Home Makala YANGA HUIONI, TSHISHIMBI UNAMUONA

YANGA HUIONI, TSHISHIMBI UNAMUONA

7892
0
SHARE

NA ABDULAH MKEYENGE


NAPENDA kumtazama Mkongomani wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi. Napenda kumtazama mchezaji huyu, iwe mazoezini iwe kwenye mechi, natumia muda mwingi kumtazama. Huwa najifunza mengi kutoka kwake, ni mchezaji wa kipekee.

Yanga wanapitia kipindi kigumu hivi sasa. Njia wanayoipita Kiitaliano ingeweza kuitwa Vea Della Rosa (Njia ya Mateso), licha ya kupitia njia hii ya nje na ndani ya uwanja, lakini Tshishimbi bado yuko vilevile.

Hachoshi kumtazama kama wanavyochosha kuwatazama wachezaji wengine wa Yanga wanaocheza kana kwamba wanalazimishwa kucheza. Unapomtazama yeye anavyocheza, ni ngumu kujua timu yake ina matatizo.

Licha ya matatizo yote yaliyoko ndani ya timu, lakini hajawahi kugomea mazoezi, kumshawishi mchezaji mwingine naye agome. Wagome wote. Mkimya kama alivyo, yeye ni kazi, kazi na yeye.

Matatizo ya Yanga ameamua kuyaweka kando, badala yake anaitumikia jezi ya Yanga mpaka katika pumzi yake ya mwisho. Rafiki yangu Ibrahim Ajib aliwahi kuniambia kwamba, anavyocheza Tshishimbi katika mazoezi, ndivyo anavyocheza katika mechi. Hachuji ubora. Ndani ya uwanja anakupa vitu vingi kwa wakati mmoja.

Kundi kubwa la wachezaji wa Yanga limeshakata tamaa na maisha ya Yanga. Kundi hilo linacheza kutokana  na kwamba, linatakiwa kucheza lakini ndani ya mioyo yao wameshachoka kuitumikia Yanga. Kinachofanya wachezaji hawa wawe hivi ni ukata, hakuna kitu kingine.

Ukata umewakatisha tamaa. Yanga ya sasa imejaza kundi kubwa la wachezaji wa ndani. Asilimia kubwa ya wachezaji hawa wametumia muda wao mwingi kulalamikia hali ya timu nje na kuacha kufanya mazoezi.

Zaidi ya hapo wachezaji hao hutumia muda wao mwingine kujiremba nywele zao kwenye vioo na ukiwaleta uwanjani, wanakuacha kinywa wazi lakini Tshishimbi mwenye mwonekano wa kirembo kama wao uwanjani ni mwanamume wa shoka. Tena mwanamume kwelikweli!

Nimeitazama Yanga katika michezo miwili ya kimataifa dhidi ya Gor Mahia hivi karibuni. Nimeutazama ule mchezo wa Nairobi, nikautazama na mchezo wa Dar es Salaam, ni Tshishimbi aliyeonekana katika mechi zote mbili. Hakuna mchezaji wa Kitanzania aliyebadili kitu, wengi walicheza kwa kutimiza wajibu, lakini hawakucheza kwa kujitolea.

Yanga iko hoi taaban na inatia huruma. Lakini Tshishimbi amebaki kama alivyo. Anapiga zake mpira mwingi na kuinamisha chini shingo yake, sijawahi kumsikia akilalamika popote pale. Ameiacha miguu yake izungumze, lakini si kinywa kama rafiki zangu wengine.

Kuna kitu cha kujifunza kwa marafiki zangu. Ni kweli Yanga ina hali mbaya hivi sasa na kila mmoja analijua hili, lakini kususa kwao na kugomea mazoezi hakuwasaidii wao. Yanga ipo na itaendelea kuwepo.

Yuko wapi Sunday Manara aliyeitwa jina la utani Computer wakati computer zenyewe zilikuwa bado hazijafika nchini? Lakini Yanga imeendelea kuwepo miaka nenda rudi. Rafiki zangu wajitolee ili wapate sehemu nyingine yenye malisho mazuri. Mchezaji akigomea mazoezi au mechi, hasara si ya timu, hasara ni yake mwenyewe.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here