SHARE

NA MWAMVITA MTANDA

UNAMKUMBUKA yule winga wa Yanga, Simon Msuva, jinsi alivyokuwa akiwasumbua mabeki hapa nchini? Basi habari njema ni kwamba jembe lingine la aina hiyo linatarajia kutua kwa Wanajangwani hao.

Unaambiwa uwezo wake dimbani na kasi yake ya kutumia miguu yake huenda ikawalazimu wachezaji wenye majina pale Yanga kusubiri kwanza na yeye kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza.

Huyo si mwingine bali ni dogo aitwae, Samuel Filipe ‘Champion’, ambaye ni raia wa DRC mwenye umri wa miaka 19 tu.

Habari ambazo DIMBA Jumatano limezipata na kuthibitishwa na winga huyo zinaaminisha kwamba, tayari mipango ya kuichezea klabu hiyo kongwe nchini imekaa vizuri, kilichobaki ni yeye kutua utakapowadia usajili wa dirisha dogo.

Licha ya umri wake mdogo, lakini balaa lake la msimu uliyopita katika Ligi Kuu ya Rwanda lilikuwa kubwa kipindi hicho akikitumikia kikosi cha Mukura ambapo alionyesha uwezo mkubwa na kuacha jina nchini humo.

Winga huyo pia alifanya vizuri alipokuwa akiichezea timu za taifa za vijana katika umri tofauti; U-17 na baadaye U-20.

Akizungumza  na DIMBA Jumatano  jana kutoka DR Congo,  nyota huyo alisema kuna uwezekano mkubwa wa kutua Jangwani dirisha dogo litakapofunguliwa mwezi Novemba mwaka mwaka huu, kwani amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na moja wa kiongozi wa juu katika klabu ya Yanga.

“Nilikuwa nawasiliana na tajiri mmoja wa Yanga ambaye alinipigia simu na sikufahamu nani amempatia namba yangu, kama wazazi wangeniruhusu sasa hivi ningekuwa Tanzania naitumikia Yanga.

“Lakini kwasasa naweza kusema nipo huru nimeshazungumza nao vizuri, jambo ambalo wanapaswa kuamini, hii ni kazi yangu, wanatakiwa kuniombea dua ili nifanikiwe zaidi,” alisema Champion.

Winga huyo amesisitiza kuwa ana mapenzi makubwa na Yanga na kwamba amekuwa akiifuatilia tangu aliposikia kuwa inanolewa na kocha msaidizi wa timu ya taifa ya DRC, Mwinyi Zahera.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here