SHARE

LONDON, England

KWA maana ya heshima, hakuna kombe linalothaminiwa zaidi barani Ulaya kama Ligi ya Mabingwa. Na thamani yake inatokana na ushiriki wa wachezaji wakubwa zaidi duniani katika kupigania taji hilo, kila mchezaji bora ana ndoto za kutwaa Ligi ya Mabingwa.
Msimu huu, vumbi la michuano hii limeanza kutimka jana na hapa tumekuandalia kikosi cha wachezaji 11 waliocheza mechi nyingi zaidi kuanzia mwaka 1992.

Kipa: Iker Casillas (mechi 156)

Kipa huyu kutoka Hispania anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi UEFA kuliko mchezaji yeyote yule. Casillas ametwaa mataji matatu ya UEFA akiwa na Real Madrid – mwaka 2000, 2002 na 2014 akiwa nahodha. Baada ya kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza, Casillas aliihama Madrid na kujiunga na Porto ya Ureno mwaka 2015.

Mabeki: Gary Neville (Mechi 109)
Neville amemaliza maisha yake ya soka akiwa na Manchester United. Beki huyu wa kulia alikuwa kwenye kikosi cha United kilichotwaa mataji matatu mwaka 1999, baada ya kuaminiwa na Kocha Sir Alex Ferguson wakati akitengeneza kizazi cha vijana ‘Class of 92’.
Mbali na mataji haya matatu, Neville alibeba tena UEFA mwaka 2008, wakati United walipoichapa Chelsea kwa penalti, mechi ikipigwa katika jiji la Moscow, Urusi.
Hata hivyo, Neville hakupangwa katika pambano hilo ambalo Ryan Giggs na Rio Ferdinand walibeba taji kwa pamoja baada ya ushindi.

Paolo Maldini (Mechi 109)

Miongoni mwa mabeki bora zaidi duniani.

Kipindi akiwa AC Milan, Maldini alibeba mataji matano ya UEFA na anashika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wachezaji wakongwe waliofunga bao kwenye michuano hiyo, akifunga kwenye pambano dhidi ya Liverpool mwaka 2005. Hapa alikuwa na miaka 36 na siku 333.

Muitaliano huyu alicheza pambano lake la kwanza mwaka 1985 na amecheza kwa zaidi ya miaka 20 kabla ya kutundika daluga mwaka 2009. Klabu ya AC Milan iliamua kustaafisha jezi namba 3 kama ishara ya kumuenzi nahodha wao.

Carles Puyol (Mechi 115)

Ukizungumzia uimara wa Barcelona huwezi kuacha kutaja jina la beki huyu kisiki wa Kihispania, Carles Puyol. Amedumu na Barca kwa zaidi ya miaka 15 tangu alipoibuliwa kutoka kikosi cha watoto na alipewa unahodha rasmi mwaka 2004. Puyol aliiongoza Barca kutwaa mataji matatu ya UEFA mwaka 2006, 2009 na 2011.

Roberto Carlos (Mechi 120)
Binadamu anayekumbukwa kwa mikwaju yake mikali kutoka kwenye guu lake la kushoto. Roberto Carlos amecheza mechi 120 za UEFA akiwa na Madrid na miongoni mwa nyota waliotamba katika kizazi cha ‘Galacticos’.
Mbrazil huyu mwenye sifa ya kukaba na kushambulia alitwaa mataji matatu ya UEFA akiwa na Madrid, kabla ya kuihama klabu hiyo na kutimkia Fenerbahce mwaka 2007.

Viungo: Cristiano Ronaldo (Mechi 127)
Kwenye mchezo wake wa 127, mshindi huyu mara tatu wa Ballon d’Or aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa michuano hii kwa kufunga bao lake la 94. Staa huyu wa Real Madrid pia anashilia rekodi ya kufunga mabao mengi kwa msimu, akifunga mabao 17 msimu wa 2013-14.
Pia yuko kwenye vinara waliofunga hat-tricks nyingi kwenye michuano hiyo akilingana na staa wa Barcelona, waliofunga ‘hat tricks’ tano kila mmoja.
Baada ya kucheza michezo 52 ya UEFA akiwa na Manchester United, Ronaldo alihamia Real Madrid mwaka 2009 na amebeba mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa.

Xavi (Mechi 151)

Kiungo huyu wa Kihispania amekuwa moyo wa mafanikio ya FC Barcelona katika michuano ya Ligi ya Mabingwa. Xavi aliibuliwa katika kituo cha La Masia, kinacholea vijana wa Barcelona. Alicheza mchezo wake wa mwisho akiwa Barcelona na kutwaa taji kwa ushindi wa bao 3-1 dhidi ya Juventus mwaka 2015.

Clarence Seedorf (Mechi 125)

Fundi wa mpira, Seedorf anabaki kuwa kiungo bora zaidi kuwahi kutokea barani Ulaya katika kipindi cha miaka ya 1990 mpaka mwanzoni mwa 2000. Mholanzi huyu ametwaa mataji manne ya UEFA akiwa na klabu tatu tofauti, Ajax, Real Madrid na AC Milan. Seedorf anasifika kwa pasi zake murua na asisti kali akiwa katikati ya uwanja na anakumbukwa kwa bao la mapema alilofunga mwaka 1995 dhidi ya Schalke kwenye sekunde ya 21.06.

Ryan Giggs (Mechi 141)

Akiwa Manchester United, Giggs anabaki kuwa mchezaji mbunifu zaidi kuwahi kutokea katika soka la Kiingereza.
Raia huyu wa Wales ametwaa mataji mawili ya UEFA, mwaka 1999 na 2008 katika miaka 23 aliyokaa Old Trafford.
Ni miongoni mwa vijana walioibuliwa kwenye ‘Class of 92’ kama Neville na anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa pili aliyefunga bao akiwa na umri mkubwa, alifunga akiwa na miaka 37 na siku 290 kwenye pambano dhidi ya Benfica mwaka 2011.

Straika: Raul (Mechi 142)

Gwiji mwingine wa soka barani Ulaya ni Raul Gonzalez.
Aliiongoza Real Madrid kwa miaka 16 tangu alipopandishwa kutoka kwenye akademi ya vijana wa klabu hiyo. Anashika namba tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa UEFA nyuma ya Ronaldo na Messi, akifunga jumla ya mabao 71.

Alijiunga na Schalke ya Ujerumani mwaka 2012 alipocheza mchezo wake wa mwisho wa michuano hii. Raul ametwaa mataji matatu ya UEFA akiwa na Real, mwaka 1998, 2000 na 2002.

Zlatan Ibrahimovic (Mechi 123)

Jembe la Ulaya. Staa huyu kutoka Sweden amecheza mechi 123 katika michuano hii akiwa na klabu 6 tofauti tofauti kwenye kipindi cha miaka 15.
Amefunga mabao 49 na ni namba sita kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwenye michuano hii.
Katika kipindi hicho chote alichocheza akiwa na Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, AC Milan, Paris Saint-Germain na sasa Manchester United, Zlatan hajawahi kubeba Ligi ya Mabingwa.

Kocha: Sir Alex Ferguson (Mechi 190)
Ni nani mwingine unadhani angestahili kukiongoza kikosi bora kama hiki zaidi ya Sir lex Ferguson?Ferguson ametwaa mataji mawili ya UEFA katika kipindi cha miaka 26 akiwa na kikosi cha Manchester United.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here