SHARE

NA WINFRIDA MTOI

KATIKA mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga tayari inaonekana kupoteza matumaini ya kutwaa taji hilo kutokana na kasi ya watani wao Simba.

Msimamo wa ligi hiyo ulivyo kwa sasa, Simba ndiyo inaongoza na pointi 71, ikicheza mechi 28, imeshinda 23, sare mbili na kupoteza tatu.

Nafasi ya pili ipo Azam FC na alama zake 54, mechi ilizocheza ni 28, imeshinda 16, sare sita sawa na ilizopoteza, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 51 ilizokusanya katika michezo 27, ikishinda 14, sare tisa, imepoteza nne.

Kulingana na pointi za timu hizo tatu ambazo mara nyingi ndizo zinapewa nafasi ya ubingwa, Yanga licha ya wadau wake kujipa matumaini kuwa inaweza kutoboa kimahesabu, lakini si kitu rahisi.

Je Yanga itawezaje kuchukua ubingwa mbele ya Simba waliwaacha kwa pointi 20 na idadi kubwa ya mabao, kwa nini isiwe Azam ambao wapo nafasi ya pili?

Kwa jinsi msimamo ulivyo, Yanga ni rahisi kuishusha Azam na kukaa nafasi ya pili kwa sababu bado hawajakutana nayo katika mechi ya mzunguko wa pili.

Imekuwa ni ngumu kuamini kama Yanga inaweza kuchuku ubingwa msimu huu, lakini  kwa  matokeo ya soka  lolote linaweza kutokea na  ndio sababu, inayoifanya Simba ishindwe kutangazwa mabingwa.

Yanga bado ina jeuri ya kuendelea kutamba mtaani kuwa inatachukua ubingwa kimahesabu ya mezani na pia kitendo cha kuifunga Simba, inaamini huenda watani wao hao wakakutana na changamoto za kupoteza pointi katika mechi 10 zilizobaki.

Yanga inatambia hapa

Pamoja na kusuasua katika michezo kadhaa, lakini Yanga ni timu ambayo haitabiriki kwa sasa, mfano mzuri ni mechi iliyocheza na Simba, hakuna aliyeamini kama itaibuka na ushindi.

Kuimarika kwa kikosi chake na wachezaji kujituma pale wanapoona mchezo huo ni lazima waondoke na pointi, ni kati ya silaha za Yanga zinazowapa jeuri kwa Yanga.

Hata michezo iliyopoteza baada ya kuifunga Simba, ilionekana wazi wachezaji  waliamua tu wenyewe kubweteka lakini walikuwa na uwezo wa kuchukua pointi hizo.

Kingine ambacho Yanga inajivunia na inaweza ikiwa chachu ya kuchukua pointi katika mechi zilizobaki, ni ahadi nono wanazoahidiwa wachezaji endapo watashinda mechi.

Hali hiyo inaweza kutokea katika mechi zilizobaki, kila mchezaji atajituma kuhakikisha pointi tatu zinapatikana katika kila mchezo kama walivyofanya kwa Simba.

Dirisha dogo lilivyoizindua usingizini 

Mwanzoni mwa msimu ni kama Yanga bado ilikuwa usingizini, lakini sasa imeamka na kutambua nini itatakiwa kufanya ili kuwapa furaha mashabiki wake.

Kitu pekee kilichofanikishwa na Wanajangwani hao kiasi cha kutamba na kuinyamazisha Simba, ni usajili uliofanywa katika kipindi cha dirisha dogo, pamoja na wadhamini kujitoa kwa dhati kuisaidia timu.

Uchezaji wa kikosi cha Yanga kwa sasa ambacho ndani yake kuna Bernard Morrison, Ditram Nchimbi na Haruna Niyonzima, kumeipa uhai safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Awali pamoja na Wanajangwani hao kufanya usajili mkubwa, walionekana  hawana tofauti na kikosi cha msimu uliopita kilichokuwa kinapita kilichokuwa finyu na kukabiliwa na ukata.

 Ilikuwa ni timu ambayo inatia shaka kwa wadau wake, pamoja na uwepo wa nyota wanaoitwa wa Kimataifa kama vile Sadney Urkhob, Juma Balinya, David Molinga na wengine lakini ilikuwa kazi bao kupatikana.

Yanga iliyopita ilikuwa kama kiamsha presha kwa mashabiki wake, wenyewe wanakuambia walikuwa wanakwenda uwanjani na panaldo za kumeza kupunguza maumivu ya kichwa.

Lakini kipindi hiki cha kina Morrison, kuna burudani nyingi zinapatikana katika kikosi hicho, ukiachana na ile ya kutembea na mpira, chenga za Niyonzima zimereje, pia amsha amsha ya Nchimbi   pale mbele za kuwalaza na viatu mabeki wa timu pinzani.

Mabadiliko ya benchi la ufundi

Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, mfumo wake umeibadilisha timu hiyo kwa kiasi kikubwa.

Licha ya kufika tayari usajili umeshafanyika, lakini anaendelea kupambana na timu inaonekana inacheza soka la kuvutia.

Eymael angekuwa ni kocha mwingine, tungekuwa tunasikia malalamiko tu kwa sasa kuwa anashindwa kupanga kikosi kwa sababu wachezaji hajawasajili yeye, lakini kinachoonekana ni wazi amekuja kuibadilisha Yanga.

Kama alivyosema mwenyewe kuwa lengo lake ni kuifanya timu hiyo ya Kimataifa na kucheza soka la kipekee Afrika, dalili zimeanza kuonekana ndani ya miezi miwili alikuwepo.

Eymael amefanikiwa kuwafanya wachezaji waliokuwa hawaonekani uwanjani kuwa lulu kwa sasa kama vile Juma Makapu na Jaffar Mohammed.

Kitu kingine alichokuja nacho kocha huyo, ni kuleta mwalimu wa viungo na mtaalamu wa tiba na viungo, hivyo kulifanya benchi hilo kusheni kila kitu. 

Hata vifaa vya kisasa wanavyotumia wachezaji kufanyia mazoezi, vimenunuliwa baada ya kocha huyo kufika na kuvihitaji kwa haraka.

Kauli ya uongozi

Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo,  Fredererick  Mwakalebela, anaweka wazi kuwa bado hawajajitoa katika mbio za ubingwa, wataendelea kupambana hadi dakika za mwisho.

Alisema  tangu wameingia madarakani kuna mabadiliko makubwa katika kloabu hiyo na sasa wachezaji wanaishi maisha wanayotakiwa kuishi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here