SHARE

NA JUMA KASESA


 

JUMAPILI iliyopita katika simulizi hii sehemu ya 45, mwanamuziki gwiji wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango   ‘King Kiki’,   aliishia akisimulia alivyoanza zoezi la kuingia madukani jijini Paris, Ufaransa kusaka vyombo vya muziki lakini kwa bahati mbaya kote alikopita akakwaa kisiki kutokana na kushindwa kumudu bei.

Kiki akiwa na mwenyeji wake, Abigael ambaye ni raia wa Algeria, baada ya kukwama wanapanga safari nyingine kesho yake kutembelea maduka mengine jijini Paris kuangalia kama watafanikiwa kupata vyombo vya muziki vya kisasa lakini vyenye bei nafuu.

Sasa Endelea…

Siku yangu ya tatu nikiwa hotelini jijini Paris niliamka asubuhi na mapema kumsubiri mwenyeji wangu, Abigael kwa ajili ya kuendelea na zoezi letu la kutafuta vyombo vya muziki kulingana na kiasi cha     fedha nilichonacho.

Abigael alikuwa na ahadi za kizungu.    Muda wa saa tatu asubuhi tayari alikuwa ameshaegesha gari yake nje ya viunga vya hoteli ninayokaa na kunifuata eneo la mapokezi.

Alinikuta nami niko tayari kwa safari.   Hatukuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kuanza mwendo wa kuzurura maduka mbalimbali aliyohisi pengine yangekuwa na bei nafuu tofauti na kule tulikopita siku moja kabla.

Tukiwa njiani Abigael alinishtua kwa habari mpya aliyokuja nayo kwangu siku hiyo.     Aliniambia amejadiliana kwa kirefu na mkewe na kuona kuna umuhimu wa kunipunguzia gharama za maisha jijini Paris.    Niliendelea kumsikiliza ili nijue nini lilikuwa kusudio lao mke na mume. Aliniomba niridhie ombi lao kutaka kunitoa hotelini nihamie nyumbani kwao.

Hoja yao ilijikita kwamba bado sijajua lini ntapata vyombo na hivyo kuendelea kuishi hoteli ni gharama kubwa ambayo wao wanaweza kuniondolea kwakuwa nyumbani kwao wana nafasi ya mimi kulala.  Nilijipa dakika mbili za kuchekesha akili na kisha kumjibu Abigael nimeridhia ombi hilo lakini pia kumtolea shukrani kwa moyo wa upendo alionao yeye na mkewe.

Siku tatu za mimi kufahamiana naye zilikuwa zimeanza kuniaminisha jamaa ni mtu mwema.     Nikirejea siku ya kwanza alivyonipokea kwake baada ya kutoswa na yule Alphonce ambaye ndiye niliyemtarajia angekuwa mwenyeji wangu, lakini kwa ujinga akaamua kunitosa kwa kujifanya siyo yeye.  Eti nimepotea.

Kumbukumbu za mwenendo wa tabia ya Abigael tangu siku ya kwanza tulipojuana mimi na yeye zilitosha kunifanya niridhie ombi hilo bila pingamizi. Akili za kuambiwa changanya na za kwako, kwani hata mimi nilibaini ni kweli kuishi hoteli ulikuwa ni mzigo kwangu ingawa nilikuwa na pesa ya kutosha niliyopewa na mfadhili Alex Alex.

Tulitumia siku ya pili kuzunguka maduka mbalimbali ndani ya mitaa ya Jiji la Paris bila mafanikio ya kupata vyombo ninavyokusudia.     Nilianza kuishiwa nguvu.

Abigael alikuwa mwenye kunipa moyo kwamba nisikate tamaa na atahakikisha tunafanikisha kupata vyombo hata kwa kutoka kwenye miji nje ya Jiji la Paris.

 

Siku ilikwisha bila mafanikio ambapo alinirudisha hotelini huku yeye akirudi nyumbani kwake kwa ahadi angenifuata kunihamisha.  Aliniacha nimalizie siku yangu ya tatu hotelini kwakuwa nimeshailipia.    Alinifuata asubuhi na kunichukua kuelekea nyumbani kwake.    Kabla hatujafika kwake nilimuomba tupitie kwenye duka linalouza vyakula na bidhaa nyingine(Super Market) kwani kuna vitu  nataka ninunue.

Alinihoji nini nataka kununua lakini nilimwambia kuna vitu nataka nitazame kidogo kama kutakasa macho.    Bila kumwambia chochote tuliingia kwenye mtaa wenye maduka makubwa ya vyakula  na kisha kununua mchele, unga, sukari, mafuta sabuni na vitu vingine na kuvilipia kisha kuvipakia kwenye gari na kuelekea nyumbani kwake.

Abigael aliniuliza chakula hicho cha nini nami kumjibu nataka nimpelekee shemeji yangu yaani mkewe kwa ajili ya kutupikia.     Jitihada zake za kunitaka nisinunue kwani kwake amejitosheleza zilikwama.    Kilikuwa chakula cha kula wiki mbili.     Niliona si vyema nipewe hisani ya kulala na bado niwaumize wenyeji wangu na mambo ya chakula.

Nilianza maisha mapya nchini Ufaransa nikiwa naishi nyumbani kwa Abigael huku tukiendelea kutafuta vyombo kwenye maduka mbalimbali bila mafanikio.

Hatimaye nililazimika kufanya uamuzi mgumu wa kuondoka Paris na kuelekea nchini Ubelgiji ambako tulipata taarifa ndiko ambako vyombo vya muziki ni bei rahisi lakini pia vizuri.

Wiki mbili za uwepo wangu nchini Ufaransa zilitosha kuona zoezi la kupata vyombo limekwama hivyo ni lazima nielekeze jicho sehemu nyingine barani Ulaya ambako ningefanikisha azma yangu.     Niliagana na familia ya Abigael kwa upendo huku nikiwaachia huzuni kubwa kutokana na mazoea tuliyokuwa tumeanza kuyajenga ndani ya muda mfupi.

Nilikwea pipa hadi mjini Brussels, Ubelgiji na kufikia katika mji wenye kuishi watu mashuhuri PlusRoger na katika hoteli ya kitalii inaitwa Albert.

Je, Kiki alifanikiwa kutimiza ndoto za kupata vyombo nchini Ubelgiji?   Safari yake mjini Brussels ilikuaje?    Nini kiliendelea yeye na Nguza Vicking ‘Babu Seya’?         Usikose kusoma DIMBA siku ya Jumapili kuendelea kupata uhondo wa simulizi hii.. Kwa maoni na ushauri 0715-629298.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here