kunasa kitasa.

Victor Lindelof

Msweden huyo anayekipiga katika klabu ya Benfica ya Ureno, mwenye uwezo wa kucheza kama beki wa kati na kulia, huenda akatua katika moja ya klabu hizi, Man United au Chelsea.

Nahodha wake wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic, aliwahi kukiri kuwa uwezo wa Lindelof anafaa kuichezea United, huku wakala wake, Hakan Cetinkaya, akizungumzia suala la uhamisho wake kila kukicha.

“Japokuwa dirisha la usajili halijafunguliwa, Lindelof ameanza kufukuziwa sana. Nitapanga kuanzisha mazungumzo na baadhi ya timu kubwa Ulaya, kwani nafasi ya yeye kuondoka Benfica ipo na kama haipo, basi kiangazi atapatikana,” alisema Cetinkaya.

Adrien Silva

Leicester City iliwahi kupeleka ofa ya pauni milioni 21 kwa ajili ya kuinasa saini ya kiungo huyo wa kati anayekipiga Ligi Kuu Ureno katika timu ya Sporting Lisbon, Agosti mwaka huu, lakini haikufanikiwa kumpata.

Na sasa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England wanafikiria suala la kurudi tena mjini Lisbon kumnyakua Silva, ambaye anavutiwa pia na mpango huo.

Memphis Depay

Licha ya kushindwa kuonesha ufundi wake uliomwezesha asajiliwe kwa ada ya pauni milioni 26 kutoka PSV, winga wa Manchester United, Memphis Depay, hajakosa timu inayohitaji huduma yake na klabu ya Everton ipo tayari kuanza mazungumzo ya kumnasa Mholanzi huyo.

Kocha wa Everton, Ronald Koeman, anahisi kuwa ana uwezo wa kukiamsha kiwango cha Depay kwa kumchukua kwa mkopo na kumsajili jumla baadaye, United pia ipo tayari kumwachia.

Cesc Fabregas

Mhispania huyu hana namba katika kikosi cha kwanza cha Chelsea tangu Antonio Conte alipotua kukinoa kikosi hicho. Kinachofuatia? Ni kuhama tu.

West Ham na AC Milan ni klabu mbili zinazotajwa kumtamani kiungo huyo, lakini changamoto iliyopo mshahara mkubwa atakaoutaka.

Hata hivyo, mojawapo ya timu hizo ingependa kumchukua kwa mkopo ili mshahara uweze kulipwa na pande mbili, na kwa sababu Fabregas anapenda kubaki jiji la London, uhamisho wa kwenda West Ham ndio unaopewa asilimia nyingi.

Kasper Dolberg

Ndio kwanza ana umri wa miaka 19 na tayari ameifungia Ajax Amsterdam mabao 11 ndani ya mechi 22 msimu huu.

Everton pia inafukuzia saini ya kinda huyu kuelekea Januari, wakati huo huo Man City na Man United zikipigana vikumbo kumsajili mshambuliaji huyo anayefanya vizuri kikosi cha kwanza cha Ajax.

Moussa Dembele

Mashabiki wa klabu ya Celtic inayommiliki mshambuliaji huyo, wanaweza kuwa na bahati mbaya, kwani wanaifaidi huduma ya mpachika mabao huyo kwa muda mfupi tu baada ya kuanza kuhusishwa na uhamisho wa hivi karibuni.

Dembele alitua Celtic kwa uhamisho wa bure Julai, mwaka huu na hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 17 ndani ya mechi 22, yakiwemo mabao mawili dhidi ya Man City, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki chache zilizopita.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, tayari ameshatuma maskauti wake kumfuatilia fowadi huyo, huku Tottenham pia ikiangaza macho yake na wanategemewa kutoa upinzani kwa Liver.

Moussa Sissoko

Kiungo huyu wa klabu ya Tottenham Hotspurs anatabiriwa kutua kati ya Inter Milan au Juventus mara baada ya kushindwa kupata namba ya kudumu tangu asajiliwe kutoka Newcastle.

Mfaransa huyo anaonekana kuwa alitua Spurs kimakosa, kwani ameshindwa kuingia jumla kwenye mipango ya kocha wake, Mauricio Pochettino na Inter au Juve mojawapo kati ya timu hizo inaweza kumsajili Januari kulingana na thamani yake sokoni.

Bastian Schweinsteiger

Utaamini kama Schweinsteiger ni mmoja wa wachezaji wanaokamata mshahara mnono pale United, licha ya kutopata nafasi ya kucheza? Sasa United haitaweza kuendelea naye msimu ujao ambapo dili la kuondoka Januari linatajwa mno.

Aidha, yeye mwenyewe alisema kwamba, hataichezea timu ya Ulaya na angependa kwenda Ligi Kuu ya China au Marekani.

Mamadou Sakho

Kinachomfanya kitasa huyu wa Liverpool asicheze chini ya Klopp msimu huu ni tabia yake ambayo haikumfurahisha kocha wake huyo walipokuwa Marekani kwenye ziara ya mechi za kujipima ubavu.

Sakho alitua Liver miaka mitatu iliyopita kwa dau la pauni milioni 18, lakini huenda akauzwa kwa nusu ya gharama hiyo ifikapo Januari, licha ya yeye mwenyewe kusema atapigania nafasi yake.

West Brom, Inter na AC Milan ni klabu zinazomnyemelea beki huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here