SHARE

MANCHESTER, England

SI umesikia namna mashabiki wa soka wanavyomponda Paul Pogba baada ya kiwango kibovu alichokionyesha kwenye pambano la ‘Manchester derby’?

Sasa baada ya kelele hizo kuzidi, Zlatan Ibrahimovic ameibuka na kuwajibu wote wanaomponda Pogba kwa kusema kuwa muda si mrefu wataona aibu.

Pogba, aliyesajiliwa na United msimu huu akivunja rekodi ya usajili duniani kwa kitita cha pauni mil 86, alicheza chini ya kiwango wakati mashetani wekundu wa Old Trafford wakichezeshwa kichapo cha bao 2-1 na mahasimu wao wa jiji, Manchester City.

Baada ya pambano hilo, mashabiki wengi walimshukia Pogba kwa madai kuwa kiwango chake hakiendani na thamani ya pesa iliyolipwa na United kumsajili kutoka Juventus ya Italia.

Lakini Ibrahimovic, raia wa Sweden, amesema kuwa wengi wanaomponda Pogba ni watu wenye chuki juu ya kiwango cha usajili wake na anaamini muda si mrefu kiungo huyu wa Kifaransa atawafunga midomo.

“Wote wenye wivu wanaongea vibaya kuhusu Pogba, ninaamini watafunga midomo yao kwa aibu,” alisema Ibrahimovic, alipohojiwa na kituo cha SFR Sport.

“Ataimarika muda si mrefu na atawazodoa wapinzani wake.

“Ukaribu wangu na Pogba ni rahisi sana: Nazungumza na ananijibu. Paul ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana,” ameongeza nyota huyo.

Licha ya kuvunja rekodi ya dunia, Ibrahimovic anaamini Pogba anatakiwa kupewa muda ili aweze kuimarika na kuendana na falsafa za Kocha Jose Mourinho.

“Kwa sasa watu wanatakiwa kuzungumza ukweli halisi ulivyo, wanamshutumu Paul na yote ni kutokana na kiwango cha pesa kilichotumika kwenye usajili wake,” alisema Zlatan.

“Sikuwa nikimfahamu Paul kabla, lakini sasa naweza kumzungumzia kidogo. Anafanya mazoezi kwa bidii na ana tamaa ya kuzidi kufanikiwa, lakini mbali na yote, tunatakiwa kufahamu kuwa bado ni kijana mdogo, anahitaji muda.”

Kikosi cha vijana wa Jose Mourinho kinatarajiwa kushuka dimbani kesho kwenye mchezo wa Kombe la Uropa dhidi ya Feyenoord na wana imani watautumia mchezo huo kufuta machozi ya kipigo walichokipata kwenye ‘Manchester derby’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here