SHARE

NA NIHZRATH NTANI

Ufukweni: Ni pembezoni mwa ufukwe maarufu wa Botafogo. Ufukwe uliopo Pwani ya bahari ya Atlantic, ndani ya jiji la Rio De Janeiro nchini Brazil. Nyuma ya ufukwe huu, macho yako yanakutana na milima miwili yenye kuvutia ya ‘Sugarloaf ‘na ‘Moro de Urca’ na kuleta taswira nzuri mahala hapo.

Wavulana wadogo wanacheza soka la ufukweni jioni hii. Kila mmoja, amejipa majina ya mashujaa wao. Mmoja anajiita Ronaldo, mwingine anajiita Rivaldo, majina mengine kama Romario, Gaucho, Dida yanasikika.

Juan Pereira, kijana miongoni mwao yeye anasema anataka kuwa kama Roberto Carlos siku moja. Hakuna anayemshangaa.

Ni maneno ya kawaida kuyasikia kutoka kwa watoto wengi wa kibrazili kuwa na ndoto ya kufuata nyayo za mashujaa wao katika soka . Kwanini kijana huyu ana ndoto ya kuwa kama Roberto Carlos?

UPANDE FURAHA, UPANDE MAJONZI KWA WAKATI MMOJA

Asubuhi ya saa nne na dakika 10. Ni Jumanne ya April 10,1973. Dunia ilikuwa inazizima kwa majonzi, baada ya kufahamika kuwa ndege aina ya Vickers Vangurad 952 iliyokuwa ikitokea katika mji wa Bristol Lulsgate nchini Uingereza na kuelekea katika mji wa Basel -Uswisi, kuanguka kusini mwa misitu ya Herrenmatt- hamlet katika mji wa Hochwald nchini Uswisi zikiwa maili chache kufika Basel.

Ndege hii iliyobeba watu 145. Ni watu 37 pekee ndio walioripotiwa kusalimika huku watu 108 wakipoteza maisha papo hapo.

Wengi wa abiria hao walikuwa wanawake kutoka Uingereza. Ajali hiyo inabakia kuwa moja ya ajali mbaya zaidi ya ndege iliyowahi kutokea katika ardhi ya nchi ya Uswisi.

Ni Jumanne hiyo hiyo ya April 10, 1973. Masaa machache baada ya kuanguka kwa ndege hiyo. Familia ya Oscar Da Silva na mkewe Vela Lucia da Silva iliyoko katika mji wa ‘Garca’ kusini mashariki mwa jimbo la Sao Paulo.

Asubuhi hiyo, familia hii fukara. Iliyokuwa ikifanya kazi ya vibarua katika mashamba ya kahawa yaliyoko katika mji huo wa Garca.

Ilikuwa imebahatika kupata mtoto wa kiume. Furaha ilikuwa imechukua nafasi kubwa kuliko majonzi ya kuanguka kwa ndege hiyo.

Mtoto huyu wa kiume walimpa jina la Roberto Carlos. Maisha ya Roberto Carlos yalijaa shida nyingi enzi ya utoto wake. Alipofikisha miaka 12. Roberto alikuwa tayari akiwajibika kufanya kazi katika kiwanda cha Torsao Cardeiro ili kuwasaidia wazazi wake.

Kila anapopata muda basi Roberto angejumuika na watoto wenzie mitaani ama ufukweni kucheza soka kama ilivyo ada ya watoto wengi wa kimaskini nchini Brazil.

Mama yake hakupenda Roberto kucheza soka, akihofia kuvunjika. Siku moja Roberto alimwambia mama yake:

‘”Iko siku wazazi wangu hawatafanya tena vibarua, kazi hii itabakia kama kumbukumbu ya kihistoria, tafadhali, niruhusu nicheze soka” Alisema Roberto.

NDOTO ILIYOTIMIA

Katika dimba la uwanja wa Santiago Bernabeu. Jose Antonio Camacho anabakia kuwa beki bora wa kushoto wa kihispania ndani ya Real Madrid.

Lakini linapokuja swali ni nani beki bora zaidi katika historia ya soka ndani ya Real Madrid? Hapana si Marcelo. Jina la Roberto Carlos lingekujia kwa haraka zaidi akilini mwako.

Roberto Carlos amepitia vilabu vya Union Sao Joao, Atletico Mineiro, Palmeiras, Inter Milan, Real Madrid, Fenerbahce, Corinthians kisha akamalizia soka lake kunako klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi.

Mnamo Agosti 1,2012 . Roberto Carlos alikuwa anatangaza kustaafu soka akiwa na miaka 39. Miaka 20 ya kucheza soka ilikuwa inafikia tamati siku hiyo.

Hata hivyo, tayari alikuwa ametimiza ndoto yake ya kuifanya familia yake kuwa tajiri. Akiwa na utajiri wa dola milion 40 hivi sasa. Soka lilimpa utajiri Roberto.

Miguu yake ilizungumza kile alichoazimia. Maisha yake ya utotoni yanabakia kuwa historia yenye kushangaza.

ATAKUMBUKWA USIKU ULE

Goli lake la adhabu dhidi ya Ufaransa. Linabakia kuwa goli bora kabisa kuwahi kufungwa kwa “free kick” katika historia ya soka Duniani.

