SHARE

EZEKIEL TENDWA NA SAADA SALIM,

UTAKUWA bado unakumbuka jinsi timu ya Taifa ya Ureno ilivyopenya mpaka ikatwaa ubingwa wa michuano ya Euro 2016 mbele ya timu kubwa zilizokuwa zimetabiriwa kutwaa ubingwa huo wakiwamo wenyeji Ufaransa.

Ureno ambayo haikuwa ikipewa nafasi kabisa ya kufika hata hatua ya robo fainali mbele ya timu kama Ujerumani, Hispania, Ufaransa, Ubelgiji, Italia, Uholanzi, Croatia na nyingine, waliuonyesha ulimwengu kwamba soka lina maajabu yake.

Kikosi hicho ambacho kilikuwa chini ya nahodha wao, Cristiano Ronaldo, kilipitia mlango wa nyuma mpaka kutwaa ubingwa huo mbele ya wenyeji wa michuano hiyo Ufaransa ambapo mpaka sasa ni raha tu nchini Ureno.

Unajua ikoje! Yanga wanaburuza mkia kwenye kundi lao A katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na baadhi ya mashabiki wameshakata tamaa lakini hesabu bado zinawabeba mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika kundi hilo, TP Mazembe ya Congo ndio wanaoongoza wakiwa na pointi saba baada ya kushinda michezo yao miwili na kutoka sare mmoja huku Mo Bejaia ya Algeria, wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi tano wakishinda mchezo mmoja na kutoka sare miwili.

Medeama ya Ghana, wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi mbili baada ya kutoka sare michezo miwili huku wakifungwa mchezo mmoja na Yanga wanashika nafasi ya mwisho wakiwa na pointi moja baada ya kupoteza michezo miwili na kutoka sare mmoja.

Kwa sasa kila timu imebakiwa na michezo mitatu ambapo kama Yanga watashinda yote hakuna shaka watavuka na kutinga hatua ya nusu fainali na kuwashangaza wale wote ambao wanadhani safari yao itashia hatua hii ya robo fainali.

Yanga kwa sasa wanajiandaa na mchezo wao dhidi ya Medeama ugenini ambapo wamepania kushinda na kufikisha pointi nne huku wakiwa na uhakika wa kuwafunga Mo Bejaia Uwanja wa Taifa na baadaye kwenda Congo kutafuta pointi nyingine dhidi ya TP Mazembe mchezo wa mwisho.

Hiyo inamaanisha kwamba kama Wanajangwani hao watashinda michezo hiyo watafikisha jumla ya pointi 10 na kutinga hatua ya nusu fainali na baadaye kutinga fainali na kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza kama ilivyo kwa Ureno ilivyofanya Euro.

Kocha mkuu wa kikosi hicho Mholanzi, Hans van de Pluijm, baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Medeama uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, aliweka wazi kwamba hajakata tamaa kwani nafasi bado ipo na lolote linaweza kutokea mbele ya safari.

“Safari haijaishia hapa, bado kuna uwezekano mkubwa wa kushinda michezo yetu iliyobakia na kutinga hatua ya nusu fainali, kilichopo tunaendelea kupambana,” alisema.

Naye winga mwenye kasi kubwa, Simon Msuva, alisema matokeo waliyoyapata katika michezo mitatu iliyopita hawajayafurahia lakini anayo matumaini makubwa kwamba michezo iliyobakia watashinda na kusonga mbele.

Kwa upande wake mshambuliaji wa kikosi hicho Mrundi, Amissi Tambwe, wakati akikabidhiwa tuzo yake ya ufungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mwishoni mwa wiki hii alisema mapambano bado yanaendelea.

“Nafasi bado ipo wazi, tunayo michezo mitatu iliyobakia ambayo kama tukishinda tunaweza kuvuka hatua inayofuata, tunawaomba mashabiki wetu wasivunjike moyo,” alisema kauli ambayo pia ilitamkwa na beki, Juma Abdul, aliyeibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita.

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here