SHARE

*Mourinho aionya Arsenal, adai mwisho wao umefika

*Emery atamba kuvunja rekodi mbili Old Trafford

MANCHESTER, England

HAKUNA kulala! Habari ndio hiyo, licha ya Arsenal kuwa kwenye kiwango cha hatari ikiwa wamecheza michezo 11 mfululizo ya Ligi Kuu England hivi karibuni bila kupoteza mchezo wowote, mashabiki wao bado wanakosa imani na kikosi chao dhidi ya Manchester United mbovu.

Mashabiki hao wa Arsenal huamini kuwa Manchester United ni moja ya timu ambazo huwa ngumu kwao na hushindwa kupata matokeo hasa wanapokuwa Uwanja wa Old Trafford.

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, anaamini kikosi chake kipo tayari kupambana na Arsenal ya Unai Emery ambayo kama ni gari basi breki zake zimekatika.

Hata hivyo, Emery ametamba kuvunja mwiko ndani ya Uwanja wa Old Trafford ambao mara ya mwisho Arsenal walishinda bao 1-0 lililofungwa na straika matata, Emmanuel Adebayor, Septemba 17, 2006.

Huku kocha huyo raia wa Hispania akiamini kuwa huu ni wakati wake wa kuvunja rekodi dhidi ya Mourinho, wamekutana katika michezo mitano lakini Emery amefungwa minne na kutoa sare mmoja tu.

“Hivi sasa tunaitazama Arsenal kivingine kabisa, wana timu nzuri na kocha mzuri, lakini sisi ni Manchester United tupo tayari kupambana mpaka mwisho,” alisema Mourinho.

Manchester United watawakosa baadhi ya wachezaji wao ambao wana majeraha huku Ashley Young akitumikia adhabu ya kadi za njano.

“Mourinho ni kocha bora, makocha wanaochipukia hujifunza mengi kutoka kwake hata mimi, Arsenal tunataka kuandika historia kwa kushinda Old Trafford, naamini hii ni nafasi yetu,” alisema Emery.

Nao Arsenal bado Mesut Ozil hatihati kuukosa mchezo huo kwa majeraha kama alivyoshindwa kujumuishwa kikosini kwenye mchezo uliopita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here