Home Makala Yanga isiipime uwezo FIFA kwa uzembe

Yanga isiipime uwezo FIFA kwa uzembe

568
0
SHARE

KLABU ya Yanga imekuwa ni klabu pekee kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo haikuwasilisha usajili wake kwa wakati hadi dirisha linafungwa.

Mpaka sasa hapajawa na majibu ya kutosheleza kutoka kwa uongozi wa Yanga, hasa sekretarieti ambayo kimsingi ndiyo inayowajibika na kazi za kila siku katika klabu hiyo ambayo ina miaka 81 hivi sasa.

Jambo ambalo lilinishangaza na kunisikitisha ni Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, ambaye alizungumza kwenye kituo kimoja cha redio akisema kwamba hajui nini kilichotokea na wala hajui walikwama wapi hadi kushindwa kufikia hatua hiyo waliyonayo kwa sasa.

Nafikiri kwa fikra ndogo tu ambazo si za kukaa darasani, lakini swali lililopo kichwani kwangu ni kwamba, kama Baraka hajui, nani anayeweza kujua na kuwaambia Wanayanga nini kilichotokea.

Mimi ninavyofikiri ni jambo moja tu kwamba, sekretarieti ya Yanga imefanya uzembe ambao kiukweli hauwezi kuvumilika, kwani haiwezekani timu ambayo ipo jirani na Makao Makuu ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kushindwa kuwasilisha usajili wake kwa wakati.

Najiuliza ikiwa Yanga, klabu kubwa yenye watu wengi imekwama kuendana na ratiba, je, itakuwaje kwa Ndanda ya Mtwara, Toto Africans ya Mwanza au Mbao FC ambayo ni timu mpya kwenye ligi? Kiukweli kuna makosa ambayo kimsingi hayavumiliki kwa sababu si mara ya kwanza makosa kama haya kufanyika chini ya sekretarieti hii ambayo ipo chini ya Baraka.

Ieleweke wazi kuwa sina tatizo na mtu yeyote ndani ya Yanga, lakini shaka yangu ni kwa nini makosa haya yanajitokeza mara kwa mara, hivyo kupata shaka na uwezo wa baadhi ya watendaji, hasa nafasi ya Katibu Mkuu.

Ikumbukwe kwamba baada ya Yanga kupata nafasi ya kucheza hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka huu, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) liliitisha semina kwa ajili ya watendaji wa timu zote zinazoshiriki michuano hiyo ili kupewa mwelekeo wa namna mashindano yatakavyofanyika, hii ikiwa ni pamoja na kanuni mbalimbali, lakini kwa masikitiko makubwa Yanga haikuwa na mwakilishi, hivyo kuingia kwenye michuano hiyo kigiza giza tu.

Ukosefu wa uwakilishi ulikosesha Yanga kujua namna namba za jezi zitakavyochapishwa kwa maana viwango (Fifa standard) sambamba na majina ya wachezaji, kwani mambo yote hayo yapo kwenye vipimo maalumu vinavyokubalika kimataifa.
Hilo lilifanya Yanga kutumia jezi tofauti kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria.

Semina hiyo ilikuwa nyeti pengine kuliko ilivyokuwa inatazamwa na Yanga na wakati mwingine kukosa semina hiyo ilichangia kwa sehemu kubwa Yanga kutofanya vizuri kwenye baadhi ya mechi zake, kwani taratibu nyingi zilikuwa mpya kwao.
Hizi ni athari za moja kwa moja ambazo Yanga ilizipata kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kwa mwaka huu.

Kadhalika msimu wa usajili, TFF iliitisha semina kwa watendaji wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara juu ya elimu ya usajili wa kimtandao (TMS), lakini Yanga haikuwa na mwakilishi, jambo ambalo naamini limesababisha kushindwa kufanya usajili.

Sasa wakati mgumu umefika kwa timu, kwani kutokana na kushindwa kufanya usajili kwa wakati kulingana na ratiba ambayo imewekwa na TFF, Yanga inaweza kushushwa daraja, hivyo kukosekana kwenye ligi ijayo.

Inawezekana ikaonekana kuwa ni jambo lisilowezekana au kuonekana ni jambo la masihara, lakini ukweli ni kwamba linaweza kutokea jambo likaonekana ni maajabu.

Kwa sababu kama TFF ikiamua kukaa pembeni, ni dhahiri kwamba FIFA halitakuwa na mswalie mtume zaidi ya kuamuru Yanga kushushwa daraja au kulipa faini.

Najiuliza, kama ikitokea Yanga imeshuka daraja, nani atawajibika katika hili, pia nani atalipa gharama za usajili uliofanywa msimu uliopita?
Hii ina maana kwamba kama makosa yanafanyika mara zote hizo na klabu imeajiri watendaji kwa ajili ya kutekeleza mambo kwa maendeleo ya klabu, ni wazi kuwa kuna tatizo.

Kwa wale ambao walisahau, ipo klabu moja ya Italia inatwa Juventus ambayo ilishushwa daraja kwa kosa la kupanga matokeo katika ligi ya Italia. Yanga katika baadhi ya mambo ipo vizuri, hasa idara ya mawasiliano kwa umma chini ya Jerry Muro imefanya vyema, kwani kazi inaonekana ila huku kwenye utawala kwa ujumla wake kuna tatizo.

Nafikiri sasa ndipo wakati mwingine ninawakumbuka baadhi ya watu waliopita kwenye klabu hiyo miaka ya karibuni, kwa maana makatibu, akiwemo Mwesigwa Selestine, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa TFF pamoja na Dk. Jonas Tiboroha, ambao kwa sehemu kubwa waliweza kuimudu nafasi hiyo.

Ninachokiamini mimi ni kwamba nguvu kubwa ya Yanga iliyonayo, hasa ya watu katika kada mbalimbali ni jambo la kushangaza kuona eti inashindwa kufanya usajili wake.

Kama hili lilikuwa haliwezi kufanywa na watu waliopo Yanga lingeweza kufanywa na Wanayanga yeyote, tena bure kama klabu isingekuwa na fedha za kumlipa mtaalamu husika.

Ifikie sehemu taaluma zichukue nafasi yake, uhakika nilionao ni kwamba viatu vya ukatibu wa Yanga ambavyo amevivaa Baraka Deusdedit havijamtosha.

Kwa hiyo, yanayotokea hivi sasa ndani ya Yanga ni ishara ya kile ninachosema kwamba viatu vimekuwa vikubwa kuliko mvaaji.
Narudia tena, inawezekana ikaonekana ni jambo lisilowezekana, ila ukweli ni kwamba Yanga inategemea kudura za TFF namna watakavyoweza kuzungumza na Fifa, vinginevyo ni majanga kwa mabingwa hao watetezi wa ligi ya Tanzania Bara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here