Usiku wa Desemba 6, 2003 katika dimba la Nou Camp. Goli lake liliisaidia Real Madrid kuvunja historia ya kutopata ushindi katika El Clasico uwanjani hapo. Ni baada ya kupita miaka 20 bila ya Real Madrid kupata ushindi dhidi ya Barcelona hapo Nou Camp.

Roberto Carlos atakumbukwa zaidi katika usiku wa Mei 15,2002. Katika fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Bayer Leverkusen ndani ya dimba la Hampden Park huko Glasgow-Scotland.

Ni pale alipotoa pasi maridadi kutoka pembezoni mwa uwanja na mpira ule bila kutulizwa ulienda kutua kwenye guu la kushoto la Zinedine Zidane na kwa kasi ile ile aliupeleka mpira ule nyavuni mwa Bayer Leverkusen.

Goli hilo linatajwa kuwa ni goli bora zaidi kuwahi kufungwa katika michuano ya Uefa. Lilikuwa goli la pili na la ushindi baada ya lile la Raul Gonzalez kusawazishwa na Lucio.

ALIKUWA BEKI BORA WA KUSHOTO ALIYEPATA KUTOKEA

Denis Irwin alikuwa beki mahiri sana wa kushoto nyakati zake. Alitumia miaka mingi akiwa ndani ya jezi ya Manchester United.

Bexente Lizarazu tunaweza mtaja kuwa mmoja ya mabeki bora wa kizazi chake. Hata, Nilton Santos aliyepata kucheza soka Brazil anatajwa kuwa mahiri enzi zao.

Lakini mpaka sasa upo mjadala ni nani beki bora zaidi wa kushoto katika historia ya soka Duniani? Yapo majina mawili tu yenye kuleta mjadala huu kati ya Roberto Carlos na Paolo Maldini.

Wote wawili wametwaa kila taji ngazi ya klabu na timu ya Taifa. Mabeki wawili wa kushoto bora kabisa niliyepata kuwashuhudia. Ni swali gumu sana kupata jibu sahihi.

Hata hivyo, Roberto Carlos anabakia kuwa beki wa kipekee. Alikuwa na stamina ya aina yake, kasi, akili, uwezo wa kukaba na kushambulia kwa pamoja. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga krosi. Uwezo wake wa kupiga mashuti makali makali hata nje ya 18. Unamfanya Roberto Carlos kuwa beki wa wa aina yake.

Bado Roberto Carlos anahesabika kama mmoja wa wachezaji mahiri zaidi wa kupiga faulo katika historia ya soka Duniani.Huku pia akifunga zaidi ya magoli 80 kwa maisha yake ya soka yakiwemo ya faulo.

UBAGUZI WA RANGI HAUKUMUACHA SALAMA

Juni 19, 2007. Maelfu ya mashabiki walikuwa wamejazana huku wakiwa hawaamini macho yao katika dimba la ‘Sukru Saracoglu’ nchini Uturuki.

Mashabiki hao walikuwa wakimtazama Roberto Carlos akitambulishwa kuwa mchezaji wa Fenerbahce. Mchezaji aliyepata kuwa mahiri zaidi alikuwa klabuni kwao na atakuwa mchezaji wao akiwa ukingoni mwa soka lake. Furaha ilioje!!

Misimu miwili ya Roberto Carlos katika soka la Uturuki ilijaa dhihaka na huzuni mwingi. Mashabiki wa timu pinzani hawakuacha kumdhihaki kwa kumtupia ndizi. Wakimdhihaki kutokana na rangi yake na kumfananisha na nyani.

Mara mbili alifananishwa na nyani lakini yeye aliwajibu kwa kuchukua ndizi hizo na kula hapo hapo uwanjani.

ALITUMIA NUSU YA MAISHA YAKE REAL MADRID

Mnamo mwaka 1995. Roberto Carlos alitua barani Ulaya katika klabu ya Inter Milan alipokaa msimu mmoja tu. Ni baada ya kukorofishana na kocha wa Inter Milan wakati huo muingereza Roy Hodgson.

Kocha huyo alikuwa anataka kumuona Roberto Carlos akicheza nafasi ya winga na sio beki lakini Carlos alipendelea zaidi kucheza nafasi ya beki wa kushoto.

Aliondoka na kuelekea Real Madrid. Ni mahala hapo alipodumu miaka 11 akiwa ndani ya kikosi cha kwanza na kutengeneza ufalme wake. Akiwa Real Madrid aliisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mengi yakiwemo mataji manne ya La Liga na mataji matatu ya Uefa.

Akicheza jumla ya mechi 584 kwa mashindano yote na kufunga magoli 71. Huku pia akishikiria rekodi ya mchezaji wa kigeni aliyecheza mechi nyingi za La Liga akiwa amecheza jumla ya mechi 370.

Roberto Carlos anabakia kuwa mchezaji pekee wa nafasi ya beki wa kushoto kushika nafasi ya pili katika tuzo za Ballon D’or mwaka 2002 na tuzo ya mwanasoka bora wa FIFA mwaka 1997. Mara zote rafiki yake Ronaldo De Lima aliibuka mshindi dhidi yake.

Roberto Carlos anabakia kuwa beki mahiri na maarufu zaidi wa kushoto aliyepata kutokea katika historia ya soka Duniani.

Hapana shaka, wapo wanaomtaja kuwa alikuwa bora zaidi kuliko Paolo Maldini. Hata hivyo, miongoni mwetu tunajivunia kumuona Roberto Carlos akiwa bora katika nyakati zake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here