SHARE

SALMA MPELI NA EZEKIEL TENDWA,

KAMA Ndanda FC wataingia kichwakichwa leo Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, bila shaka wanaweza kukumbana na kipigo kikali kutoka kwa Yanga kutokana na hasira walizonazo wana-Jangwani hao.

Hasira za mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara zinatokana na sare ya bao 1-1 waliyoipata dhidi ya African Lyon, katika mchezo wao uliopita na kuwaacha watani zao wa jadi, Simba wakiendelea kutanua kileleni mwa msimamo wa Ligi.

Yanga watakuwa wenyeji wa Ndanda FC katika mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, huku ukitarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na kila timu kuhitaji pointi tatu, hasa ikizingatiwa kuwa huu ni mzunguko wa lala salama.

Jambo la kufurahisha kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba wachezaji wataingia wakiwa na morali ya hali ya juu, baada ya kupewa chao na kuila sikukuu ya Krismasi kwa raha, wakiondokana na yale mawazo ya kugoma kufanya mazoezi kwa siku mbili mfululizo.

Lingine kubwa ni kwamba, kwa sasa kikosi hicho kimekamilika kila idara baada ya Donald Ngoma ambaye aliukosa mchezo uliopita dhidi ya African Lyon kutokana na kuwa na kadi tatu za njano, leo atashirikiana na wenzake, hasa kwenye safu ya ushambuliaji kuhakikisha wanafunga mabao mengi iwezekanavyo.

Yanga wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 37 nyuma ya watani zao wa jadi, Simba, wanaoongoza wakiwa na pointi 41, hivyo mabingwa hao watetezi wanatarajiwa kupambana iwezekanavyo ili kuondoka na pointi zote tatu leo.

Katika hatua nyingine, mashabiki wa timu hiyo wameliomba benchi lao la ufundi kuhakikisha kiungo wao ‘mkata umeme’ Justin Zulu, waliyemsajili kutoka Zesco ya Zambia anapangwa.

Mpaka sasa Yanga wamecheza michezo miwili ya mzunguko wa pili dhidi ya JKT Ruvu na African Lyon, lakini kiungo huyo hakupata nafasi na sasa mashabiki wanataka apangwe ili waone uwezo wake.

Shabiki wa Yanga aliyejitambulisha kwa jina la Edson Hawanga alisema: “Mpaka sasa hatujauona uwezo wake (Zulu) hivyo tunaliomba benchi la ufundi limpe nafasi kesho (leo) ili angalau na sisi tuone nini anacho mguuni kwake.”

Katika mchezo huo Yanga itawakosa wachezaji wake watatu kutokana na matatizo mbalimbali, ikiwamo majeraha ambao ni Matheo Antony, Beno Kakolanya na Malimi Busungu, ambao hata kwenye mechi iliyopita hawakuwepo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here