SHARE

NA JESCA NANGAWE,

JESHI la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa kina dhidi ya wasanii, askari na watu wengine wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Tayari jeshi hilo linawashikilia baadhi ya wasanii, askari na watu wengine wanaotuhumiwa kushiriki biashara hiyo haramu.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, tayari amewasimamisha askari wake 12 waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa wamo kwenye mtandao wa dawa za kulevya.

Alisema operesheni hiyo ni endelevu na haitamwacha mtu yeyote anayejihusisha na biashara hiyo na kufafanua kuwa uchuguzi dhidi ya askari na watu wengine waliotajwa unaendelea na mara ushahidi dhidi yao utakapokamilika watawapandisha kizimbani wakati wowote kuanzia sasa.

Miongoni mwa wasanii wanaoshikiliwa na jeshi hilo kufuatia operesheni iliyofanywa na Makonda yumo mshindi wa taji la Miss Tanzania mwaka (2006), Wema Sepetu, Dogo Hamidu, Khalid Mohamed (TID) na mtangazaji maarufu wa Clouds TV, Babuu wa Kitaa ambao juzi walifika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kwa mahojiano maalumu.

Kwa upande wake Kamanda wa Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema bado wanaendelea kuwashikilia watuhumiwa hao kwa mahojiano zaidi.

Wasanii wengine waliotajwa na Mkuu wa Mkoa, Makonda ambao wanatakiwa kufika kituoni kesho Jumatatu ni Vanessa Mdee, Tunda na watu wengine, Halidali Kavila, Amani, Kashozi na Omary Sanga.

Katika hatua nyingine nyota wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul Diamond Platinum jana alijikuta akizushiwa na mitandao ya kijamii kuwa yu miongoni mwa watu wanaotuhumiwa na biashara ya dawa za kulevya ingawa Kamanda Sirro alipoulizwa alikana msanii huyo kusakwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here