SHARE

NA WINFRIDA MTOI

YANGA inatega mitego kila kona kuhakikisha dirisha dogo linapofunguliwa inakuwa rahisi kuimarisha kikosi chao ili kuondoa mapungufu yanayoonekana hivi sasa.

Dirisha dogo la usajili Tanzania Bara litafunguliwa Desemba 16 mwaka huu na Kamati ya Utendaji ya Yanga inachosubiri ni ripoti ya kocha wao, Charles Boniface Mkwasa, atakapoifikisha mezani.

Kuelekea mchakato huo, inadaiwa maskauti wao wamepiga hodi katika kikosi cha Lipuli wakihitaji saini ya mpachika mabao hatari wa timu hiyo, Daruweshi Saliboko.

Hadi sasa katika orodha ya wafungaji, Saliboko ana mabao sita akifukuzana na kina Meddie Kagere mwenye mabao nane na Paul Nonga aliyefunga mabao saba.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Lipuli ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema huenda baadhi ya nyota wao wanaofanya vizuri wakawakosa kuanzia Januari mwakani.

Alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya timu kubwa  kuanza kuwafuatilia wachezaji wao akiwamo Saliboko anayetakiwa na Yanga kwa udi na uvumba.

“Watu wa Yanga wameanza kumfuatilia mfungaji wetu Saliboko, bado ana mkataba wa miezi sita lakini haitakuwa rahisi kuendelea kubaki kama atatangaziwa dau nono, ukiangalia Yanga ni timu kubwa,” alisema.

Mtoa habari huyo alisema kwa upande wao hawatakuwa na kipingamizi kwa sababu wanajua maisha ya wachezaji wanategemea soka, kinachotakiwa ni kujipanga kuziba mapengo yao.

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dkt. Mshindo Msolla, hivi karibuni aliweka bayana mipango yao ya usajili kuwa itategemea na ripoti ya Mkwasa atakayokabidhi baada ya ligi kusimama.

“Tutasajili dirisha dogo, tunasubiri ripoti ya mwalimu, wachezaji tunaohitaji kipindi hiki ni wale wenye moyo wa kujituma kuipambania Yanga,” alisema Msolla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here